Sunday, 20 September 2015

WANANCHI ZANZIBAR WAMPONGEZA DK. SHEIN




BAADHI ya wananchi wa jimbo la Mtabwe, ambalo amezaliwa mgombea urais wa chama cha CUF, Maalimu Seif Sharifu Hamadi wamempongeza na kumshukuru mgombea urais wa CCM, Rais Dk. Ali Mohammed Shein, kwa kuwajengea barabara mpya ya lami na kuwaondoshea usumbufu waliokuwa wakiupata kwa miaka mingi.
Walisema pamoja na Maalimu Seif, kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwemo Waziri Kiongozi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, lakini alishindwa kuijenga barabara ya kwenda kijijini kwao mpaka imejengwa na serikali ya CCM, chini ya Dk. Shein.
Aidha, walisema walikuwa wakipata shida kutokana na ubovu wa barabara hiyo na kwamba kipindi cha mvua walilazimika kupanda gari za punda ili kufika kwenye shughuli zao.
Wakizungumza na Uhuru, jana, kwa nyakati tofauti wananchi hao, walisema shughuli za kijamii na kiuchumi zilisimama kutokana na ubovu wa barabara.
Tamima Salehe Juma mkazi wa Bahanasa alisema wanaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), chini ya Dk. Shein kwa kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kuwaondoshea usumbufu wananchi.
Alisema pamoja na Maalimu Seif kuzaliwa kijiji cha Mtabwe na kushika nyadhifa mbalimbali serikalini lakini alishindwa kuijenga upya barabara hiyo mpaka imetengenezwa na serikali ya CCM.
“Unajua mwisho wa barabara hii ndiko alikozaliwa Maalimu Seif, lakini siku zote hizo alishindwa kuitengeneza kama si juhudi za makusudi za Dk. Shein hadi sasa ingekuwa na mashimo hata gari zilikuwa hazijiji huku,” alisema.
Mbarouk Juma Ali mkazi wa Bwagamoyo, alisema pamoja na jimbo la Mtambwe kuongozwa na CUF, tokea mfumo wa vyama vingi ulipoingia lakini wameshindwa kuitengeneza barabara hiyo.
Alisema uongozi wa CCM, chini ya Dk. Shein, umewakomboa wananchi wa jimbo hilo kwa kuijenga upya barabara hiyo ambayo ilikuwa mbovu kwa miaka mingi.
Alisema kipindi cha mvua walilazimika kutumia usafiri wa Punda kufika kwenye shughuli zao lakini baada ya kujengwa upya uchumi wa wananchi unaimarika kutokana na kufanya shughuli zao kwa uhakika.
Asha Salehe Juma mkazi wa Mtambwe, alisema jimbo hilo lilikuwa nyuma kimaendeleo kutokana na ubovu wa barabara.
Alisema CCM, imewakomboa wananchi wa jimbo hilo licha ya Maalimu Seif, kuzaliwa jimboni humo lakini lilikuwa nyuma kimaendeleo kutokana na kukosa miundombinu ya barabara na maji safi na salama.
Sheha wa Shehia ya Mtambwe, Kaskazini, Suleiman Bakari Hamis, alisema anaishukuru serikali ya awamu ya saba kwa kufanya mambo mengi ya maendeleo katika jimbo hilo.
Alisema barabara ya kutoka Bahanasa kwenda Mtambwe ilikuwa mbovu kwa miaka mingi lakini baada ya Dk. Shein kuingia madarakani ameijenga upya kwa kiwango cha lami na kuwaondoshea usumbufu wananchi.
Hamis alisema serikali ya Dk. Shein pia ilifanikiwa kupandisha bei ya zao la karafuu kutoka sh. 5,000, kwa kilo moja na kufikia sh. 15,000, kwa kilo moja.
Alisema mafanikio yaliyopatikana katika utawala wa Dk. Shein ni makubwa na kwamba ni faraja kwa wananchi ambapo hivi sasa uchumi umeimarika.
Kwa upande wake, Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Miundombinu, Pemba, Hamad Ahmed Baucha, alisema barabara tano zimejengwa kwa kiwango cha lami kwa msaada wa Mfuko wa Maendeleo unaofadhiliwa na watu wa Marekani (MCC).
Alizitaja barabara hizo kuwa ni Mzambarau Karimu- Finya-Mapofu yenye urefu wa kilomita nane, Mzambarau Takao- Finya yenye urefu wa kilomita tisa, Bahanasa- Mtambwe yenye urefu wa kilomita 13.8, Chwale-Likoni yenye urefu wa kilomita 1.9 na Kipangani-Kangagani yenye urefu wa kilomita 27.
barabara zenye urefu wa kilomita 500, ambapo kati ya hizo kilomita 271, zimejengwa kwa kiwango cha lami na zilizobakia zimejengwa kwa kiwango cha changarawe.

No comments:

Post a Comment