Sunday, 20 September 2015

SHEIN; NITAIFANYA ZANZIBAR VISIWA HURU VYA UWEKEZAJI NA VIWANDA




NA MOHAMMED ISSA, MICHEWENI
MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema iwapo atapewa ridhaa ya kuiongoza tena Zanzibar, atahakikisha visiwa hivyo vinakuwa eneo huru la uwekezaji na viwanda.
Amesema serikali yake, imetenga maeneo huru kwa ajili ya uwekezaji, Unguja na Pemba kwa lengo la kuvibadili visiwa hivyo na kukuza uchumi wa wananchi na taifa.
Mgombea huyo alisema hivi sasa kuna muwekezaji ameonyesha nia ya kutaka kujenga kiwanda cha sukari katika wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba.
Aidha, alisema katika awamu ya pili ya utawala wake, ataboresha sekta ya uvuvi na kuwa ya kisasa ili iweze kuwanufaisha wananchi na kukuza pato la taifa.
Dk. Shein alisema alisema hayo jana katika mkutano wake wa tatu wa kampeni kisiwani Pemba, uliofanyika wilaya ya Micheweni na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi na wanaCCM.
Dk. Shein tayari amefanya mikutano ya kampeni katika wilaya ya Chake Chake mkoa wa Kusini, Konde na Micheweni mkoa wa Kaskazini, Pemba.
Alisema atahakikisha Zanzibar, inakuwa eneo huru la uwekezaji na viwanda na kwamba tayari maeneo ya uwekezaji yametengwa na wakati wowote yataendelezwa.
Dk. Shein alisema kwa Unguja wametenga eneo la Fumba na Pemba wilaya ya Micheweni ambayo maeneo hayo yatakuwa mahusus kwa uwekezaji ili kuboresha maisha ya wananchi na serikali kupata mapato.
Mgombea huyo alisema pango huo utaanza wakati wowote na tayari wilaya ya Micheweni kuna muwekezaji ameonyesha nia ya kutaka kujenga kiwanda cha sukari na kitakapokamilika kitatoa ajira kwa vijana.
Alisema eneo la Fumba, tayari mfanyabiashara Said Salumu Bakharesa ameonyesha nia ya kutaka kujenga kiwanda cha maziwa ambacho kitakuwa kikubwa katika nchi za Afrika Mashariki.
Dk. Shein alisema katika awamu ya kwanza ya utawala wake, alianzisha wizara maalumu ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kuiboresha sekta hizo.
Hata hivyo, alisema dhamira yake ni kuhakikisha sekta ya uvuvi inaboresha zaidi na kuwa ya kisasa ambayo itawanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.
Alisema tayari watu kadhaa wameonyesha nia ya kutaka kujenga viwanda vya samaki Unguja na Pemba na kwamba hilo likifanikiwa litaifanya sekta hiyo kuimarika na kuwanufaisha wananchi.
Dk. Shein alisema baada ya kuingia madarakani, sekta ya uvuvi imekuwa na mafanikio makubwa ambapo katika kipindi cha miaka minne na nusu, tani 148,535, za samaki zilivuliwa na kuingizia serikali sh. bilioni 532.
Aidha alisema serikali ya Korea, ilileta vifaranga vya samaki ambapo walianzisha mabwawa sita ya kufugia samaki na kuwafundisha wananchi namna ya kufuga samaki.
“Najuwa wananchi wengi wa Micheweni na maeneo mengine munategemea uvuvi hivyo mukinichagua nitaiboresha sekta hiyo ili kuwa ya kisasa, itakayowanufaisha na kujipatia kipato,” alisema.
Alisema hivi sasa kuna vikundi vidogo vidogo vya uvuvi 167, vyenye wanachama 36,000.
Dk. Shein alisema dhamira yake ni kuibadilisha wilaya ya Micheweni ili kuwa tofauti na ilivyo sasa.
Alisema katika wilaya hiyo, huduma muhimu za jamii zimeboreshwa ikiwa ni pamoja na kujengwa barabara, umeme na maji.
Kuhusu Hospitali ya Micheweni, alisema itapandishwa hadhi na kuwa ya wilaya ambapo itawekewa vifaa vya kisasa.
Alisema baada ya kuingia madarakani alihakikisha huduma za uzazi zinatolewa bure kwenye hospitali zote za serikali.
Dk. Shein alisema atahakikisha sekta ya utalii inaboreshwa zaidi ili kukuza pato la taifa na kuwa mbadala wa kilimo.
Aliwaomba wananchi wamchague kuwa rais pamoja na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, wabunge, wawakilishi na madiwani.
Mgombea huyo alisema mwaka huu, Chama kitapata ushindi mkubwa kutokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ulivyofanikiwa visiwani humo.

No comments:

Post a Comment