NA MOHAMMED ISSA, PEMBA
KWA yoyote anayekuja
Zanzibar, atakubali kuwa visiwa hivyo vimepiga hatua kubwa ya kiuchumi na
kisiasa.
Ni ukweli usiopimgika
kuwa Zanzibar, na mabadiliko hayo yamesababishwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja
na utawala imara chini ya uongozi wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein.
Ukiangalia historia ya
Zanzibar, hasa katika kipindi kama hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, utakubali
kuwa sasa imebadilika kwani chaguzi nyingi zilizopita zilikuwa zinatawaliwa na
vurugu na fujo lakini hivi sasa hali ni shwari na kila mtu anaendelea na
shughuli zake.
Uongozi wa Dk. Shein,
umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuibadilisha Zanzibar, kisiasa na kiuchumi
tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Dk. Shein ambaye pia
anagombea urais wa Zanzibar, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivi sasa
amekuwa midomoni mwa wananchi wengi wa visiwa hivyo kutokana na kazi kubwa
aliyofanya kwenye awamu ya kwanza ya utawala wake.
Mgombea huyo ambaye hivi
karibuni alizindua kampeni zake za urais katika katika uwanja wa Kibanda Maiti
mjini Zanzibar, anasema iwapo atapewa ridhaa ya kuviongoza tena visiwa hivyo,
ataleta mageuzi makubwa ya kisiasa na kiuchumi.
Dk. Shein anasema ambaye
kwa sasa anaendelea na kampeni zake, kisiwani Pemba, anasema Ilani ya Uchaguzi
ya CCM, imetekelezwa kwa asilimia 90.
Akizungumza katika
mkutano wa hadhara wa kuinadi Ilani ya Uchaguzi wa Chama, uliofanyika kijijini
kwao Chokocho wilaya ya Mkoani mkoa wa Kusini Pemba, mgombea huyo alielezea
mambo kadhaa yaliyomo kwenye Ilani hiyo huku akitamba kuisimamia na kuitekeleza
ipasavyo iwapo atachaguliwa.
Dk. Shein, anasema lengo
na dhamira ya kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ipo pale pale
na kwamba atahakikisha Zanzibar, ina madilika.
Dk. Shein anasema
atahakikisha anafanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii visiwani humo,
ili kuifanya Zanzibar, kuwa ya maendeleo zaidi ya sasa.
Anasema pamoja na
mgombea urais wa chama cha CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, kudai ataifanya
Zanzibar, kuwa kama Singapore kwa siku 100, lakini uwezo huo hana kwani hata
hiyo Singapore haikupata mafanikio kwa kipindi cha siku 100, bali ilichukua
muda mrefu kufikia maendeleo hayo.
Dk. Shein anasema katika
utawala wake, atahakikisha anaboresha sekta ya elimu ili wananchi waweze kupata
elimu bora kuanzia shule za awali, msingi, sekondari na vyuo.
Anasema ili taifa lolote
duniani liweze kuendelea ni lazima liwekeze kwenye elimu hivyo serikali yake
itahakikisha inatoa elimu bora kwa wananchi wote.
Dk. Shein anasema katika
Ilani ya Uchaguzi ya Chama, imeweka kipaumbele kikubwa kwenye sekta ya elimu na
kwamba tayari kazi imeanza kufanyika ambapo shule 19, zilijengwa kwenye maeneo
mbalimbali ya Pemba.
Anasema atazihamasisha
sekta binafsi kujenga shule za maandalizi kwenye vijiji mbalimbali vya
Zanzibar, ili kila mwanafunzi mwenye umri wa kwenda shule, anapata nafasi hiyo
na kwa shule za msingi waanda mpango maalum ili watoto waweze kula chakula
mashuleni.
Anasema hivi sasa elimu
ya msingi inatolewa bure bila ya mzazi kuchangia kitu chochote kuanzia darasa
la kwanza hadi la saba.
Dk. Shein anasema katika
miaka mitano ijayo, kiwango cha watoto wanaoingia sekondari kitaongezeka kutoka
asilimia 20, na kufikia asilimia 80.
Anasema katika Shule ya
Mtule iliyoko Paje na Chwaka watajenga mabweni ili vijana waweze kukaa na
kwamba watakamilisha ujenzi wa shule 20, za sekondari ambazo zitawekewa
teknolojia za mawasiliano.
Mgombea huyo anasema
serikali itajenga vyuo vya mafunzo ya awali na kwamba wataanza katika kijiji
cha Mtambwe pamoja na kuimarisha vyuo vya walimu.
Anasema katika mwaka wa
kwanza wa uongozi wake, ataondosha michango ya wazee kwenye shule za sekondari
ambapo elimu ya sekondari itakuwa bure.
“Natangaza kuondosha
michango katika mwaka wa mwanzo wa utawala wangu, elimu ya sekondari itakuwa
bure,” anasema na kushanigiliwa na wananchi wengi.
Anasema anadhamiria
kuanzisha chuo kikuu kipya ambacho kitajengwa katika kijiji cha Dole na kwamba
ataendelea kuboresha elimu ya vyuo vikuu.
Dk. Shein anasema wanawake
watapewa nafasi maalumu ya kusoma masomo ya sayansi ambapo serikali itajenga
shule maalumu kwa ajili ya wanawake.
