Thursday, 1 October 2015

CCM YAJIHAKIKISHIA USHINDI




NA KHADIJA MUSSA, MUSOMA
CCM imezidi kujihakikishia ushindi katika jimbo la Musoma mjini, baada ya maelfu ya wananchi kufurika katika mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwenye kata ya Mwisenge, wilayani hapa.
Jimbo hilo lilikuwa ni ngome ya CHADEMA na mbunge wake Vincent Nyerere, ambaye kwa sasa anaonekana kushindwa kulitetea jimbo hilo, kutokana na mgombea wa CCM, Vedastus Mathayo kunaonekana kukubalika zaidi na wananchi.
Hata hivyo katika maeneo mbalimbali ya mji wa Musoma, hakuna mabango wala vipeperushi vinavyomnadi Nyerere na badala yake maeneo yote yamepambwa na mabango yanayonadi wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya urais na ubunge, jambo linaonyesha kukubaliwa kwa chama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa Musoma walisema wameshituka na kuamua kuachana na CHADEMA kwa kuwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Nyerere alishindwa kuwaletea maendeleo.
Mwita Manyama ambaye ni mmoja wa wananchi katika eneo hilo, alisema Nyerere ameshindwa kuwasaidia, hivyo ni bora wakimchagua Mathayo, ambaye amekuwa akitoa misaada mbalimbali bila ya kujali itikadi za kisiasa wala  kidini.
Naye Bhoke Chacha alisema Mathayo amekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Musoma, hivyo atahakikisha anawashauri wanawake wenzake kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kumchagua Dk. John Magufuli katika nafasi ya urais na ubunge wamchague Mathayo, pamoja na madiwani wote wa CCM.
Alisema hawana sababu ya kuchagua viongozi wa CHADEMA kwa sababu wameshindwa kuwasaidia, ambapo walikuwa wakimfuata mbunge kwa ajili ya kumwomba msaada wa kuwaongeza mitaji, hasa wajasiriamali, lakini aliwatosa.
 Mathayo ambaye hakuwepo katika mkutano huo kutokana na kupata msiba, alipokuwa akitajwa uwanja mzima ulishangilia, jambo lilionyesha kuwa anakubalika.
Akizungumza katika mkutano huo,Samia alisema mgombea wa urais wa CCM, Dk. Magufuli ndiye anayefaa kukabidhiwa kijiti na Rais Jakaya Kikwete kutokana sifa nzuri alizokuwa nazo na uwezo mkubwa wa kuliongoza taifa.

No comments:

Post a Comment