NA CHARLES MGANGA, GEITA
BAADHI ya wananchi wamesema mgombea urais kupitia CCM, Dk.
John Magufuli, ndiye sahihi wa kuliongoza taifa katika awamu ya tano kutokana
na sifa na vigezo alivyonavyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye kampeni za Dk.
Magufuli, wananchi hao walisema wamekuwa wakimsikiliza mgombea urais kupitia UKAWA,
Edward Lowassa na kugundua ahadi zake ni danganya toto.
John Mazweto, mkazi wa eneo la Kazuramimba mkoani
Kigoma, alisema Watanzania wa sasa hawadanganyiki kirahisi kwa sababu wana upeo
mkubwa wa kupambanua mambo.
Alisema anachokifanya mgombea huyo wa UKAWA ni
kuwarubuni watu ili aweze kupata nafasi hiyo na kuliangamiza taifa.
“Kwa mtu yeyote mwenye upeo wa kuangalia mbali, huna
sababu ya kugundua kinachozungumzwa na mgombea wa UKAWA ni uongo wa kupindukia.
Ahadi zake ni uongo ambao hata mtoto
mdogo anagundua,” alisema Mzweto.
Mkazi huyo alisema ni ukweli ulio wazi, mgombea wa CCM,
Dk. Magufuli ataibuka mshindi wa nafasi hiyo kwa kishindo kikubwa.
Amos Cyprian wa Nguruka, Kigoma naye alisema utendaji
kazi wa Dk. Magufuli unafahamika kwa kila Mtanzania, hakuna asiyefahamu
uchapakazi wake.
“Hivi kuna mtu asiyejua utendaji kazi wa huyu mheshimiwa
(Dk. Magufuli). Kama hakuna basi huyo ni kipofu. Hujui kusoma, hata picha?” alihoji
Cyprian.
Ashura Ally wa Biharamulo, alisema Dk. Magufuli ndiye
anayeuzika ukilinganisha na wagombea wengine saba wanaowania nafasi hiyo ya
urais wa awamu wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Huyu mtu ni muadilifu…kashfa yake iko wapi. Hebu
waangalie hao wengine wana harufu ya ufisadi tupu. Dk. Magufuli ndiye chaguo la
Mungu na sahihi kwa awamu ijayo,” alisema Ashura ambaye ni mfanyabiashara ndogo
ndogo wa Biharamulo.
Akiwa katika kampeni katika maeneo mbalimbali mkoani
Kigoma na mjini Biharamulo, Dk. Magufuli alisema Watanzania wanapaswa kufanya
uamuzi makini siku ya uchaguzi.
Aliomba waendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi
kiendelee kuongoza nchi, kwa sababu kina sera zinazotekelezeka zilizo katika
ilani.
Aliwaasa kutohadaika na ahadi zinazotolewa na wagombea
wa upinzani kwani, nyingi hazina ukweli wowote.
“Najua watakuja na kuwaambia mambo mengi. Eti mnaambiwa,
mtajengewa nyumba bora ndani ya muda mfupi, huyo anayetoa ahadi jimboni kwake
wanafunzi hawana hata sare za shule,” alisema Magufuli.
Alisema Watanzania wawasikilize wapinzani wanachoahidi,
lakini wawe makini katika uamuzi wao.
“Wasikilizeni, lakini pimeni wanachokiongea. Naomba
mnipe ridhaa ya kuongoza nchi ili kwa kushirikiana na wabunge wa CCM, tuweze
kuijenga Tanzania mpya,” alisema Dk. Magufuli.
No comments:
Post a Comment