Tuesday 3 October 2017

JPM ATEMA NYONGO




RAIS Dk. John Magufuli ametumia saa moja, dakika 57 na sekunde 24, kutema nyongo, akielezea vitendo vya ufisadi na ubadhilifu wa mali za umma, vilivyokuwa vikifanyika nchini.
Amesema, uwajibikaji mbovu wa baadhi ya viongozi wa umma waliojiendekeza kwenye maslahi binafsi, umechangia wananchi kutonufaika na rasilimali zilizopo.
Dk. Magufuli ameeleza kwamba, hawezi kuwasaliti Watanzania kwa kutosema ukweli na kwenye vita ya uchumi aliyoianzisha, hakuna wa kumzuia.
Akizungumza jana, Dar es Salaam, kwenye Mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa nchini (ALAT), Rais Magufuli alisema, licha ya wingi wa rasilimali zilizopo, taifa halijanufaika.
Alisema serikali yake imelazimika kuchukua hatua za makusudi katika kulinda rasimali zilizopo, akitolea mfano mafanikio ya muda mfupi yaliyopatikana baada ya kudhibiti biashara ya madini ya Tanzanite.
“Tulipozuia katika siku chache, uzalishaji wa Tanzanite umekuwa zaidi ya mara 30. Kuna siku zilipatikana kilo zaidi ya 18, haijawahi kutokea tangu Tanzanite ianze kuchimbwa.
“Ni vita kubwa, lakini kwa pamoja tutashinda. Tanzania imenufaika na asilimia tano tu, huku asilimia 97 ya fedha zilizopatikana kwenye Tanzanite, zikinufaika katika mataifa mengine,” alisema.
Alisema tangu biashara ya madini ianze kudhibitiwa, kumeibuka malalamiko kutoka kwa watu waliokuwa wakinufaika na wizi huo.
Dk. Magufuli alibainisha kwamba, wakati hayo yakitokea, kundi kubwa la Watanzania, wamekuwa wakitaabika kwa umasikini uliotopea, wakati mali zinazoibwa ni za matrilioni ya shilingi.
“Tumechezewa vya kutosha na ndiyo maana nayasema haya hadharani. Nataka niwahakikishie, katika awamu ya tano chini ya uongozi wangu, hakuna wa kutuchezea.
“Waje wanalia, wanazunguka wakijitahidi kutuchonganisha, hakuna wa kutuchezea. Ni aibu Tanzanite zikasombwa, lakini nchi inayoongoza duniani kwa kuiuza ni Tanzania,” alisisitiza.
Rais alieleza kuwa, maendeleo siyo lelemama kwani wengi wanaolalamika ni wanufaika na mfumo uliokuwepo.
UFISADI BENKI
Katika sekta ya fedha, Rais Magufuli alieleza namna ambavyo vigogo wa benki na serikali walivyokuwa wakijinufaisha kwa fedha mbalimbali za umma.
Alisema awali, fedha za maendeleo zilizopaswa kupelekwa kwenye maeneo husika, baadhi ya vigogo wa serikali walikuwa wakizihifadhi benki kwenye akaunti maalumu ya akiba.
Alifafanua kwamba, fedha hizo hucheleweshwa kwa kipindi cha miezi sita, kisha kigogo huyo hulipwa riba ya asilimia nne kwa fedha za serikali.
“Baadae serikali inapokosa fedha, inalazimika kukopa fedha zake benki kwa riba ya asilimia 26. Huo ndiyo mchezo uliokuwa ukifanywa.
“Kwa hatua zinazochukuliwa na serikali, hakuna kiongozi yeyote wa benki atakayefurahia,” alisema.
Ili kukabiliana na wizi huo, Rais Magufuli alisisitiza kuwa, fedha zote zikitoka Benki Kuu (BOT), zipelekwe moja kwa moja kwenye eneo husika na asitokee yeyote wa kuzizuia.
“Ziache ziende moja kwa moja, hakuna kuzishikashika. Ndiyo maana fedha za elimu zinakwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya mwalimu mkuu.
“Asitokee wa kuchezea fedha ambazo siyo zake. Hao waliokuwa wakizichezea ndiyo waliokuwa wakifanya mchezo na mabenki,” alisema.
Alibainisha kuwa, kulikuwa na benki zaidi ya 54, zote zikifanya biashara na serikali kupitia Hazina.
Kwa kuwa benki hizo zilikuwa hazikopeshi wananchi wa kawaida kujenga nyumba au shughuli za kilimo, alisema  zilikuwa zikifanya biashara na serikali.
Rais alisema kuna benki ambayo ilijinadi kuwa makao makuu yake ni Tanzania, lakini fedha ilizozihifadhi ni asilimia tano pekee.
“Fedha zingine zote zipo kwenye benki zingine katika visiwa vya Cyprus, lakini kwenye usajili wake, imeandikwa makao makuu yapo Dar es Salaam.
“Benki hiyo ilikuwa ikitakatisha fedha haramu na ilifungiwa nchini Marekani, lakini ilikuwepo nchini kwa miaka mingi na wataalamu wa BOT, hawakuchukua hatua zozote,” alifafanua.
Pia, alieleza kuwa benki ya serikali, ambayo ilipata hasara, bado iliendelea kuongezewa fedha.
Alisema licha ya kupata hasara kwa viwango vya hasi sita, 11 hadi 22, katika vipindi tofauti, iliongezewa fedha huku wafanyakazi na meneja wa benki hiyo wakiendelea kuwepo.
