NA
CHRISTOPHER LISSA
SISI waafrika ni watu wa ajabu sana. Unajua ni wadogo,
lakini nasema, ni udogo wa mawazo. Umaskini wa mawazo ni umasikini mbaya kupita
wote.
Unaweza ukawa na almasi mfukoni, akaja tapeli na kijiwe
kimetengenezwa kama almasi, akakuambia: “Ebu tuone almasi yako. Bwana aa! Hii
ya kwako sio almasi ni chupa tu, almasi ni hii.”
“Mkabadilishana. Yeye akachukua almasi yako na akakuachia
kichupa na ukatoka hapo unashangilia kama zuzu!”
Hayo si maneno yangu bali ni ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu
Nyerere katika moja ya hotuba zake.
Maneno haya yamegeuka kweli hasa katika kipindi hiki cha
mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Inashangaza kuona wafuasi wa genge la UKAWA wakipiga vifua vyao kumshangilia mgombea
urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, wakiamini fika kuwa ni almasi ambayo inathamani kubwa inayoweza kufikia
thamani ya kuinunua Ikulu.
Inauma kuona watu hawa hasa vijana wa mjini waliokuwa
wakionekana wajanja, ‘wamepigwa changa la macho’ mchana kweupe na viongozi wao
wajanjawajanja, wanaojinufaisha kupitia
mgongo wa Lowassa, kwa kuamini kuwa
mgombea huyo ni almasi waliyoichukua kutoka CCM na wafuasi
wanashangilia.
Kama alivyosema
Nyerere hapo juu, UKAWA wamedanganywa na
kipande cha chupa ‘Lowassa’ huku wakiikataa
almasi halisi ambayo ni mgombea wa CCM,
Dk. John Magufuli ‘Tingatinga’.
Rais wa zamani wa Marekani Hayati John Kennedy aliwahi kusema: “Usiulize Marekani itakufanyia
nini, jiulize wewe utaifanyia nini Marekani?”.
Magufuli ni almasi kwa sababu amefanya mambo mengi ya
thamani kubwa na hana makandokando yanayawoweza kuwa sumu kubwa kwa mustakabali
wa taifa hili. Yanaonekana kwa macho.
Ni dhambi kulinganisha
thamani ya almasi ‘Magufuli’ na kipande cha chupa yao? Tena kipande hiki kilimeguka kutoka kwenye chupa iliyokuwa
imejaa sumu kali ya ufisadi uliotafuna taifa hili na kutesa wananchi, kabla ya chupa hiyo
kuvunjwa vunjwa kisha kutupwa katika
lundo la makapi, kisha viongozi wa UKAWA kuiokota na kuwapelekea wafuasi wao na
kuwadanganya kuwa wameokota almasi.
Ajabu wafuasi wanashangilia
kipande cha chupa ambacho wanaamini watakibadilisha kwa Watanzania kwa
thamani ya nchi yao. Haiwezekani.
Picha tu ya mikutano ya kampeni ya UKAWA inayoendelea inadhihirisha
thamani ‘sifuri’ ya Lowassa. Amekuwa
akisitiriwa sana na wapambe wake ili kumlindia heshima.
Ni kioja UKAWA kudai eti Lowassa ameahirisha mkutano Tanga ili kuepusha maafa kwa sababu mkutano ulijaa sana na majeruhi walikuwa wengi .
Hivi watu wenye akili timamu wenye lengo la kusikiliza sera
za mgombea makini wa Chama chao, wakiwa uwanjani watajeruhiwa vipi kama kweli wote ni watu
wenye akili timamu na mkutano umeandaliwa na viongozi wenye akili
timamu? Huu si usanii jamani?
Tena Lowassa anaahirisha mkutano huo kwa kusema ‘Naombeni
kura zenu. Mtanipa kura?” Yaani hilo tu basi?
Harakati zote za Lowassa zinadhihirisha fika uchu binafsi alionao wa kwenda Ikulu.
‘Ikulu hapakimbiliwi. Hakuna Biashara Ikulu. Lowassa anayetaka
kwenda Ikulu kutaka faida yoyote Ikulu pale, hatufai hata kidogo.
‘Najua kwa mtu halisi kabisa, Ikulu ni mzigo. Hupakimbiliwi.
Si mahali pa kupakimbilia hata kidogo, huwezi kupakimbilia Ikulu.
‘Unapakimbilia kwenda kutafuta nini? Ni mgogoro, ni mzigo
mkubwa kabisa. Pazito pale. Huwezi kupakimbilia na watu safi hawapakimbilii.
‘Ukiona mtu anapakimbilia Ikulu na hasa anapotumia vipesa
kwenda Ikulu, huyo ni mtu wa kuogopa kama ukoma.
‘Mtu yeyote anayeonekana anapenda sana kwenda Ikulu na hata
yupo tayari kununua kura ili kumwezesha kufika Ikulu, ni wa kumkwepa kama
ukoma.
‘Kwanza, hizo fedha kapata wapi? Mtanzania wa leo hawezi
kununua watu bila kwanza yeye kununuliwa. Na kama kanunuliwa, atataka
kuzilipaje? Kazipata wapi?
‘Watanzania wote ni masikini tu. Mtanzania anaomba urais
wetu kwa hela, amezipata wapi?
‘Pili, kama hajanunuliwa, kazipata wapi? Kama kakopa,
atarudishaje? Ikulu pana biashara gani mtu akope mamilioni halafu aende ayalipe
kwa biashara ya Ikulu?
‘Ikulu mimi nimekaa kwa muda wa miaka ishrini na mitatu.
Ikulu ni mahali pazito. Kuna biashara gani Ikulu?
Haya ni maneno yaliyotamkwa na Mwalimu Nyerere, akiwausia
watanzania kuwa makini na wanasiasa wanaopigana kufa na kupona ili waende
Ikulu.
Ni maneno yaliyotamkwa miaka mingi iliyopita, lakini bado
yana maana kubwa kwetu. Watanzania tuamke. Tuzinduke. Tusikubali kutumiwa.
No comments:
Post a Comment