CHAMA Cha Mapinduzi (CCM),
kimemuonya mgombea urais wa chama cha CUF, Maalimu Seif Sharifu Hamad, kuacha
‘chokochoko’ na badala yake afanye kampeni za kistarabu bila ya kuwagawa
wananchi.
Aidha kimesema viongozi wa chama hicho
wameanza kugombana baada ya kuona mikutano ya mgombea urais wa Chama, Dk. Ali
Mohammed Shein, imefanikiwa vilivyo kisiwani Pemba.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar,
Vuai Ali Vuai, alisema hayo jana katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa
Zanzibar, Dk. Shein, uliofanyika wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema Maalimu Seif ameanza
‘chokochoko’ kutokana na wafuasi wake kuanza kuwashambulia wanaCCM na kuharibu
magari yanayokwenda kwenye mikutano ya Chama.
Vuai alisema pamoja na kusaini
makubaliano maalumu ya uchaguzi ambayo ni pamoja na kufanya kampeni kwa
ustaarabu lakini wafuasi wa CUF, wameanza vurugu kwa kuwashambulia wanaCCM na
kuchana picha za wagombea wa CCM.
Alisema hila hizo zinafanywa na
Maalim Seif ambaye ameshindwa kuwadhibiti wafuasi wake na kwamba Chama
kinamtaka afanye kampeni za kistarabu.
Kwa mujibu wa Vuai, viongozi wa CUF,
wameanza kulumbana baada ya kuona mikutano ya Dk. Shein, inafanikiwa vilivyo
kisiwani Pemba.
Alisema Dk. Shein amefanya mikutano
mitatu ya kampeni kisiwani humo ambayo maelfu ya wananchi na wanaCCM,
walijitokeza kumsikiliza.
Vuai alisema viongozi hao wa CUF,
juzi, walikuwa na kikao cha dharura kujadili namna wanavyoweza kuwazuia watu
kwenye mikutano ya CCM.
“Hivi sasa CUF, wameanza kulumbana
baada ya kuona mikutano yote ya mgombea wetu (Dk. Shein), wananchi wanajitokeza
kwa wingi. Waliweka kikao na kuulizana kuwa pamoja na kugawa vespa kila jimbo
lakini hazijasaidia kuwazuia watu wasihudhurie mikutano ya CCM,” alisema.
Alisema mwaka huu, CUF imeshikwa pabaya
baada ya kuwadanganya watu kwa miaka mingi na kwamba CCM itapata ushindi mkubwa
kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na
Nishati, Ramadhani Abdallah Shaabani, alisema mwaka huu, Dk. Shein ana kila
sababu ya kushinda kutokana na mambo mengi ya maendeleo aliyofanya.
Akizungumzia suala la mafuta na
gesi, alisema anawashanga CUF, kuidandia hoja ambayo hawaifahamu na kwamba
suala hilo limeshapatiwa ufumbuzi.
Shaabani alisema suala hilo lime
kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na tayari linafanyiwa kazi kwa nguvu zote ikiwa
ni pamoja na kuingia makubaliano ya awali.
Aliwataka CUF, kuacha kudandia mambo
ambayo hawayafahamu na kwamba sheria ya mafuta na gesi imeshanzisha ambapo
katika baraza la wawakilishi lijalo muswaada huo utawasilishwa ili uwezwe
kupitishwa na kuwa sheria.
Shaabani alisema Zanzibar, itakuwa
na mamlaka kamili ya kuchimba na kutafuta nishati hiyo na mapato
yatakayopatikana yatawanufaisha wananchi na serikali kwa ujumla.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed, alisema mwaka huu, lazima
CCM ipate majimbo kisiwani Pemba.
Alisema wananchi wa kisiwa hicho
wana kila sababu ya kuwachagua wagombea wa Chama kutokana na mambo mengi
yaliyofanyika katika utawala wa Dk. Shein.
No comments:
Post a Comment