Dk. Magufuli alibainisha kuwa, yote anayoyaelezea, wahusika hawatapendezewa nayo, lakini anayaeleza hayo ili Watanzania waelewe madudu yaliyokuwa yakifanyika serikalini.
WATUMISHI HEWA
Katika mkutano huo, uliohudhuriwa na mameya, madiwani, wakurugenzi na makatibu tawala kutoka halmashauri mbalimbali nchini, Rais Magufuli alitangaza kiama kingine kwa watumishi hewa.
Rais aliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango, kuhakikisha sh. bilioni 38, zilizolipwa kama pensheni kwa watumishi hewa, zinarudishwa.
Alisema watumishi hewa walikuwa wakiigharimu serikali sh. bilioni 19.8, kama malipo ya mishahara kwa mwezi, hivyo kwa mwaka, zaidi ya sh. bilioni 238 zilitumika.
Pia, alisema zaidi sh. bilioni 142.9, zilikuwa zikitumika kulipa mishahara kwa watumishi waliokuwa na vyeti vya kughushi.
“Ukiyazungumza hayo, hawatakupenda maana ndio hao wanaoandika kwenye mitandao. Hata wakiandika najua ni wale 12,000.
“Tanzania ina wananchi milioni 54, kwa hiyo hao 12, 000, wakitukana mimi nafurahi,”alisema.
Rais Magufuli aliwataka viongozi kutoka mamlaka za serikali za mitaa, kushugulikia waliohusika kwenye pembejeo hewa, ambapo zaidi ya bilioni 50, zilibainika kuwa madeni ya kughushi.
Alisema ubadhirifu huo umefanyika kwa kuwaandikisha hata watu waliofariki na wasioweza kulima.
POSHO KWA MADIWANI
Rais Dk. Magufuli pia amesema hatoongeza posho kwa madiwani, kwani kwa sasa kipaumbele cha serikali ni kuwahudumia wananchi.
Alisema kama kuna madiwani wasiokuwa na kazi ya kujiingizia kipato, ni vyema wakajiuzulu.
Kauli hiyo aliitoa kufuatia ombi lililotolewa na Mwenyekiti wa ALAT, Gulamhafidhi Mukadamu, kutaka serikali iongeze posho za madiwani kutoka sh. 350,000 hadi sh. 800,000, kwa mwezi.
“Hebu mjitathimini namna ambavyo, wananchi walivyokuwa na changamoto nyingi. Kuna ulazima wa kuwaongezea posho?
“Ina maana tusijenge barabara, tusinunue dawa, tusipeleke fedha kugharamia elimu bure. Sasa niwaombe kwanza tumuogope Mungu,” alisema.
Alieleza kuwa, madiwani wana wajibu wa kuwatumikia Watanzania, ndio maana wanatakiwa kuwa na kazi nyingine ya kujiingizia kipato.
“Mnapojaza fomu, unaambiwa lazima uwe na kazi maalumu ya kukuingizia kipato. Sasa kama wapo madiwani waliojaza hiyo fomu na hawana kazi ya kujiingizia kipato, wajiuzulu udiwani.
WAKURUGENZI WALEVI
Kwenye mkutano huo, Rais Magufuli hakusita kutoa onyo kwa wakurugenzi walevi, ambao alisema hatosita kuwaondoa.
“Nimepata taarifa za watu watatu au wanne, ambao ni walevi sana. Wale wajihesabu wataondoka.
“Ninazungumza kwa uwazi kama kuna mkurugenzi mlevi, acha kabisa kuigusa pombe pale utakapoiona. Katika kipindi hiki uonekane umejirekebisha,” alisisitiza.
Rais alisema ni lazima kuhakikisha maadili ya nchi yanazingatiwa.
Aliwataka wakurugenzi kudhibiti migogoro inayoikumba halmashauri, ikiwemo ya kisiasa.
Alisema adui siyo vyama vya siasa, bali ni wezi wa rasilimali za nchi, hivyo muhimu kujikita katika kukabiliana na changamoto za wananchi.
“Ninaomba hayo mkayasimamie. Yanapunguza uadilifu na utendaji kazi kwenye halmashauri. Mkaendelee kuwahimiza Watanzania kudumisha amani na uzalendo.
“Nchi zote zilizotajirika, watu wake hawakwepi kodi. Nataka kuwahakikishia Watanzania kila senti itakayotolewa kwa serikali, itatumika ipasavyo,” alieleza.
Pia, Rais Magufuli alitoa rai kwa wakuu wa mikoa nchini, kuiga utendaji kazi unaofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Alisema endapo wakuu wengine wa mikoa wangefanyakazi kama Makonda, wakurugenzi wasingekuwa na jukumu zito la kuhudumia wananchi.
Awali, akimkaribisha Rais, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema serikali itaendelea kusimamia makusanyo ya mapato.
Alizishukuru halmashauri kwa namna zinavyodhibiti mianya ya upotevu wa fedha.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Suleiman Jafo, alieleza kuwa, endapo halmashauri zitashindwa kusimamia rasilimali, nchi haitoweza kupiga hatua za kimaendeleo.
Mwenyekiti wa ALAT, Mukadam, aliipongeza serikali inavyoendelea kutoa ruzuku kwa ajili ya utoaji elimu bure.
Aliiomba serikali kuongeza watumishi mara baada ya wengi kuondolewa, kufuatia kukutwa na vyeti vya kughushi.

No comments:

Post a Comment