Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Balozi Seif Ali Idd amesema mwanasiasa anayedai akichaguliwa ataibadilisha
Zanzibar kwa siku 100 kuwa Singapore, huyo ni muongo.
Amesema ingekuwa kauli hiyo ni ya
ukweli, mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, angeweza
kuibadili Pemba kuwa Singapore ndani ya miaka 20 aliyokuwa kiongozi serikalini.
Kauli ya Balozi Iddi imetokana na
kauli ya Maalimu Seif Sharif Hamad, ambaye ni mgombea wa CUF katika nafasi ya urais
Zanzibar, kuwa ataibadilisha Zanzibar na kuwa Singapore ndani ya siku 100,
endapo atachaguliwa kuwa rais.
Balozi Iddi alisema Maalimu Seif ni
mtu muongo na ndio maana hajawahi kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu zaidi ya mara
nne alizoshiriki akiwa mgombea wa CUF.
Alisema Maalim alianza kugombea urais
visiwani humo tangu mwaka 1995, lakini amekuwa akiangushwa na viongozi
mbalimbali kutokana na kutokuwa na ushawishi.
"Naamini Dk. Shein atamwangusha
tena na ninamwambia kama anataka mabadiliko, aanze yeye mwenyewe ndani ya Chama
chake," alisema.
Alisema Maalim ni mtu mbaya na kama
ukitaka kugombana naye, mweleze unataka kugombea ukatibu mkuu wa CUF.
Balozi Iddi alisema mgombea huyo wa
CUF hana sera yeyote ya kuleta mabadiliko na kwamba alichobakia nacho ni kuwa
na sera za uongo kwa wananchi.
CCM yawaombea waliopoteza
vitambulisho wapigekura
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar),
Vuai Ali Vuai amesema CCM imeiandikia barua Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuiomba
iwaruhusu kupigakura wananchi waliopoteza vitambulisho vyao.
Pia, amesema CCM kamwe haiwezi
kutumia sh. bilioni nne kwa ajili ya kununua shahada za kupigiakura kwa
wananchi wa Unguja na Pemba.
Vuai alisema hayo juzi kwenye
mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Paje, ulioko Kusini
Unguja.
Alisema CCM inajiamini katika
uchaguzi huu na ndio maana inaamini itaibuka na ushindi wa zaidi ya asilimia
60.
"Tunawaeleza wapinzani sisi hatuwezi
kutoa fedha ili tushinde kwa kununua shahada za kura na ndio maana tumeiomba
ZEC kuwaruhusu wapigekura wale waliopoteza vitambulisho," alisema.
Vuai alisema kama wangekuwa
wamenunua shahada wasingekubali kuiandikia NEC kuiomba iwaruhusu wale waliopoteza
vitambulisho wapigekura.
Alisema shutuma zinazotolewa kwa CCM
ni sehemu ya kuanza kushindwa kwa CUF na ndio maana wanatoa visingizio vingi.
Katika hatua nyingine, Vuai alisema
Serikali ya Umoja wa Kitaifa imepiga hatua kubwa visiwani humo kutokana na
maendeleo makubwa.
No comments:
Post a Comment