Tuesday, 3 October 2017

WALAJI NYAMA HII INAWAHUSU




MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Maghembe, amewatoa hofu wakazi wa jiji hilo, kuhusu uwekezano wa kula nyama zinazohifadhiwa kwa kutumia dawa aina ya formalin, inayotumika kuhifadhi maiti hospitali.
Akizungumza na gazeti hili, jijini Dar es Salaam, juzi, Dk. Grace alisema, dawa hizo haziuzwi madukani kama nyingine, wanachofanya ni kuziagiza kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na kuzisambaza hospitalini kwa ajili ya kutunzia maiti zisiharibike.
Kwa mujibu wa Dk. Grace, dawa hizo zinauzwa kwa bei ghali mno, siyo rahisi kwa mtu wa kawaida kuzinunua na mara nyingi hutumika katika maabara za kisayansi.
Hata hivyo, Dk. Grace alisema, baada ya kupata taarifa hizo, wamezifanyia kazi kwa kuziwasilisha kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), ili ifanye uchunguzi wa kina na kubaini iwapo ni kweli zinatumiwa kufukuza inzi kwenye mabucha ya nyama.
Dk. Grace alikuwa akijibu swali aliloulizwa kuhusu taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa, baadhi ya wamiliki wa mabucha jijini Dar es Salaam, wamekuwa wakitumia dawa hiyo kwa ajili ya kufukuza nzi mabuchani au wanaposafirisha nyama.
Kusambaa kwa taarifa hizo kumeanza kuwapa hofu wakazi wa jiji hilo, ambao baadhi yao wamekuwa wakiogopa kununua nyama kwa kuhofia kuathiriwa na dawa hiyo.
Imedaiwa kuwa, dawa hizo zimekuwa zikipatikana kwenye maduka makubwa yanayouza dawa za binadamu na zinauzwa holela kwa bei nafuu.
Kwa mujibu wa taarifa hizo za mitandao, dawa hiyo inapoingia kwenye mwili wa binadamu, huenda moja kwa moja kwenye ini na kusababisha madhara makubwa kiafya, ikiwemo kifo.
Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam, waliozungumza na Uhuru, wamedai kuwa katika siku za hivi karibuni, nzi wamepungua kwenye mabucha kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Mmoja wa wakazi hao, Juliana Kashoke alidai kuwa, siku za nyuma, kila walipokuwa wakiingia buchani, walikumbana na nzi wengi, lakini siku hizi hawapo.
 “Labda ni kweli wanatumia dawa hizi, lakini serikali inatakiwa kutoa tamko, ambalo litawafanya wananchi wajiepushe kwa maradhi yanayoweza kuwakumba wanapokula nyama yenye dawa hiyo,”alisema.
Aidha, alisema iwapo ni kweli wapo wamiliki wa baadhi ya mabucha wanaotumia dawa hiyo, wachukuliwe hatua kali.
Kwa upande wake, Makundi Jeremiah, alishauri serikali ifanye uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo, kabla halijaleta madhara kwa wananchi.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wengine wa jiji hilo walisema kutokuwepo kwa nzi wengi kwenye mabucha ya nyama, kumetokana na wamiliki kuzingatia usafi.
Mtazamo huo, uliungwa mkono na Dk. Grace, ambaye alisema zipo dawa maalumu za kuua nzi na huenda ndizo zinazotumiwa na wamiliki wa mabucha.
“Tunafanya uchunguzi ili kubaini ukweli wa jambo hilo. Tunasubiri uchunguzi wa TFDA, ambao utatoa taarifa kamili,”alisema.
Alisema taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii haina ukweli wowote, hivyo wanachofanya sasa ni kusubiri uchunguzi wa TFDA, ambao utatoa taarifa kamili kuhusu matumizi hayo mabuchani.
“Taarifa tumezisikia na tunazifanyia kazi, tayari TFDA wanalifanyia uchunguzi jambo hilo kama lina ukweli wowote,” alisema.
Dk. Grace alisema, kuna dawa za kufukuzia inzi ambazo zinauzwa, inawezekana wanazitumia hizo.
Alisema mabucha yanapowekwa katika mazingira ya usafi, kuna uwezekano mkubwa wa kutokuwepo inzi ambao wanazagaa buchani, lakini likiwa chafu ni lazima wawepo.
Mganga Mkuu huyo alitoa wito kwa wenye mabucha, kuweka mazingira yao kwenye hali ya usafi na kuweka mashine za kisasa za kukatia nyama na kuacha kutumia miti.
Ofisa Habari wa TFDA, Gaudencia Simwanza, alisema kwamba, huo ni uvumi na haujathibitishwa, hivyo wanaendelea na uchunguzi wa suala hilo.
Baadhi ya wauza nyama katika soko la Kisutu, walisema usafi wa mazingira katika maeneo yao ya kazi, ndiyo yanayosababisha kutokuwepo kwa inzi.
Walikiri kwamba, zamani inzi walikuwa wakirandaranda kwenye mabucha kutokana na mazingira waliyokuwa wanafanyia kazi, kwani hakukuwa na feni wala kiyoyozi ambacho kina uwezo mkubwa wa kufukuza inzi.
Mmoja wa wauzaji wa nyama katika soko hilo, ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema hawatumii dawa yoyote ya kuwafukuza inzi, bali wameboresha mabucha yao kwa kuweka viyoyozi na feni  ili wasiweze kutua au kuzagaa ovyo.
“Unajua huu ubaridi inzi hawawezi kukaa, ndio maana baadhi yao unawaona ukutani, hivyo feni na kiyoyozi, inzi hawawezi kukaa hata siku moja,”alisema.
Alisema  hakuna mfanyabishara anayetumia dawa ya kutunzia maiti kwenye nyama wala dawa nyingine yoyote.
Kwa upande wake, muuza mnyama mwingine sokoni hapo, alisema hawawezi kuweka dawa hiyo kwenye nyama wakati wao na familia zao wanakula.
“Unajua hata mimi na kula nyama, halitakuwa jambo jema  kuweka dawa hiyo kwenye nyama, ingawa familia yangu nayo ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa nyama,”alisema.

No comments:

Post a Comment