Monday 2 October 2017

MWINYI: NI FEDHEHA KWA NCHI VIKONGWE KUENDELEA KUUAWA


RAIS mstaafu Ali Hassan Mwinyi, amesema anasikitika kuona mauaji ya vikongwe yaliyomfanya ajiuzulu uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi miaka ya 1970, yakiendelea na kwamba, hiyo ni fedheha kwa Tanzania.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya 'Siku ya Wazee Duniani', jana mjini hapa, Mzee Mwinyi alisema hakuna haja tena kwa sasa kiongozi kujiuzulu kutokana na mauaji, bali serikali inapaswa kupambana na wauaji wote ili kutoruhusu hali hiyo kuendelea.

Mwaka 1976, akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, Mzee Mwinyi alilazimika kujiuzulu nafasi yake, baada ya kutokea mauaji katika mkoa wa Shinyanga, lakini miaka tisa baadae, aliteuliwa kuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda, ambapo aliiongoza nchi kwa miaka 10.

"Sababu za kujiuzulu kwangu uwaziri wa mambo ya ndani ya nchi, kulitokana na kulinda heshima ya taifa,"alisema.

Alifafanua kuwa, kuongezeka kwa wazee ni jambo jema, linaloonyesha taifa linapata maendeleo, lakini kuwaua vikongwe ni aibu na fedheha kubwa na alitaka tabia hiyo ikomeshwe.

Rais mstaafu Mwinyi alisema vyombo vya habari vina jukumu kubwa  la kutoa elimu kwa watu wenye tabia ya kuuwa vikongwe nchini na kuongeza kuwa, wakati wote atalia navyo anapoona havitekelezi jukumu hilo kikamilifu.

Hata hivyo, alisema kwa sasa hali inaonekana kuwa imetulia kutokana na mauaji ya vikongwe kupungua, lakini bado anasikitishwa kuona hata mzee mmoja akiuawa.

Aliiomba serikali kutunga haraka sheria ya wazee ili iwalinde, badala ya kutegemea sera na kauli katika utoaji huduma, ambazo mwisho huishia kwenye makaratasi.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika ya Wazee, Sebastian Bulegi, alimtwisha jukumu Mzee Mwinyi, kumwomba afikishe maombi kwa Rais Dk. John Magufuli kuhusu mambo manne.

Bulegi aliyataja mambo hayo kuwa ni sheria itakayoendana na Sera ya Wazee ya mwaka 2003, huduma bora bila malipo kutokana na wazee kusumbuliwa, mauaji ya kikatili na malipo ya pensheni kwa kuwa hivi sasa, wanaolipwa ni asilimia nne na ni waliokuwa watumishi wa umma.

Bulegi pia alisisitiza suala la uwakilishi katika vyombo vya uamuzi, ikiwemo bunge, ambapo alisema wakipewa nafasi, watakuwa na mchango mkubwa wenye maslahi kwa taifa.

Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema serikali imetoa kipaumbele kwa wazee na haitasita kuwahudumia kila inapobidi.

Ummy alisema hadi sasa wazee 135,415, wametambuliwa na zaidi ya wazee 200,000, wamepatiwa vitambulisho vya bima.

Akizungumzia huduma kwa wazee, alisema serikali inapeleka kila mwezi fedha katika kambi 17 za wazee, huku ikiwa imeshanunua bajaji 10, kwa ajili ya kuwahudumia, ikiwemo majiko matano ya kupikia.

Wakati huo huo, Wilayani Ilala, Dar es Salaam, serikali imewapiga marufuku walimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, kuwatoza wazazi fedha za chakula na masomo ya ziada, baada ya kumalizika kwa vipindi.

Imesema wale watakaofanya hivyo, watawachukulia hatua kali, ikiwemo kuondolewa kazini.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa wilaya hiyo, Sophia Mjema, wakati wa maadhimisho hayo, ambayo kiwilaya yalifanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Sophia alisema ni marufuku kwa walimu kuwatoza wazazi fedha za chakula na masomo ya ziada na kuwataka pale watakapokumbana na kadhia hiyo, watoe taarifa ili waweze kuwachukulia hatua za kinidhamu.

“Mtoto wako hajaleta fedha ya tuisheni, mtoto hajaleta fedha ya chakula, mtoto hajaleta nini, ninasema marufuku. Kuna wazee ndio wanaolea watoto kule nyumbani, kuna wazee ndio wanaopeleka watoto kule hospitali.

“Ukishamwambia huyu mzee jambo hili, hawezi tena kwa sababu nguvu inamwishia na nauli ya kuja kila siku kulalamika hana na mtoto anabakia nyumbani,”alisema.

