Na Nathaniel Limu, Ikungi
HARAKATI za Tundu
Lissu kutetea ubunge jimbo la Singida Mashariki
zimeingia dosari baada ya baadhi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA kukihama
chama hicho na kurejea CCM kwa madai chama hicho cha kimedumaza maendeleo ya
jimbo hilo.
Baadhi ya viongozi waandamizi katika jimbo hilo, waliohama
hivi karibuni na kurejea CCM ni Mwenyekiti
CHADEMA Kata ya Mungaa, Ali Juma Kiemi, Katibu Mwenezi CHADEMA Kata ya Mungaa, John
Mpaki na Katibu Mwenezi CHADEMA Kata ya Ikungi, Khamisi Mazonge.
Viongozi hao kwa
sasa wanatumiwa na CCM katika kampeni ya kuiondoa CHADEMA Jimbo la Singida Mashariki.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni CCM katika Kijiji
cha Kinyamwandio, Tarafa ya Ikungi, Mazonge alisema CHADEMA jimbo la Singida Mashariki
katika miaka yake mitano iliyopita, haijaleta maendeleo na kusababisha jimbo hilo kushika mkia
kimaendeleo mkoani Singida.
“Kilichofanyika
katika miaka hiyo ni maneno matupu tena ya upotoshaji, maendeleo katika sekta
zote yamesimama, wananchi tumedanganywa kuwa serikali ndiyo yenye jukumu la kuliletea
jimbo letu maendeleo na si wakazi wake. Ilidaiwa kuwa serikali ina fedha za
kutosha kuleta maendeleo, lakini hadi sasa hatujaziona hizo fedha,” alifafanua
Mazonge.
Katika hatua
nyingine, Mazonge aliwataka mgombea urais kupitia UKAWA, Waziri Mkuu
aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick
Sumaye, wawatangazie Watanzania kuwa sasa wanaunga mkono serikali tatu.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti CHADEMA Kata ya
Mungaa, Kiemi alitumia fursa hiyo
kuwataka wana CHADEMA katika jimbo hilo kuhama kwa kuwa licha ya kudumaza
maendeleo, jimbo hilo litakuwa tanuru la kuzalisha vijana watumishi na walinzi
wa nyumba za wasomi.
“Niwatake
wenzangu waliobakia CHADEMA wafanye maamuzi sahihi mapema ya kurejea CCM na
waondokane na fikira potofu, kuwa Tundu Lissu, ni mkombozi wao. Lissu hawezi
kuwa mkombozi kwa vile hajaleta maendeleo yoyote jimboni kwa miaka mitano. Alicholeta
ni maneno matupu na kwake vitendo ni mwiko…maendeleo huletwa kwa vitedo na si
vinginevyo,”alisema.
Pia, Kiemi alisema amechukizwa na kuhuzunishwa na
kitendo cha CHADEMA kumpokea Lowassa na kumuuzia chama kizima.
“Lowassa licha ya
kununua CHADEMA, amekilazimisha chama
kupokea makapi marafiki zake kutoka CCM na kuyapa nafasi zikiwemo za ubunge. Makapi
hayo yamewaengua wanachama wa CHADEMA waliokijenga chama hadi kikawa na nguvu, hii
ni dhambi kubwa,”alisema.
Baadhi ya
wanachama wa CHADEMA na wakazi wa jimbo la Singida mashariki,wameanza kuingiwa
na na hofu kwamba Lissu anaweza
kupoteza nafasi yake mwaka huu, kama
upepo wa kisiasa jimboni humo utaendelea kama ulivyo hivi sasa.
No comments:
Post a Comment