MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewatia hatiani
vigogo wawili wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan Trade) na
kuwapa adhabu ya kulipa faini ya sh. milioni 20, kila mmoja na iwapo
watashindwa, watatumikia kifungo cha miaka mitatu.
Washitakiwa waliopewa adhabu hiyo ni Mkurugenzi wa
Utafiti na Mipango wa mamlaka hiyo, Samweli Mvingira na Naibu Mkurugenzi wa Fedha
na Utawala, Judith Msuya, ambao walitiwa hatiani kwa makosa manne ya matumizi
mabaya ya madaraka.
Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita
na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha, baada ya kusikiliza
ushahidi wa pande zote husika.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkeha aliwatia hatiani
washitakiwa hao katika mashitaka manne, kutokana na upande wa jamhuri kuweza
kuthibitisha mashitaka dhidi yao pasi na kuacha shaka yoyote.
Hata hivyo, Hakimu Mkeha aliwaachia washitakiwa hao
katika shitaka la tano, kwa kuwa upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha
mashitaka pasi na kuacha shaka.
Akitoa adhabu, Hakimu Mkeha alisema kila mshitakiwa katika shitaka la kwanza hadi la nne kwa kila kosa, atalipa faini ya sh. milioni tano, akishindwa atakwenda jela miaka mitatu.
Hakimu Mkeha alisema, kesi hiyo ilikuwa na
washitakiwa watatu, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Tan Trade, ambaye alifariki
dunia wakati shahidi wa kwanza alipotoa ushahidi.
Washitakiwa hao baada ya kupewa adhabu hiyo,
walipelekwa gerezani kutokana na kushindwa kulipa faini, ambapo jana,
alionekana mahakamani hapo ndugu wa Judith, akiwa ameleta risiti aliyolipia
faini ya sh. milioni 20.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao
wanadaiwa kati ya Septemba, 2007 na Julai, 2008, katika makao makuu ya Tan
Trade, yaliyoko wilayani Temeke, Dar es
Salaam, walitumia madaraka yao vibaya kwa kuagiza gari lililotumika kinyume cha
Sheria ya Manunuzi ya Umma, hivyo kusababisha AL Hamadi Motors FZD kupata faida
ya sh. 34,895,400.
Pia, walikuwa wakidaiwa tarehe hiyo na mahali hapo,
walitumia madaraka yao vibaya kwa kununua gari lililotumika kwa lengo la
kumnufaisha Humer Stars sh. 32,773,475.
Washitakiwa hao walikuwa wakidaiwa bila kufuata utaratibu wa kushindanisha
zabuni, waliagiza gari lililotumika na kusababisha AL Hamad kupata faida ya sh.
34,895,400.
Shitaka la nne, walikuwa wakidaiwa kukunua magari
hayo bila ya kufuata utaratibu wa zabuni.
Shitaka la tano lililokuwa likiwakabili washitakiwa
hao ambalo mahakama iliwaachia huru, walikuwa wakidaiwa kutumia madaraka yao
vibaya, uzembe na kumsababishia mwajiri wao kupata hasara ya sh. 49,145,855.05.
No comments:
Post a Comment