NA CHARLES MGANGA, MPWAPWA
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema Tanzania itaendelea kuvutia na kuwapokea wawekezaji na kwamba, wanapokuja nchini wanapaswa kuajiri Watanzania kwanza ili kupunguza tatizo la ajira.
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema Tanzania itaendelea kuvutia na kuwapokea wawekezaji na kwamba, wanapokuja nchini wanapaswa kuajiri Watanzania kwanza ili kupunguza tatizo la ajira.
Pia, amesema serikali imechoshwa na vifo na maumivu yanayosababishwa na mapigano ya wakulima na wafugaji na kwamba, atashughulikia kikamilifu migogoro hiyo.
Akizungumza na wananchi wa
Mpwapwa katika uwanja wa Chuo cha Ualimu, Dk. Magufuli alisema imekuwa kawaida
kwa wawekezaji kuwatumia wafanyakazi kutoka nchi wanayotoka huku Watanzania
wakikosa fursa hiyo.
Dk. Magufuli alisema katika serikali yake ya awamu ya tano, atahakikisha wawekezaji wanapewa sharti la kuajiri wazawa asilimia fulani.
"Imekuwa kawaida wawekezaji kuajiri watu wao hata katika nafasi ambazo watanzania wana uwezo nazo," alisema Dk. Magufuli.
Alisema wawekezaji hao watakapokubaliana na sharti la serikali yake, Watanzania hao watakaoajiriwa walipwe mishahara mizuri kama wafanyavyo kwa raia wa kigeni.
"Tukikubaliana na wawekezaji, mishahara lazima walipwe vizuri na huo ndiyo utakuwa mkakati wa serikali yangu," alisema.
Alisema lengo ni kujenga mazingira mazuri na usawa katika suala zima la uwekezaji.
Aidha, Dk. Magufuli alisema suala la kuhitajika uzoefu kwa wafanyakazi wakati wa kuomba ajira, serikali yake itaangalia uwezekano wa kuondoa vikwazo hivyo kwa wanaoomba kazi.
"Imekuwa kawaida mtu akiomba kazi anaambiwa lazima awe na uzoefu wa miaka mitano, sasa ameipata wapi wakati ndiyo kwanza ametoka chuoni.
"Kwani hata wabunge nao wamepata uzoefu wapi? Mimi nimepata wapi uzoefu wa urais, hilo litaangaliwa," alisema.
Alisema kitendo cha kutoa sharti kwamba lazima mfanyakazi kabla ya kuajiriwa awe na uzoefu, ni mbinu chafu za kuwanyima watu kazi na kwamba kanuni hizi zinapaswa kubadilishwa.
Hata hivyo, Dk. Magufuli alisema atahakikisha anaboresha maslahi ya wafanyakazi wa kada zote, lengo likiwa kuboresha maisha yao.
Alisema kodi ya ajira ya asilimia 11 bado ni kubwa, ikipunguzwa itawanufaisha Watanzania na huo utakuwa mkakati wake wa kwanza ili kuwapa nafuu wafanyakazi wa kada zote.
Aidha, Dk. Magufuli alionyesha kushangazwa na kitendo cha kuhamishwa Chuo cha Utafiti wa Maradhi ya Mifugo kutoka Mpwapwa kwenda Dodoma Mjini.
Alisema kutokana na kitendo hicho, atafuatilia kwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kujua sababu ya kuhamishwa chuo hicho.
"Nasikia Chuo cha Utafiti wa Mifugo, ambacho kilikuwa na wataalamu, kimehamishwa, hili nitalifuatilia kujua sababu," alisema.
Amewataka wananchi wa Mpwapwa na Kongwa, kuachana na siasa za upotoshwaji wa ahadi hewa kutoka kwa wapinzani hasa UKAWA.
Dk. Magufuli alisema inashangaza mgombea wa UKAWA, Edward Lowassa kutoa ahadi ambazo hazitekelezeki na kuwataka Watanzania kupuuza siasa za ulaghai.
Ahuzunishwa na mapigano
Katika hatua nyingine, Dk.
Magufuli ameeleza kuhuzunishwa kwake na mapigano ya wakulima na wafugaji na
kubainisha kuwa hilo litadhibitiwa kikamilifu na kwa usawa.
Akiwa Kibaigwa, Dk. Magufuli alisema kwa muda mrefu nchi imekuwa kisiwa cha amani na kimbilio la wageni hivyo, matukio ya vurugu na mauaji hayastahili.
Aliahidi ili kuondokana na tatizo la wakulima na wafugaji kuvutana kila kukicha, sheria inampa mamlaka ya kugawa ardhi na kwamba, atakuwa tayari kuyagawa maeneo hayo.
"Nikimteua mkuu wa mkoa, wilaya au kamanda wa polisi, mapigano yakatokea, basi nitamtimua. Nataka wakulima walime kwa ufanisi na wafugaji vivyo hivyo," alisema Dk. Magufuli.
No comments:
Post a Comment