Na Hamis Shimye, Zanzibar
MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein, ameahidi kutoa kompyuta
katika shule za sekondari za Kusini Unguja na kuongeza walimu wa sayansi katika
shule hizo.
Akizungumza katika mkutano wa
kampeni, uliofanyika jimbo la Paje,
Kusini Unguja, jana, Dk. Shein alisema kuongeza idadi ya walimu wa sayansi katika
shule hizo kutasaidia kuongeza ufaulu katika masomo hayo.
"Serikali itaboresha sekta ya
elimu kwa kujenga shule na tayari tunamalizia shule 22, tulizoanza kuzijenga
mwaka jana,”alisema.
Mbali na hilo, alisema wamefanikiwa
kutekeleza ahadi walizoahidi na kusisitiza kuwa ahadi ya maji katika eneo la
Paje kwa baadhi ya maeneo inatarajiwa kumalizika hivi karibuni.
Dk. Shein alisema anaamini mambo
mengi aliyoyaahidi yatamalizika kwa kuwa kila alichokiahidi lazima kitekelezwe
kwa wananchi wa Zanzibar.
Aliwaomba wananchi wa Paje kujitokeza
kwa wingi tarehe ya uchaguzi mkuu na kuhakikisha wanampa kura za kutosha ili
aweze kushinda kwenye uchaguzi huo.
Shamsi awashangaa viongozi wa CUF
ALIYEKUWA Waziri Kiongozi wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, amesema anashangazwa na
viongozi wa CUF kulalamika serikali haitoi ajira wakati Wizara ya Ajira ilikuwa
chini yao.
Nahodha alitoa kauli hiyo juzi kwenye
mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea urais wa CCM wa Zanzibar, uliofanyika katika
uwanja wa Paje, Kusini Unguja.
Alisema katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa
(SUK), wizara za ajira, biashara, utalii, viwanda, viwanja vya ndege na
barabara zilikuwa zinasimamiwa na mawaziri wa CUF.
"Anapotokea mpinzani anayesema
serikali ya CCM haitoi ajira, huyo apimwe akili. Ningekuwa mimi ndiye Maalim
Seif, ningewaita mawaziri wangu na kuwauliza kimetokea nini. Lakini wao kila
mtu ni kulalamika tu, haijulikani kiongozi nani," alisema.
Nahodha alisema CUF wakiulizwa kwa
nini wanashindwa, wanadai sera inayotekelezwa ni ya CCM, lakini kazi ya
upinzani ni kutoa mawazo na kutengeneza sera mbadala.
Alisema alikuwa akiwategemea CUF
kufanya mambo hayo, lakini imekuwa kinyume, badala yake wamekuwa watu wa
kulalamika ovyo bila sababu za msingi.
"Nawaomba ndugu zangu tumpe
kura za kutosha Dk. Shein kwa kuwa ni mtu makini na mwenye uwezo wa kuleta
maendeleo kwa wananchi," alisema.
No comments:
Post a Comment