Na
Mwandishi Wetu
BAADA
ya kuona maji yamewafika shingoni, Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umeamua kujiuliza
na sasa kuja na mbinu mpya ya kampeni.
Mgombea
wa UKAWA, Edward Lowassa ameonekana kupata tabu sana ya kuhutubia mikutano ya
hadhara na hivyo kuanza kupoteza mvuto kwa hadhira, wakiwamo wanachama na
wapenzi wa vyama vinavyounda umoja huo.
Tabu
hiyo inatokana na kudorora kwa afya yake na hivyo kuwiwa vigumu kunadi sera za
chama chake, ambacho anakipeperushia bendera ya urais, badala yake kumwachia kazi
hiyo mpiga debe wake mkuu, Frederick Sumaye kumpamba na kumwombea kura.
Kwa
hali hiyo, habari kutoka ndani ya UKAWA zimesema leo mgombea huyo na baadhi ya
viongozi wa umoja huo watakutana na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Bahari
Beach, Dar es Salaam, ambako pamoja na mambo mengine, utazinduliwa mkakati mpya
wa kampeni ujulikanao kama ‘Toroka Uje’.
‘Toroka
Uje’ ni kauli mbiu ambayo ilitumika katika mashindano ya soka ya ‘mchangani’,
maarufu kama ‘Ndondo Cup’ , yaliyomalizika hivi karibuni wilayani Temeke, Dar
es Salaam, kwa udhamini wa Dk. Juma Mwaka. Maana ya maneno hayo ni mashabiki
watoroke majumbani mwao kwenda viwanjani kushuhudia michuano hiyo.
Chanzo
chetu cha habari kimesema kikao hicho cha jana usiku, kilitarajiwa kufanya tathmini
ya utendaji wa mgombea huyo kwenye kampeni na jinsi ya kujipanga upya, ambapo
baadhi ya viongozi wa CCM walio wafuasi wa Lowassa watatangaza kujiunga.
“Toroka
Uje itamkumba mwana mama aliyekuwa na nafasi nyeti ndani ya Umoja wa Wanawake
wa CCM, ambaye awali alijipambanua kuwa mmoja wa wafuasi wakubwa wa Lowassa
akiwa CCM,” chanzo hicho kilisema huku kikimtaja jina (linahifadhiwa).
Chanzo
hicho kilisema mama huyo ni mtata hata akiwa ndani ya CCM na huko anakohamia,
bila shaka CHADEMA atawasumbua kwa sababu ana uchu wa madaraka kama alivyo
mgombea wao.
Lakini
pia chanzo hicho kilieleza kuwa mwanasiasa wa siku nyingi nchini, ambaye pia ni
mfanyabiashara, anatarajia kutangaza rasmi kujiunga na UKAWA ingawa alikuwa
akifanyakazi za kimkakati za CHADEMA kwa siri huku akiwa CCM.
“Unakumbuka
hivi karibuni mwanasiasa huyo alilipuliwa kwenye mitandao ya kijamii kwa kutoa ushauri
kwa UKAWA na akaja juu akikanusha na kutishia kushitaki aliyeasisi mawasiliano
hayo ambayo aliyaita ya uzandiki?” kilihoji chanzo hicho.
Hata
hivyo, chanzo hicho kimesikitishwa na wimbi la kupokea watu kutoka CCM, ambao
hawana faida ndani ya UKAWA, badala yake wanaingia kuwafunika watu waliomwaga
damu na kutoka jasho kuzijenga CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
“Angalia,
hivi watu kama Makongoro (Mahanga), Msindai (Mgana), Guninita (John) wana faida
gani UKAWA tangu wahamie, kama si mizigo na kuziba nafasi za ‘wazawa’ wa vyama
hivi vinavyounda UKAWA? Hivi tukishindwa wataendelea kubaki UKAWA?” Kilihoji
chanzo hicho.
Siku
za karibuni, Lowassa amekuwa akishindwa kuhutubia mikutano ya hadhara ya
kampeni na badala yake hutafutwa visingizio vya kuahirishwa mikutano.