AFYA
Kuhusu huduma za afya,
mgombea huyo anasema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita waliimarisha
huduma hizo ambapo Hospitali ya Mnazi Mmoja imepanda hadhi na kuwa ya rufani.
Anasema Hospitali ya
Abdala Mzee iliyoko Pemba inajengwa upya ambapo baada ya kukamilika itakuwa na
uwezo wa kupokea wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Dk. Shein anasema
serikali yake itapambana na magonjwa yote yanayowakabili wananchi ili yaweze kumalizika
kabisa.
Anasema tayari madaktari
wengi wameongezwa kwenye hospitali mbalimbali zilizopo visiwani humo.
Dk. Shein anasema hivi
sasa, daktari mmoja anawahudumia watu 9,000 ,badala ya 30,000, katika miaka
mitatu iliyopita.
Kwa mujibu wa Dk. Shein,
serikali itajenga hospitali mpya na ya kisasa ya rufani ya Zanzibar, na kwamba
hospitali hiyo pia itatibu magonjwa ya saratani.
Anasema katika miaka
miwili ya mwanzo wa utawala wake, atatoa matibabu bure kwa kila mwananchi wa
visiwa hivyo.
Dk. Shein aliwataka
wananchi kuendelea kuichagua CCM, kwani ina dhamira kubwa ya kuleta maendeleo
ya wananchi.
Anawataka wananchi
wasikubali kudanganywa na vyama vingine ambavyo havina uwezo wa kuwatumikia
wananchi na kwamba havitashinda.
MAPATO
Dk. Shein anasema katika
miaka mitano ijayo, mapato ya Zanzibar, yatafikia sh. bilioni 800, hivyo mambo
mengi yatafanyika.
Anasema hawezi kuahidi
kuwa ataifanya Zanzibar, kuwa kama Singapore kwa kipindi cha siku 100, kama
alivyoahidi Maalimu Seif, kwani kutoa ahadi hiyo ni kuwadanganya wananchi.
“Mimi nimekwenda
Singapore nimekaa siku tano, nimezungumza na mawaziri pamoja na rais wao lakini
hatuwezi kuwafikia kwa siku 100, hata wenyewe hawakuijenga nchi hiyo kwa siku
100, hivyo wanaodai wanataka kuifanya Zanzibar, kwa siku 100, wanawadanganya,”
anasema huku akishangiliwa.
MAJI
Kuhusu sekta ya maji,
anasema hivi sasa maeneo mengi ya visiwa hivyo, yanapata huduma ya maji safi na
salama tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Anasema atahakikisha
huduma ya maji vijijini yanafikia asilimia 85, kutoka asilimia 70, maeneo ya
mijini yafikie asilimia zaidi ya 85.
UMEME
Dk. Shein anasema mwaka
2010, aliahidi kupeleka umeme Kisiwa Panza na Makoongwe, ambapo jana
alienda kuuzindua umeme katika vijiji hivyo.
Anasema umeme vijijini,
umefikia kwa asilimia 103, ambapo imevuka lengo katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita.
WAZEE
Kuhusu wazee, mgombea
huyo anasema serikali yake ilijitahidi kuwaenzi wazee kwa kuwajenga nyumba
mzuri na kuwapelekea huduma muhimu ambapo kuanzia Aprili mwakani kila mzee mwenye
umri wa miaka 70, atalipwa pensheni ya sh. 20,000, bila ya kujali kuwa
anafanyakazi serikalini, sekta binafsi au hana kazi.
“Pensheni hiyo atalipwa
kila mzee mwenye umri wa miaka 70, hata kama sio mfanyakazi basi atalipwa
pensheni. Nafanya hivyo ili kutimiza azma yangu ya kuwasaidia wazee,” anasema
na kuibua shangwe kwa wananchi waliojitokeza katika mkutano huo.
Anasema atahakikisha
anawawekea mazingira mazuri wazee ikiwa ni pamoja na makazi na matibabu bure
wanapoenda hospitali.
UWANJA WA NDEGE
Anasema aliahidi
kuimarisha uwanja wa ndege wa Pemba ambapo hivi sasa unafungwa taa ili ndege
ziweze kuruka usiku.
Dk. Shein anasema
amaefanya mambo mengi mazuri katika visiwa hivyo ambapo aliwataka wananchi
wamchague ili aweze kuendeleza gurudumu la maendeleo.
WANANCHI
Hmad Bakari Haji mkazi
wa Matuleni, anasema anaimani kubwa na mgombea huyo kutokana na kufanya mambo
mengi ya maendeleo visiwani humo.
Anasema katika utawala
wa Dk. Shein, amefanikiwa kuiongoza nchi kwa salama na amani ambapo hivi sasa
wananchi wanaishi kwa umoja na mshikamano.
Mwalimu Juma Omar mkazi
wa Chake Chake, anawashauri wananchi wenzake, wamchague mgombea huyo kutokana
na kazi kubwa aliyofanya katika utawala wake.
Anasema Dk. Shein ni
mchapakazi hodari, msikivu na kiongozi shupavu ambaye ameleta mabadiliko
makubwa ya kisiasa na kiuchumi visiwani humo.
No comments:
Post a Comment