Monday 2 October 2017

MAJALIWA AAGIZA WANAOVURUGA AMANI WAFICHULIWE

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaomba viongozi wa jumuiya na taasisi zote za dini nchini, kuhakikisha zinawapiga vita watu wanaopanga kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini, kwa sababu watakwamisha maendeleo.

Amesema serikali inaelewa kwamba, dini ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya maendeleo ya ustaarabu wa mwanadamu, kwani inatoa elimu ya maadili mema yenye kuwafanya waumini waepuke maovu mbalimbali.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana, wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa 48, wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya, uliofanyika katika eneo la Kitonga, Kata ya Msongola, wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Alisema kila Mtanzania anatakiwa kuhakikisha anadhibiti matukio yote yenye viashiria vya uvunjifu wa amani, kwa kutoa taarifa katika mamlaka husika.

”Tanzania ni nchi salama na yenye utulivu, hivyo ni lazima wote tushirikiane kuitunza. Napenda niwahakikishieni kuwa, serikali inaunga mkono juhudi za jumuiya za kidini katika kupiga vita maovu ya kila aina; mathalan utumiaji dawa za kulevya, wizi, rushwa na uzinzi, ambao husababisha madhara mengi ukiwemo ugonjwa wa ukimwi,”alisema.

Alisema iwapo dini zitatumika vizuri, itawezekana kwa haraka kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli  la 'Hapa kazi tu', kwani kila mtu ataepuka uzembe na kuwajibika ipasavyo.

Waziri Mkuu alisema ana imani kwamba, jumuia hiyo kama zilivyo taasisi zingine za kidini, itaendeleza kazi kubwa ya kupambana na maovu katika jamii kwa kuwapatia waumini wake na wananchi kwa ujumla, elimu na maarifa ya kuboresha tabia zao na maadili yao kiroho.

Alisema amani na utulivu uliopo nchini, unatokana na mambo mengi, ikiwemo ustawi wa wananchi, kuweza kufanya shughuli zao vizuri na kuwa na imani na serikali, ambayo imejiwekea mikakati ya kuhakikisha wananchi, hususan wanyonge, wanapata faraja ndani ya nchi yao.

Waziri Mkuu alisema mambo hayo yameweza kupatikana baada ya serikali kupambana na rushwa na ufisadi pamoja na kuimarisha maadili ya watumishi wa umma, ambayo yamekuwa chanzo cha kupotea kwa amani na utulivu katika baadhi ya nchi.

“Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kupambana na ufisadi, kupitia mikataba mibovu na kuimarisha maadili ili kujenga imani kwa wananchi, kuondoa migongano na tofauti ya kipato, kuwa na matumizi mazuri ya rasilimali za umma, kuleta tija kwa kuongeza thamani ya huduma na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato,”alisema.

Awali, Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuia ya Waislamu Waahmadiyya Tanzania, Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry, alisema jumuiya hiyo imekuwa ikifanya mikutano kila mwaka, kwa lengo la kukumbushana misingi sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu na kukuza undugu wao.

Sheikh Chaudhry alisema mkutano wa mwaka huu, umejumisha watu zaidi ya 4,000, kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, na wageni kutoka nchi za Uingereza, Canada, Rwanda, Uganda, Ujerumani, Kenya, Burundi, Malawi na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Alisema jumuiya hiyo mbali na masuala ya kidini, pia inatoa huduma mbalimbali za kijamii kama elimu, maji na afya kwenye mikoa mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment