Monday 2 October 2017

KIKWETE ATEMBELEA SHULE ALIYOSOMA KIBAHA


RAIS mstaafu Jakaya Kikwete amewasihi wadau na viongozi waliosoma Shule ya Sekondari Kibaha, kuangalia namna ya kutatua changamoto ya uhaba wa madarasa, ambayo inasababisha mlundikano wa wanafunzi madarasani.

Amesema mbegu ya kuwa yeye mwanasiasa ilipandwa shuleni hapo, baada ya kuchaguliwa kuwa kiongozi wa baraza la shule, kutokana na harakati zake za kutetea haki za wanafunzi.

Kikwete aliyasema hayo jana, katika ukumbi wa Shirika la Elimu Kibaha, wakati wa mahafali ya 50 ya wanafunzi wa kidato cha nne wa shule hiyo, ambayo alipata elimu yake ya sekondari kuanzia mwaka 1966 hadi 1969.

Alisema atashirikiana na wadau mbalimbali kuona namna bora ya kusaidia kupunguza au kuondoa tatizo la upungufu wa madarasa.

Rais mstaafu Kikwete alisema, haipendezi na hajafurahishwa na hali ya miundombinu ilivyo chakavu, jambo linaloathiri mazingira ya kujifunza na ufundishaji.

Alieleza kuwa, changamoto hizo siyo sababu ya kushindwa, bali uwepo wa changamoto huongeza umakini, bidii na ubunifu ili kufika mahala pazuri zaidi.

Hata hivyo, alifurahi kusikia serikali imejidhati kukarabati shule kongwe nchini, ikiwemo Shule ya Sekondari Kibaha.

"Vuteni subira, maana kulingana na kasi ya awamu ya tano, naamini ukarabati huo hautachelewa,"alisema.

Alisema Shirika la  Elimu Kibaha ni chemchemi ya elimu bora iliyozaa viongozi bora na wataalamu wanaoliletea sifa taifa.

Kikwete alisema shirika hilo ni tunu muhimu iliyoachwa na muasisi na Baba wa Taifa  Mwalimu Julius Nyerere, kwa kushirikiana na nchi za Nordic.

"Jamii ya Watanzania inaendelea kushuhudia matokeo mazuri ya shule ya sekondari Kibaha katika mitihani ya kitaifa kwa kidato cha nne na cha sita.

"Pia, ushindi na tuzo katika nyanja zingine na mafanikio kwa wanajumuia ya shule hii ni ushahidi tosha kwamba, shirika hili ni chemchemi ya elimu bora iliyozalisha wanasiasa, madaktari, maprofesa, wataalamu na viongozi wa juu,"alifafanua.

Kuhusu miradi ya uzalishaji kwenye shirika hilo, alisema ni wazo la kufanyiwa kazi kwani itawasaidia kuwajengea vijana moyo wa kupenda kazi za mikono na kuwa  mtaji.

Kikwete aliwatakia mafanikio mema wahitimu, hususan katika mtihani wa kidato cha nne kitaifa, unaotarajiwa kuanza Oktoba 30, mwaka huu.

Kabla ya shughuli ya mahafali hayo, Kikwete alipata fursa ya kutembelea bweni alilokuwa akilala, maktaba, maabara na maeneo mengine shuleni hapo.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Elimu Kibaha, Profesa Patrick Makungu, alisema shirika linakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu na vifaa vya kufundishia fani  za ufundi.

Alieleza kuwa shirika hilo ni taasisi ya huduma iliyoanzishwa miaka 54, iliyopita na jukumu lake kubwa ni kupigana ili kuwashinda maadui ujinga, maradhi na umasikini.

Profesa Makungu alisema mkakati wao ni kuhakikisha wanatoa wanafunzi na wanavyuo wenye maarifa, ujuzi na nidhamu katika elimu ya msingi, sekondari, ufundi stadi, mafunzo kwa maofisa tabibu na uuguzi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha, Chrisdom Ambilikile, alisema shule hiyo ipo vizuri kitaaluma baada ya kufanya vizuri kwa miaka 13 mfululizo.

Alisema mwaka jana, walipanda kwa ufaulu kitaifa, kufikia nafasi ya 16 kutoka ya 69 na kwa mwaka huu, wanatarajia kupanda zaidi.

Ambilikile alisema miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na upungufu wa madarasa matano, ambao unasababisha mlundikano wa wanafunzi katika vyumba vichache vilivyopo .

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1965, kwa msaada wa kifedha kutoka nchi za Nordic, ikiwa na wanafunzi 110. Kwa sasa ina wanafunzi 728, wote  wakiume, walimu 57. Wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne kwa mwaka huu ni 116.

No comments:

Post a Comment