Thursday, 1 October 2015

WAMESHINDWA





Na Waandishi wetu, DODOMA
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema hana shaka na ushindi wake pamoja na wagombea wa CCM na kwamba, wapinzani tayari wameshindwa.
Aidha, ameonya kuwa ni marufuku kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), kuchukua maeneo ya watu bila kuwapa fidia.
Akizungumza na wakazi wa Dodoma jana, katika Uwanja wa Jamhuri, Dk. Magufuli, alisema imekuwa kawaida kwa CDA kutoa fidia kwa watu katika viwango vya chini.
"CDA imekuwa na kawaida ya kuchukua maeneo ya watu, lakini hawatoi fidia kwa kiwango kinachostahili kwa majibu wa sheria,” alisema Dk. Magufuli.
Aidha, Dk. Magufuli alisema kwamba kumekuwa na mwingiliano wa majukumu kati ya CDA na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.
Dk. Magufuli, ambaye alikuwa akizungumza huku maelfu ya wakazi wa Dodoma wakishangilia, alisema kwamba zipo taratibu kwa mujibu wa sheria za ardhi na mipango miji.
Dk. Magufuli alisema sheria inaeleza kwamba unapotaka kumhamisha mtu katika eneo lake, yapo mambo ya kuzingatia kabla ya kuchukua hatua hizo.
Alisema kabla ya mtu kuchukuliwa eneo lake, lazima alipwe fedha za fidia, za usumbufu na zile atakazokubali hasa pande zote zinapofikia muafaka.
 "Haya yote yanapaswa kuzingatiwa kabla ya watu kuchukuliwa maeneo yao,”  alisema Magufuli.
Alisema kitendo cha CDA kuchukua eneo la ekari 10 kwa kupewa fidia ya viwanja vitatu, si haki.
"Huwezi kuchukua eneo kubwa la namna hiyo, halafu mtu anapewa fidia ndogo, haiwezekani,” alisema.
Dk. Magufuli alisema pamoja na CDA kuwepo kisheria, mambo ya msingi yanapaswa kuzingatiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Kuhusu suala la viwanda, Dk. Magufuli alisema serikali yake itahakikisha inajenga viwanda katika mikoa kulingana na mazao yanayolimwa.

Alisema haiwezekani mkoa kama Dodoma kuwepo na kiwanda cha ngozi au maziwa huku mji huo ukiwa na idadi kubwa ya mifugo.
Alisema kitendo cha kuanzisha viwanda, pia kutawezesha wengi kupata ajira na kukuza uchumi.
"Serikali yangu itaweka mazingira bora katika suala zima la viwanda," aliongeza.
Mgombea huyo aliitahadharisha bodi ya mikopo kubadilika kwa kuwapa mikopo wanafunzi wanaostahili.
Katika kuboresha maslahi ya walimu, alisema serikali yake itaanzisha tume ambayo itashughulikia changamoto zao.
Alisema bodi hiyo inapaswa kutoa mikopo kwa mujibu wa sheria, hasa wanafunzi wenye sifa.
Alisema wanafunzi hao wakipata mikopo hiyo, wanapaswa kusoma siyo kutumia fedha hizo kufanya biashara.
Alisema wanafunzi wa aina hiyo wakibainika na serikali yake, watachukuliwa hatua kwani watakuwa wakiibia serikali.
Katika kuhakikisha anakuza uchumi wa Dodoma, Dk. Magufuli, alisema atahakikisha mapato yanayopatikana, yanatumika kwa kazi hiyo.
Alisema kwa sababu Dodoma ni mkoa ulio katikati ya nchi, atahakikisha anaufanya mkoa huo kuwa jiji.
Alisema Dodoma inaunganisha miji mikuu ya Cairo na Cape Town ya Afrika Kusini.
Alisema hata barabara ya kutoka Babati hadi Dodoma , itamalizwa kwa kiwango cha lami.
"Barabara hiyo ikikamilika itasaidia kukuza uchumi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla.
" Dodoma bado imekuwa kiungo kwa nchi jirani zinapopitisha bidhaa zao kutoka bandari, "alisema Magufuli.
Alisema anaamini baada ya muda mfupi, mkoa wa Dodoma utakuwa kitovu katika uchumi wa Taifa.
Baada ya kuzungumza na wananchi, baadhi ya wananchi walirudisha kadi za vyama vyao, miongoni mwao ni Katibu Mwenezi wa Chadema, Mkoa wa Dodoma.
Kiongozi huyo wa Chadema Mkoa, alisema amevutiwa na Dk. Magufuli, ambaye tangu alipopitishwa kugombea, alimkubali.
Hata hivyo, mwenezi huyo wa Chadema aliyehamia CCM, alisimulia vitisho anavyopata kutoka kwa wanachama wa Chadema kwa uamuzi wake.
Lakini Dk. Magufuli aliwaambia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime kushughulikia vitisho hivyo kwa njia ya meseji.
Kabla ya kuhutubia Uwanja wa Jamhuri, Dk. Magufuli alihutubia mikutano mingine katika miji ya Mpwapwa, Kongwa na Kibaigwa.
Wakataeni wapotoshaji-Warioba
Akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, aliwaasa wananchi kuwakataa na kuwapuuza wagombea ambao hawafahamu historia ya Tanzania.
Alisema wagombea wanaodai serikali ya CCM haijaleta maendeleo katika miaka 54 tangu kupata Uhuru, hawafai kupewa nafasi yoyote ya uongozi na kuwaonya vijana kuacha kuwashabikia.
Alisema ni vyema wagombea hao wakachujwa vizuri kwani, viongozi wote waliotangulia wamefanya mambo makubwa na kuiweka nchi mahali pazuri, ikiwemo kudumisha amani na usalama.
 ‘’Tusikilize hawa wenzetu wanayoongea, lakini tuyachuje kwa umakini… mtu asichafue historia ya nchi hii kwa sababu imetoka mbali na mengi mazuri yamefanyika,” alisema na kuongeza:
“Vijana msiwashabikie wagombea wa aina hii, badala yake mnatakiwa kulinda amani kwani hata hii mnayoiona hivi sasa ililetwa na vijana wakiwemo wakina Mzee Lusinde katika miaka ya 1961.’’
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, alisema hakuna mtu ambaye atasijifu kuwa amemsaidia Dk. Magufuri katika kupata uteuzi wake .
Alisema kutokana na hali hiyo, Dk. Magufuli hana deni na mtu yeyote na ataongoza taifa kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania na kwamba, uteuzi wake umesimamiwa kwa neema za Mungu.
“Hakuna aliyemfikisha hapa Dk. Magufuli, hana deni na mtu zaidi ya kusukumwa na dhamira yake njema ya kuwatumikia watanzania. Kuna watu wameanza kupita mitaani wakidai eti Magufuli ni mkali, hivyo akipewa urais atawabana wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela, alisema mkoa wa Dodoma ni kambi ya CCM, hivyo hakuna sababu ya Dk. Magufuli kukosa kura za kutosha.
Alisema kazi iliyopo mbele ni kuhakikisha Dk. Magufuli anapata ushindi wa kishindo na kwamba, mkoa wa Dodoma wako tayari kuendeleza historia ya kuwachagua kwa kishindo wagombea wa CCM.

No comments:

Post a Comment