Mkuu huyo wa wilaya alisema, serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, ilishatangaza kwamba, elimu ni bure, hivyo walimu waache tabia ya kuwatoza fedha wazazi.

Alisema wazazi watakaokumbana na kadhia hiyo, watoe taarifa ili  mwalimu aliyefanya hivyo achukuliwe hatua na kuondolewa.

Sophia alisema wazee hawapaswi kusumbuliwa kwa sababu waliisaidia nchi katika mambo mbalimbali ili kuhakikisha kunakuwa na amani, hivyo serikali inatambua umuhimu wao.

Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Victorina Ludovick, alisema wagonjwa 193,557, walipatiwa matibabu kwa msamaha, ambayo yaligharimu zaidi ya sh. bilioni moja katika bajeti ya mwaka 2016/2017.

Alisema katika kipindi hiki, wazee 17, 589, walipatiwa huduma mbalimbali za msamaha katika vituo vya kutolea huduma za afya katika manispaa hiyo.

Kwa mujibu wa Dk. Victorina, halmashauri hiyo ina wazee 44,222, kutoka katika kata 36 na kwamba, hadi sasa wanaendelea na usajili na tayari wazee 15,000, wasiojiweza walishapigwa picha kwa ajili ya kudurufu na kupatiwa vitambulisho.

Katika hatua nyingine, wazee wa Halmshauri ya Manispaa ya Kinondoni, wamelaani mashambulizi ya kihalifu dhidi ya raia,  mauaji wilayani Kibiti mkoani Pwani na mauaji ya wazee kwa imani za kishirikina.

Pia, wameipongeza serikali chini ya Rais Dk. Magufuli, kwa kuwajali na kutekeleza kwa vitendo sera ya serikali ya kuwapa matibabu bure, jambo ambalo wamedai kwao ni kama ndoto.

Hayo yalizungumzwa na wazee hao wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, ambayo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, yalifanyika jana, katika viwanja vya CCM Mwinjuma, Mwananyamala.

Akisoma risara ya wazee wilayani humo, Nassoro Juma, alisema, mashambulizi, mauaji dhidi ya raia huko Kibiti na yanayowahusu vikongwe kwa imani za kishirikina, yanalenga kulitia doa chafu taifa.

“Sisi wazee tunaomba hatua zichukuliwe haraka kudhibiti mashambulizi na mauaji hayo.Pia, kila mtanzania mzalendo, ashiriki kikamilifu katika kukomesha vitendo hivi vyenye nia ovu ya kulichafua taifa,”alisema Juma.

Aliongeza: "Sisi wazee kupewa kadi za matibabu bila malipo pamoja na huduma zingine tumeona kama ni ndoto. Haijawahi kutokea. Tumshukuru rais pamoja na manispaa yetu kwa kutukumbuka.”

Wazee hao wameomba serikali kuwasaidia kupanda mabasi yaendayo haraka (UDART), treni za abiria na kuingia na kutoka katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo bila malipo.

Pia, wameomba kusamehewa ankara za maji, kutokulipa vyoo vya umma, kuongezewa pensheni na kukopeshwa mitaji ili waweze kujikimu.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta, aliwahikishia wazee hao kuwa, serikali itahakikisha wanapata huduma zote za msingi bila kubughudhiwa.

Aliwashauri wazee hao kuanza kuunda vikundi vya maendeleo ili iwe rahisi kuwafikia na kuwahudumia kuliko mtu mmoja mmoja.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Festo Dugange, alisema kila mzee wilayani humo, atapatiwa kadi kwa ajili ya huduma za afya na kutakuwa na vituo katika kata zote kwa ajili ya kugawa kadi hizo, ambapo pia katika Hospitali ya Rufani ya Mwananyamala, litatengwa eneo maalumu kwa ajili ya wazee.

Akitoa ripoti ya huduma za wazee, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya, Halili Katani,  alisema jumla ya wazee 4,166, wametambuliwa katika kata 20 za maispaa hiyo, ambapo 1,838 ni wanaume na 2,328 ni wanawake.

“Wazee  2530 wamepatiwa vitambulisho  vya matibabu bila malipo sawa na asilimia 60. Katika vituo 27, wazee 7,475, wamepata  huduma ya matibabu  bila malipo kutoka Januari hadi Agosti, mwaka huu,”alisema Halili.

Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani ambayo hufanyika Oktoba Mosi kila mwaka, ambapo kitaifa yaliadhimishwa Dodoma, kaulimbiu ya mwaka huu ikiwa 'Kuelekea Uchumi wa Viwanda  Tunathamini Mchango, Uzoefu na Ushiriki wa Wazee'.

No comments:

Post a Comment