Monday, 2 October 2017

BIL. 168/- KUTUMIKA KUBORESHA ELIMU YA UALIMU




NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Profesa Simon Msanjila, amesema kuwa serikali inatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 168, katika kutekeleza mradi wa kuboresha elimu ya ualimu hapa nchini.
Profes Msanjila, aliyasema hayo jana, wakati akifungua mkutano wa wadau wa elimu, uliofanyika mjini hapa na kusema kuwa, lengo la mkutano huo ni kuwasilisha taarifa ya mahitaji ya vyuo vya ualimu vya serikali vinavyotoa mafunzo ya stashahada na astashada.
Alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Canada na kwamba, ulianza kutekelezwa Machi, mwaka huu na utatekelezwa  kwa kipindi cha miaka mitano.
“Mradi huo ambao umeanza tangu mwezi Machi, mwaka huu, una lengo la kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika vyuo  vya ualimu vya serikali ili kuandaa walimu bora wa ngazi zote, kuanzia ngazi ya chini hadi ngazi za juu,”alisema Profesa Msanjila.

Aliwataka wadau hao kutumia siku mbili za mkutano huo kuyafanyiakazi watakayoyajadili ili kufanikisha malengo ya mradi huo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo ya Ualimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Basiliana Mrimi, alisema mradi huo ni  katika miradi mingi na uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, unaofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa maedeleo, ikiwemo Serikali ya Canada, ambayo ni mdau mkubwa katika uwekezaji  kwenye sekta ya elimu.
Alisema maeneo ambayo yataguswa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya vyuo  vyote 35 vya ualimu vya serikali, upatikanaji wa vifaa vya ufundishaji na ujifunzaji na kuboresha mtaala wa elimu ya ualimu.
Alisema ili mtaala utekelezeke, wafukunzi wa vyuo vya ualimu watafanyiwa mafunzo ya mtaala mpya ili wakautekeleze kwa ufanisi.
Alisema katika mwaka huu wa fedha, serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imejipanga kuwekeza kwenye miundombinu ya elimu, kuanzia ngazi ya chini kabisa mpaka vyuo vikuu.
“Lakini pia Serikali na wadau wa maedeleo katika mwaka huu wa fedha, itaimarisha miundombinu ya vyuo vikuu kwa lengo la kuboresha utoaji wa elimu ngazi ya vyuo vikuu.”alisema Mrimi

No comments:

Post a Comment