Na Angela Sebastian, Bukoba
MKUU wa Mkoa wa Kagera, John Mongella, amewataka
wasimamizi wa uchaguzi wa mikoa ya Kagera na Geita, kutoonyesha hisia zao za
kisiasa kipindi hiki cha uchaguzi hata kama wana mapenzi na chama fulani.
Aidha, aliwataka kuhakiki vifaa vya kupigiakura ili
kuepuka makosa na dosari zilizojitokeza katika uchaguzi uliopita.
Mongella, alitoa agizo hilo jana, wakati wa mafunzo ya
siku mbili kwa wasimamizi wa uchaguzi, waratibu wa uchaguzi wa mikoa na
wasimamizi wasaidizi wa majimbo yanayofanyika uchaguzi mjini hapa. Mafunzo hayo
yanaendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Mongella aliwataka wasimamizi hao wahakikishe wana hakiki
majina ya wagombea, vifaa na fomu mbalimbali baada ya kuvipokea kutoka NEC, ili
kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza.
Alisema anafahamu kuwa kila mtendaji ana mapenzi na chama
fulani, lakini aliwataka wasionyeshe mapenzi yao wakati huu wa uchaguzi, badala
yake wafanyekazi kwa haki ili mgombea apate haki yake.
Mkuu huyo wa mkoa aliwataka wasimamizi hao kuwaelimisha
mawakala ili kujua kazi zao na kwamba hawapaswi kuingilia kazi za watendaji
walio vituoni.
Aliwaagiza wasimamizi wa uchaguzi kuendelea kutoa elimu
kwa wananchi juu ya utunzaji wa shahada zao za kupigiakura.
Ofisa wa NEC, Kanda ya Ziwa, Deogratius Nsazugwanko,
alisema elimu inayotolewa kwa waratibu na wasimamizi wa uchaguzi ni ya mwisho,
ambapo watajifunza mambo mbalimbali, yakiwemo wajibu wa msimamizi wa uchaguzi
vituoni, fomu zinazotumika, kuhesabu kura na kujumlisha kura.
No comments:
Post a Comment