Monday, 14 September 2015

ASASI ZISIINGIE KICHWA KICHWA KWENYE SIASA,BAADHI ZIMEJIVIKA NGOZI ZA KONDOO






WANANCHI wakiwa katika moja ya mikutano ya kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mikutano kama hii hutumiwa na wagombea wa nafasi ya urais kunadi sera na ilani ya vyama vyao.

Na John Kiroboto
KIPINDI hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu nchini kinashuhudia watu wengi wakijitokeza kwa njia mbalimbali kuzungumza kwa kisingizio cha kutoa mchango wao katika kuhakikisha uchaguzi unafanyikka kwa amani, uhuru, utulivu na haki.
Makundi yanayojitokeza ni wanasiasa wenyewe ambao ndio wanaowania kuchaguliwa, tume za uchaguzi ambazo ndizo zenye dhamana ya kusimamia uchaguzi, Jeshi la Polisi ambalo linatazamiwa kulinda amani na utulivu, wanahabari wanaotazamiwa kuelimisha na kuhabarisha jamii, lakini na asasi za kiraia, zinazojinasibu kutoa elimu na kusimamia haki.
Wote hawa hujitokeza kupitia majukwaa mbalimbali yakiwamo ya kuzungumza moja kwa moja kwenye mikutano ya hadhara na ya ndani, kuandika na kutangaza, lakini pia kufanya midahalo na mijadala inayoelimisha na kuhabarisha jamii kuhusu uchaguzi.
Katika majukwaa yote hayo, ni dhahiri kauli zinazotolewa huambatana na hisia za wachangiaji hao na moja kwa moja kwa kusoma hisia hizo, msikilizaji, mtazamaji na msomaji anaweza kubaini nini kinamaanishwa na kwa ajili gani na ya nani kwa wakati huo.
Wapo ambao wakizungumza moja kwa moja hujibainisha na vyama fulani au makundi fulani ya watu katika jamii; lakini hivi sasa ni kwa vyama vya siasa hususan tawala cha CCM na vingine ambavyo vinaunda umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kwa kifupi ni kuwa katika yote hayo kambi mbili hujibainisha wazi, moja ya CCM na nyingine ya Ukawa, huku vyama vingine visivyo na nasaba na pande hizo mbili vikibaki ama kutazama na au kushangilia malumbano yanavyoendelea.
Baadhi ya vyombo vya habari na hata asasi za kiraia maarufu kama AZAKI, vimekuwa vikijibainisha katika pande hizo, huku vikijisahau kuwa vinatakiwa kutokuwa na upande na hivyo kutenda mambo yao kwa usawa ili kuepuka lawama na malalamiko. Isipokuwa vile vilivyo maalumu kwa propaganda.
Hilo limekuwa likishindikana kutokana ama na viongozi wa vyombo au wamiliki wao kusimamia upande mmoja ama kwa makusudi au kwa maelekezo maalumu au pia kwa matarajio fulani, kwamba kiongozi huyu akiingia madarakani pengine neema itawashukia.
Lakini pia wamekuwapo wazungumzaji ambao pengine kwa makusudi au kwa kuekelezwa, hujikuta wakiongeza chumvi katika wanayoyasema au kushawishi umma ili uwaamini, kwa sababu tu ni wasemaji au viongozi wa vyombo au taasisi hizo.
Lawama nyingi zinaelemea vyombo vya habari na AZAKI ambao wamejikuta wakiingia katika mkumbo wa vyama vya siasa ambavyo vina ajenda kuu za ‘kuing’oa CCM madarakani’ kwa vyovyote vile iwavyo na kujikuta wakihanikiza lugha hiyo hiyo kwa jamii.
Hapa chama tawala na serikali yake vimekuwa vikitupiwa madongo na tope na kuonyesha kwamba havijafanya lolote tangu kuzaliwa kwa Taifa hili, kwa kutumia kauli za miaka 50 ya Uhuru hakuna kitu kilichofanyika, na watoaji wa matamshi hayo wakionekana wenye siha njema wakiwasemea masikini waliosawajika.
Jumamosi nilisikiliza kipindi cha Power Breakfast on Saturday kinachorushwa na kituo cha Clouds Radio, ambapo Mratibu wa AZAKI,  Onesmo ole Ngurumwa alikuwa akizungumzia Ilani ya Uchaguzi iliyoandaliwa na Azaki, akisisitiza kuwa ndiyo inayostahili kuzingatiwa kutokana na kwamba za vyama vinavyogombea uongozi havina mashiko.
