Monday, 2 October 2017

TUNAWASHANGAA WANAOMBEZA RAIS MAGUFULI




CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimesema kuzungumzia maendeleo ya demokrasia peke yake bila kuwekwa mkazo wa uzalishaji mali kwa ajili ya uchumi, hakuna tija.
Kimesema siasa pekee haina ubavu wa kuleta mabadiliko yanayoweza kuwaondolea wananchi dhiki, unyonge na umasikini, hivyo kuwashangaa wanaobeza juhudi za Rais Dk. John Magufuli.
Mwenyekiti wa ADC Taifa, Hamad Rashid Mohamed, aliyasema hayo katika mahojiano na Uhuru, makao makuu ya chama hicho, yaliyoko Bububu, Mkoa wa Mjini Magharubi, Unguja.
Hamad alisema, ikiwa hakuna utashi au nia njema kwa kila upande, hususan upinzani na ule unaotawala, ni kazi bure kujigamba kuwa, nchi inaheshimu demokrasia ya kweli wakati wananchi wake bado ni wanyonge na maskini.
Alisema kwa upande mmoja, upinzani umekuwa ukiutupia lawama utawala, lakini cha ajabu hata pale wapinzani  wanapopata nafasi ya kuongoza serikali, baadhi yao huvunja misingi ya demokrasia kwa kubadili katiba za nchi zao ili kukataa kuondoka madarakani.
Akitoa mfano, alisema aliyekuwa Rais wa Malawi, Bakili Muluzi na Rais Pier Nkurunziza wa Burundi, wamehusika na mchakato wa kubadili katiba za nchi zao ili waendelee kubaki madarakani wakisahau kuwa, wao walitoa madai ya kupigania demokrasia iheshimiwe.
"Utashi wa kisiasa na nia njema, vinahitajika kwa pande zote mbili, kwa vyama tawala na vile vya upinzani. Demokrasia kupewa nafasi kubwa bila kuweka mkazo wa kujiletea maendeleo na kujijenga kiuchumi, huo ni sawa na upuuzi usiokadirika,"alisema.
Aliyataja mataifa kama China, Taiwan, Dubai, Oman, Malaysia na Hong Kong kuwa, hakuna madai ya vyama na demokrasia, lakini mataifa hayo yamepiga hatua kubwa kimaendeleo katika uchumi huku wananchi wake wakiishi maisha bora kuliko zile zinazojidai ni waumini wa demorasia .
"Maendeleo ya demokrasia hupatikana ikiwa wote mna utashi wenye mizania sawa. Nawashangaa wanasiasa wanaombeza Rais Dk. John Magufuli, anapohimiza watu kufanyakazi, uzalishaji na ujenzi wa  viwanda. Siasa na demokrasia siyo msingi unaobadili maisha ya jamii na kuwatoa katika umaskini," alisema.
Alisema mataifa yaliyoendelea kiuchumi hayashabikii siasa baada ya kumalizika uchaguzi na viongozi wake wa kisiasa huwa tayari kumaliza matatizo yatokanayo na dosari ndogo ili kulinda usalama wa watu na kutaka wafanye kazi za uzalishaji mali.
"AL Gore alikubali yaishe kwa George W Bush, Hillary Clinton naye alifunika kombe baada ya matokeo kujaa aina ya utata na Rais Donald Trump. Marekani sasa inasonga mbele huku watu wake wakiwa na maisha bora yasiyo na unyonge wala  umaskini,"alisema.
Hamad, ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Maliasili wa Zanzibar, alisema ipo haja kwa viongozi wa kisiasa na serikali kuumwa na umaskini wa watu, watoto kutopata elimu bora, wakulima, wavuvi na wafugaji kukosa zana za kisasa kuliko madai ya demokrasia.
"Unapigania maendeleo ya demokrasia huku hospitali zenu  hazina dawa, huduma duni za  tiba na ukosefu wa vifaa tiba. Kiongozi unapoumwa unatibiwa nje kwa kodi za wananchi masikini halafu unasimama na kusema unapigania haki na usawa,"alisema Hamad.

No comments:

Post a Comment