Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili kwenye Uwanja wa Demokrasia wa Kibanda Maiti mjini Unguja kwa uzinduzi rasmi wa kampeni za chama hicho tawala za kugombea Urais wa Zanzibar |
Sehemu ya gharika ya watu kwenye Uwanja wa Demokrasia wa Kibanda Maiti mjini Unguja wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za chama hicho tawala za kugombea Urais wa Zanzibar |
Rais Kikwete akisisitiza jambo wakati akihutubia kwenye Uwanja wa Demokrasia wa Kibanda Maiti mjini Unguja wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za chama hicho tawala za kugombea Urais wa Zanzibar |
MOHAMMED ISSA NA SULEIMAN JONGO, ZANZIBAR
SHUGHULI katika mji wa Unguja, jana zilisimama kwa muda kufuatia mkutano mkubwa wa ufunguzi wa kampeni za urais wa Zanzibar, uliofanyika katika viwanja vya Kibanda Maiti mjini hapa.
Mkutano huo wa kihistoria ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Zanzibar pamoja na viongozi wa Chama na serikali.
Akizungumza katika mkutano huo, mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, alisema atahakikisha unaulinda Muungano wa Tanzania pamoja na kudumisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Rais Jakaya Kikwete alisema wapinzani wataendelea kuwa wasindikizaji na kwamba wengine ni wazoefu wa kusindikiza.
Alisema anashangazwa na kauli inayotolewa na mgombea urais wa chama cha CUF, Maalimu Seif Sharif Hamad, kudai kuwa serikali haijafanya kitu wakati yupo madarakani na kwamba kama haijafanya kitu, kwanini hakuondoka mapema.
Wakati Rais Kikwete akisema hayo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema Maalimu Seif amewahi kuwa Waziri Kiongozi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, lakini ameshindwa kuifanya Zanzibar kuwa nusu Singapore, sasa kama atakuwa rais atawezaje kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore kama alivyodai.
Kinana alisema hayo baada ya Maalimu Seaif katika mkutano wake wa ufunguzi wa kampeni, kudai kuwa akipewa ridhaa ya kuiongoza Zanzibar, ataifanya kama Singapore.
Akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza katika ufunguzi wa kampeni hizo, Dk. Shein, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama, Zanzibar, alisema uchumi wa Zanzibar, umekuwa kutoka asilimia 5.2 na kufikia asilimia 7.2 hivi sasa.
Dk. Shein alisema atahakikisha anayalinda na kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na Muungano na kwamba hakuna mtu ama kikundi cha watu wanaoweza kuthubutu kuuvunja Muungano.
Alisema hafanyikazi kwa kumuogopa mtu na kwamba ataendelea kujenga heshima za viongozi.
"Nitaongoza serikali bila ya kumuogopa mtu, nitajenga heshima kwa kila viongozi. Nitadumisha Muunganao, utaendelea kuwepo na kutunzwa," alisema.
Alisema aliyoyafanya katika utawala wake, hayana idadi, hayana hesabu na kwamba atahakikisha nchi inapata maendeleo zaidi.
Dk. Shein aliwaomba wananchi wa Zanzibar wamchague kuwa rais kwa muhula mwingine ili aweze kuwaletea maendeleo zaidi ya aliyoyafanya.
Alisema Muungano wa Tanzania ulidumishwa na waasisi wa taifa kwa utaratibu maalumu wa kikatiba na kisheria.
Dk. Shein alisema kuhusu mafuta na gesi, tayari serikali imeshatengeneza sera ya mafuta na tayari rasimu imeshatungwa.
Alisema mafuta hayawezi kuchimbwa kwa siku 100, kama baadhi ya watu wanavyofikiria na kwamba huo ni mchakato unaoweza kufikia hata miaka mitano.
Dk. Shein alisema atafanya kampeni za kistaarabu na kwamba atazunguka Unguja na Pemba kuhakikisha Chama kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
"Niko tayari kuitetea CCM, nitazunguka Unguja na Pemba kueleza sera za Chama na tutahakikisha tunashinda," alisema.
RAIS KIKWETE
Akizungumza katika mkuatano huo, Rais Kikwete alisema wapinzani ni wasindikizaji na wengi wana uzoefu wa kusindikiza.
Rais Kikwete alisema wapinzani wameshashindwa na kwamba Dk. Shein anasubiri kuapishwa kutokana na mambo mengi aliyofanya.
"Sababu ya Chama kuendelea kushinda ni kutokana na kuongoza nchi vizuri kwa amani na utulivu," alisema.
Alisema Dk. Shein katika utawala wake amefanya mambo mengi na hivi sasa matunda yake yanaonekana.
Rais Kikwete alisema anashangazwa na kauli ya Maalimu Seif, ambaye anadai kuwa Zanzibar haina maendeleo wakati mwenyewe yupo serikalini na kama hakuna kilichofanyika kwanini hakutoka.
