Monday, 2 October 2017

WATOA RUSHWA UCHAGUZI WA CCM WILAYA KUFYEKWA


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakuna atakayebaki salama, endapo itathibitika mgombea ametumia fedha kutoa rushwa kwa wapigakura ili ashinde uchaguzi.
Kimesema ikibainika hivyo, CCM itafuta matokeo na kuchukua hatua kwa muhusika
Pia, kimepiga marufuku vikao visivyo halali vya ngazi za matawi, kata hadi wilaya, vinavyotumika kuweka misimamo ya makundi au safu za watu maarufu na kwamba, wameomba vyombo vya ulinzi vifuatilie na kuwatia mbaroni wahusika.
Kimesema kinafuatilia harakati za wagombea wa ngazi ya wilaya walioteuliwa juzi na kwamba, endapo itabainika mgombea ameshinda kwa njia ya rushwa kwa wajumbe, Chama kitafuta uchaguzi na kumuondoa kwenye orodha ya wagombea.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula, alisema hayo jana, alipozungumza na Uhuru, kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa ngazi ya wilaya, unaotarajiwa kufanyika Alhamisi wiki hii, katika maeneo mbalimbali nchini.
“Zipo taarifa katika baadhi ya maeneo, watu wanakaa vikao kuweka misimamo ya safu zao, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu na kanuni za uchaguzi.
“Wengine wanazunguka kufanya kampeni na kutoa rushwa ili wachaguliwe, nao tunapata taarifa zao,”alisema.
Mangula alisema, Kamati ya Usalama na Maadili ipo kazini na tayari imeshabaini kasoro katika baadhi ya maeneo, likiwemo jiji la Dar es Salaam, ambapo kuna watu wameanza kukusanyana na kufanya vikao vya hovyo kwa ajili ya kupanga safu.
Alisema, CCM imedhamiria kupata wagombea bora, watakaoshinda uchaguzi bila kutumia fedha kuwarubuni wapigakura, kwa kuwa uzoefu unaonyesha wanaotumia fedha ni wale wasio na uwezo wa kushinda kwa sifa za uongozi.
“Tunatumia vyombo vyetu kufuatilia nchi nzima na tumeomba vyombo vingine vya usalama vifuatilie kwa kuwakamata wahusika wanaotoa rushwa kwenye uchaguzi. CCM inatakiwa kuonyesha mfano kwa kuwa Ilani yake inapiga vita suala la rushwa,”alisema.
Akizungumzia kuhusu watendaji wa CCM, Mangula alisema makatibu wa mikoa na wilaya, watakaojihusisha na upangaji safu kwa kutoa maelekezo kwa wapigakura ili achaguliwe mtu fulani, watakuwa ‘wamekalia kuti kavu’.
Alisema watendaji wanatakiwa kusimamia uchaguzi kwa haki na kufuata kanuni na utaratibu, badala ya kuwashinikiza wapigakura ili kupata viongozi wanaotakiwa na makundi ya viongozi kwa maslahi yao na wengine kupanga safu za uchaguzi mkuu 2020.
“Watendaji wanapaswa kufanyakazi yao kama refarii kwa kuhakikisha wanatenda haki kwa kila mgombea na kwa kila mwanachama, badala ya kupendelea mtu ama kundi fulani. Mtendaji atakayebainika, atakuwa amejiondoa mwenyewe,”alisema.
Katika hatua nyingine Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM, alisema zipo taarifa za watumishi wa serikali waliogombea na kushinda kwenye uchaguzi wa CCM na jumuia zake, jambo ambalo ni kinyume na maelekezo ya Chama.
“Kama kuna mtumishi wa serikali amepenya kwenye nafasi yoyote, ni vema akachagua kuacha kazi serikalini na kubaki kuwa mjumbe au kiongozi kwenye Chama. Tulishatoa maelekezo, lakini baadhi ya watendaji hawakulisimamia vema suala hilo, hivyo ni vyema makada hao wakajitoa wenyewe,”alisema.
Mangula alisema CCM inaongozwa na katiba, kanuni na miongozo, hivyo lazima izingatiwe na katika maboresho yanayoendelea ndani ya Chama ili kuhakikisha kinarejesha heshima na misingi yake.
Aliwaonya wanachama, wakiwemo wajumbe wa mikutano mikuu ya wilaya, kuwa makini na wasikubali kuburuzwa na viongozi wanaowalazimisha kuweka misimamo  kwenye uchaguzi wa wilaya.
Jumamosi iliyopita, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, ilipitisha na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea wa nafasi za uongozi wa ngazi za wilaya, ambapo iliwaengua wagombea wa nafasi za uenyekiti kwenye wilaya nne.
Akitoa taarifa baada ya kikao hicho, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey  Polepole, alisema NEC ilijadili majina zaidi 1,400 na kufanya uteuzi wa wagombea.
Katika taarifa hiyo, Polepole alisema wagombea walioteuliwa kuwania nafasi za uongozi ngazi ya wilaya, wanapaswa kuzingatia maadili ya Chama, watakapokwenda kinyume, watachukuliwa hatua, ikiwemo kufukuzwa.
Polepole alitaja wilaya ambazo wagombea wake wameenguliwa kuwa ni  Moshi Mjini na  Siha mkoani Kilimanjaro, Makete mkoani Iringa na wilaya ya Musoma mkoani Mara, ambapo uchaguzi utatangazwa baada ya NEC kuamua kuigawa wilaya hiyo kuwa na wilaya mbili za kichama, yaani Musoma Mjini na Vijijini.

No comments:

Post a Comment