Nilimsikia Ngurumwa akidai kuwa Azaki ni mhimili wa nne wa Dola baada ya Serikali, Bunge na Mahakama, kwa hiyo zina nafasi kubwa katika jamii kwenye kuelimisha na hata kusimamia haki za ushiriki wa wananchi katika kuchagua viongozi na chama kinachofaa kuiongoza Tanzania ijayo.
Niliheshimu mawazo yake kama alivyotumwa na Azaki na akiwa mwanasheria nikaamini kwamba ni mtu ambaye atasimamia kwenye ukweli na hataupindisha wala kuongeza chumvi katika anayoyasema katika kuelimisha umma wa wananchi.
Nilitarajia asingejinasibu kuwa Azaki ni mhimili wa nne, labda kama angerekebisha kauli na kusema ‘tunajiita mhimili wa nne’. Asubiri abatizwe si kujibatiza mwenyewe kwa kudhani kuwa kazi anayofanya ni kubwa sana katika jamii kuliko makundi mengine kama yaliyotajwa hapo juu.
Alikwenda mbali zaidi pale alipoamua kuiponda serikali iliyoko madarakani, kwamba kwa miaka zaidi ya 50 sasa bado inakalia kujenga barabara badala ya hivi sasa “tungekuwa tunazungumzia kupeleka ndege Marekani…!”
Lakini pia katika kuongeza chumvi akitaka kusisitiza na kuhalalisha anachokisema, akadai kuwa nchini wapo watu ambao hawapati hata mlo mmoja kwa siku! Mwenye akili timamu lazima aamini kwamba watu wa aina hiyo hawapo nchini kwani wameshafariki dunia wote, kwa sababu kukosa mlo mmoja kwa siku ina maana hawana uhai.
Nilimsikia pia akiponda vyombo vya habari kuandika habari za wagombea na badala yake waandike habari kuhusu wananchi, akitaka wananchi ndio wazungumze ya kwao ili yaandikwe badala ya kila siku “kusikia Lowassa, Magufuli”.
Mbona wananchi wakiuliza maswali kwenye mikutano ya hadhara wagombea wanakataa kuyajibu na kudai hayana maana? Mwananchi wa Mvumi, Chamwino Dodoma, anamuuliza mgombea kuhusu kutuhumiwa na sakata la mtambo wa kufua umeme wa Richmond, anajibiwa kuwa hilo swali halina maana! Yapi yataandikwa ya wananchi?
Ieleweke, kuwa matatizo ya wananchi yanajulikana kwa wagombea, hivyo hivi sasa ni fursa yao kuyatafutia majawabu, badala ya kutaka kuulizwa maswali tena. Nani hajui matatizo ya elimu, afya, maji nakadhalika?  Ngurumwa hataki wagombea hususan wa CCM wakalalamikia matatizo yaliyopo na eti badala yake  waseme mazuri waliyoyafanya tu? Inasikitisha, kwani wananchi hawana macho?
Kiongozi wa Azaki anapaswa  aelewe, kuwa mataifa yote duniani hivi sasa yanaendelea na ujenzi wa barabara, aende Marekani, aende Afrika Kusini, aende Finland, China na kwingineko, barabara na madaraja vinajengwa kama hapa kwetu licha ya mataifa hayo kupata uhuru wao miaka zaidi ya hii ya Tanzania.
Kauli kama hizi na zingine ndizo zinashawishi kuhitimisha kuwa wapo watu wanaongoza taasisi na asasi kama hizi tayari wakiwa na misimamo ya pande na wanatumia nafasi walizonazo kudanganya umma kwa malengo yao ya kisiasa.
Hawa ndio wanaokuwa ndani ya taasisi hizo wakizitumia kama ngozi za kondoo huku wao mbwa mwitu wakiwa ndani, kwa maana kuwa ni wanasiasa wanaojivika ngozi za taasisi na asasi za kiraia na kuonekana wanatetea watu bila kuzingatia itikadi, kumbe wao wakiwa na itikadi zao rohoni.
Si siri, kwamba zipo baadhi ya asasi nchini ambazo zilishaingia ‘mikataba’ na wafadhili wanaotaka kuona CCM inang’oka madarakani kwa udi na uvumba na zilishashuhudiwa zikishirikiana na baadhi ya wapinzani kupanga mikakati ya kufanikisha azma hiyo ambayo haina chembe ya demokrasia hata kidogo.
Ni bahati mbaya hata wafadhili hao nao wamekuwa wakiwaaminisha kuwa hilo litawezekana na “mtashinda saa nne asubuhi…watake wasitake na Ikulu mtaingia”. Huo ni upotoshaji mkubwa na ni vema badala ya kulazimisha wananchi kumeza sumu, waachwe waamue wenyewe kwenye masanduku ya kura Oktoba 25.


No comments:

Post a Comment