Alisema Dk. Shein ni kiongozi makini, mvumilivu, mzalendo na mwenye uchungu wa nchi.
"Tutampigania ashinde na atashinda. Uchaguzi wa mwaka huu ni mtu na mtu, mjue mtu wako muombe kura mpaka tuipate," alisema.
Akizungumzia suala la mafuta na gesi, alisema limeshamalizwa na hivi sasa Zanzibar ina mamlaka yake ya kuchimba nishati hiyo na mapato yatakuwa ya Wanzanzibar.
Hata hivyo, alisema wapinzani wanadandia hoja ya mafuta na kwamba wamechelewa.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete alimkabidhi Ilani ya Uchaguzi, Dk. Shein na kushangiliwa na maelfu ya watu waliojitokeza.
MKAPA
Mzee Benjamini Mkapa jana alikuwa kivutio kikubwa katika mkutano huo, ambapo baada ya kutangaziwa muda wake wa kuhutubia, maelfu ya wananchi walimshangilia huku wakiwa na shauku ya kumsikiliza.
Mzee Mkapa ambaye ni rais msaafu wa awamu ya tatu, alisema anaimani kubwa na Dk. Shein kwamba ni mtu makini, muadilifu na mchapakazi.
Alisema Dk. Shein anapigania maendelea ya Wazanzibar bila ya ubaguzi hivyo ana kila sifa ya kuongoza tena nchi hiyo.
Mzee Mkapa alisema Dk. Shein anauwezo mkubwa wa kudumisha Muungano na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, hivyo aliwataka wananchi wamchague.
KINANA
Akizungumza na kuvuta hisia za watu wengi, Kinana alisema anashangazwa na kauli za Maalimu Seif, ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, lakini hakuwahi kuifanya Zanzibar kuwa hata nusu Singapore, sasa atawezaje kuifanya Singapore ikiwa atapata urais.
Alisema Maalimu Seif anadanganya watu na kwamba mwaka huu ni vyema akaandaliwa mafao yake mapema kwani atashindwa vibaya.
"Tutawaalika wapinzani wakati wa kuwaapisha Dk. Shein na Dk. John Magufuli, hawa kazi yao ni kudanganya watu," alisema.
MZEE MWINYI
Akizungumza na umati wa wananchi na wana-CCM, Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassani Mwinyi, aliwataka wananchi wamchague Dk. Shein kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya Zanzibar.
KARUME
Naye Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, alisema amani iliyopo hapa nchini haikuteremshwa kwa kamba, bali inatokana na CCM hivyo aliwataka wananchi wawachague viongozi wote wa Chama.
DK. BILALI
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharibu Bilali, aliwataka wananchi wamchague Dk. Shein na Dk. John Magufuli kwani wana kila sifa.
Huku akinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Dk. Bilali alisema bila ya CCM nchi itayumba na kwamba kuna kila sababu ya wananchi kuichagua CCM.
BALOZI IDI
Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idi alisema serikali ya Zanzibar, chini ya Dk. Shein imefanya mambo mengi na kwamba wapinzani wanadanganya watu.
Alisema mwaka huu, CCM itakizika chama cha CUF na inawezekana ikiwa ndio mwisho wake.
Balozi Idi alisema chama cha CUF hakiwezi kudumu kwa miaka mitano ijayo, hivyo anaamini baada ya uchaguzi itakuwa ndio mwisho wake.
Kwa upande wake, Kada wa CCM, Hamza Hassani Juma alisema mgombea mwenza wa CHADEMA, Juma Duni Haji, ni bumbuwazi na kwamba hata chama chake hakifahamu.
Alisema Duni ananasibiwa na jina lake ambalo ni 'Duni' hivyo hajui analolifanya.
Juma alisema Duni aliondoka serikalini na kuchukua maslahi yake yote ambapo hivi sasa anadai hakuchukua kitu chochote.
Alisema Maalimu Seif abaada ya kuonekana anatangatanga mitaani, alichukuliwa na kukaribishwa ukumbini, lakini anashindwa kuwa na fadhila.
Juma alisema mwaka huu, Maalimu Seif akikataa matokeo hatasubiriwa tena na kwamba hata hiyo nafasi yake anaweza akaikosa.
BORAAFYA
Mwenyekiti wa Chama mkoa wa Mjini Magharibi, Borafya alisema Duni alipelekwa CHADEMA kwa mkopo na hivi sasa hata la kuzungumza hana bali anazungumzia suala la uzazi wakati hata mtoto hana.
Alisema CUF imeuzwa na Edward Lowassa na dalali wake alikuwa Mansour Yussuf Himidi.
Katika mkutano huo, wasanii Mzee Yussuf na Nasibu Abdul 'Diamond' walikonga nyoyo za wana-CCM, wananchi na mashabiki waliojitokeza katika mkutano huo.
Wasanii hao pia walizikonga vilivyo nyoyo za viongozi wakuu waliohudhuria kampeni hizo
No comments:
Post a Comment