Ilitokea
Geita na kutoa kisingizio cha vipaza sauti havifanyi kazi huku aliyetangaza
kuahirisha akisikika; Nako Tanga mkutano uliahirishwa kwa madai kuwa watu zaidi
ya 100 walizirai kutokana na msongamano uwanjani ili kumwona Lowassa.
Afya
ya mgombea huyo imeendelea kutatiza kutokana na kazi ngumu ya kampeni licha ya
kushauriwa na madaktari kupumzika. Mahali ambako aliweza kuhutubia, hakuzidisha
dakika tano, ambazo wananchi walitazamia kumsikiliza akimwaga sera, lakini
akaishia kujisifu mahudhurio na kuomba kura.
WAFUASI
WAZIDI KUIKIMBIA UKAWA
VUGUVUGU
la Kundi la Magufuli kwa Maslahi ya Umma (M4PI), limeingia jijini Mwanza na
kubomoa ngome ya UKAWA baada ya watu 189, wakiwemo vigogo kutoka kundi la ‘Team
Lowassa’ na wanachama wa vyama mbalimbali kujiunga na CCM.
Wanachama
hao kutoka CHADEMA, ACT Wazalendo, UDP, CUF na Jahazi Asilia, walijiunga na CCM
kwenye mkutano wa M4PI uliofanyika katika Hoteli ya New Mwanza, jana na kuamsha
ari mpya ya ushindi wa CCM pamoja na mgombea wake wa urais, Dk. John Magufuli.
Akizungumza
katika mkutano huo, Mwenyekiti wa M4PI Taifa, Donatus Rutagimbwa, aliasa kuwa
itikadi za vyama zisiwanyime Watanzania viongozi bora, wachapa kazi na
waadilifu kama Dk. Magufuli.
Rutagimbwa,
ambaye mara kwa mara alikuwa akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria
mkutano huo, alisema kikundi chake hakifungamani na itikadi ya chama chochote,
wanaangali maslahi ya taifa ndiyo maana wanazunguka nchini kuhamasisha Watanzania
wachague viongozi bora hususan Dk. Magufuli.
“Leo
tumekutana hapa kwa ajili ya kuwapokea watu wanaojiunga timu ya Magufuli For
Public Interest (Magufuli kwa Maslahi ya Umma), tumeweka pembeni itikadi za
vyama vyetu, kabila zetu, dini zetu, tunataka maslahi ya taifa, tutaanza
kuelimisha watu nyumba kwa nyumba, kwa nini Magufuli,” alisema.
Alifafanua,
kati ya wagombea urais wote, Dk. Magufuli pekee ndiye ana sifa stahili, anaweza
kusimamia maslahi ya Tanzania kwa ajili ya Watanzania wote, tofauti na Edward
Lowassa, anayetafuta urais wa shoo kwa ajili ya maslahi yake na watu wachache
wanaomzunguka.
Msimamizi
wa M4PI taifa, Jacqueline Mzindakaya, alisema wafuasi hao 189 wamejiunga na kikundi
hicho baada ya kutafakari kwa kina toka kampeni za uchaguzi mkuu zianze,
wakabaini Lowassa, aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, hastahili kuwa rais wa
Tanzania inayoondoka kwenye umaskini, ataididimiza tena kwenye umaskini.
Kati
ya wafuasi hao, wamo waliokuwa katika makundi ya Team Lowassa, Friends of
Lowassa, 4U Movement, Bodaboda na Shirika la Wamachinga Mwanza, ambao yalikuwa
yakimpiga kampeni mwanasiasa huyo.
Akizungumza
kwa niaba ya Friends of Lowassa, Yohana Chacha, ambaye ni Mwenyekiti wa Shirika
la Umoja wa Machinga Mwanza, (SHIUMA), alisema vijana wasitumike ovyo,
wataliangamiza taifa kwani Lowassa hana sifa za kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa
Tanzania.
No comments:
Post a Comment