MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha
UPDP, Fahmi Dovutwa, ameipongeza
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwaengua wagombea wa uenyekiti wa wilaya nne na
kusema kwamba, kama mtu sio kada, ni muasi hafai kuwa kiongozi.
Amesema uamuzi uliofanywa na CCM
ni wa kuigwa na vyama vingine vya siasa nchini, kwa sababu uongozi ni lazima
apewe mtu ambaye ni kada.
Dovutwa alitoa kauli hiyo jana,
alipozungumza na gazeti hili kuhusu uamuzi uliochukuliwa na NEC, wa kuwaengua
wagombea hao, kutokana na kasoro za maadili zenye viashiria hatarishi kwa
Chama.
Alisema kila chama kina utaratibu
wake wa kuwapata wagombea, hivyo haijarishi wilaya nne kuenguliwa na hata
ingekuwa mkoa.
Mwenyekiti huyo alisema hatua ya
CCM kuwaengua wagombea wa wilaya nne ni wa kuigwa na vyama vyote vya kisiasa
nchini.
Kwa mujibu wa Dovutwa, uongozi wa
chama ni lazima apewe mtu ambaye ni kada, siyo muasi, hivyo huyo hafai kuwa
kiongozi na hilo siyo la CCM, bali ni la vyama vyote nchini.
“Kama mikoa wanaonyesha kuna uasi,
hauwezi kuendelea na waasi. Mwanachama wa chama sawa sawa na askari, kama
askari ana ndimi mbili hafai kuwa askari,”alisema.
“Kama wenyewe wameona wanachama
hao wameasi, wapo kinyume na chama, nadhani kwa utaratibu wa chama wapo sahihi,
kwani kila chama kina utaratibu wake,”alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Taifa wa Chama cha TLP, Augustine Mrema, alisema CCM imefanya jambo zuri
kuwaengua wagombea hao, kwani imeona
haiwezi kuendelea na wanachama, ambao hawana viwango na sifa.
Mrema alisema uamuzi uliofanywa na
Chama una nia njema ya kukijenga katika misingi ya maadili.
Mwishoni mwa wiki iliyopita,
akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kumalizika kwa mkutano wa NEC,
ambao ulipitisha majina ya wagombea wa uenyekiti wa katika wilaya nchini,
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, alisema wagombea hao walienguliwa katika wilaya nne.
Alizitaja wilaya hizo kuwa ni Moshi
Mjini, Siha na Hai zote za mkoa wa Kilimanjaro na Makete mkoani Iringa. Alisema
uchaguzi katika wilaya hizo utatangazwa tena.
Pia, uchaguzi kwenye wilaya ya
Musoma utatangazwa baadaye, baada ya Halmashauri Kuu kuamua kuundwa kwa wilaya
mpya mbili za kichama , ambazo ni Musoma Mjini na Musoma Vijijini.
Alisema wagombea waliopitishwa
kushiriki uchaguzi huo wanapaswa kuzingatia kanuni za uchaguzi, uongozi,
maadili na katiba ya CCM.
Polepole alisema wagombea
watakaoshindwa kuzingatia maadili, Chama kitawachukulia hatua, ikiwemo
kuwafukuza uanachama.
No comments:
Post a Comment