Tuesday 20 October 2015

DK. MAGUFULI AICHARUKIA HALMASHAURI YA NYANG'WALE


Na Peter Katulanda, Sengerema

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk John Magufuli ameionya Halmashauri ya wilaya ya Nyang’wale mkoani hapa iachane na mpango wa kukopa sh Milioni 700 katika Benki CRDB, utaumiza wananchi.

Amesema, mpango huo hauna tija kwa wananchi wa wilaya hiyo mpya maana itaibidi iwakamue wananchi kulipa riba ya mkopo huo na kuchelewesha maendeleo ya wananchi.

Halmashauri hiyo ilikuwa ikitarajia kukopa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kulipa fidia ya ardhi na mali za wananchi wanaopisha ujenzi wa makao makuu ya wilaya pia nyumba za watumishi.

Dk Magufuli alisema hayo jana wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa wilaya ya Nyang’wale kwenye Kijiji Nyijundu mkoani Geita, ambao licha ya mvua kubwa kunyesha katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo walijitokeza kwa wingi katika mkutano huo.

“…nasema huo mpangoa wa kukopa fedha CRDB achaneni nao, kama mmekosa fedha za kulipa fidia subirini zimebaki siku tano ..orodheshani majina ya wananchi hao mimi nitaleta fedha mlipe,” alieleza.

Aliamsha shangwe  na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi hao aliposema riba ya asilimia 18 itakayolipwa kutokana na mkopo huo ni kubwa watakamua na kuumiza wananchi.

“Sitaki kuwaingilia… lakini wananchi wanahitaji madawa mahospitali, kwenye zahanati, madawati shuleni na huduma nyingi mbalimbali, kama mmekosa fedha  mimi ntakapokuwa rais ntawalipa hiyo ndiyo kazi yangu ya kwanza hapa,”

Dk Magufuli pia aliahidi atakaopchaguliawa kuwa rais wa awamu ya tano atajenga nyumba za wafanyakazi wa halmashauri hiyo kupitia Wakala wa Ujenzi wa Nyumba za serikali (TBA) chini ya Wizara yake ya Ujenzi ili mapato ya wilaya hiyo yatumiwe kuhudumia wananchi badala ya kulipa fidia ya mkopo usiokuwa na tija au ulazima kama huo.

DkK Magufuli aliyewasili mkoani hapa juzi akitokea mkoani Mwanza na kupokewa kwa shamrashamra na maelfu ya wananchi wa Geita vijijini na mjini, pia alipata mapokezi makubwa na ya heshima kuliko mgombea yeyote wa urais katika wilaya hiyo ya Nyang’wale na Sengerema.

Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano mwingine mkubwa uliofanyika kwenye uwanja wa Mnadani, Dk Magufuli alisisitiza kuwa ahadi ya ujenzi wa barabara za Sengerema- Kamanga, Sengerema-Nyehunge hadi Nkome kwa kiwango cha lami, iko pale pale.

Pia alisema atakaopingia Ikulu ataagiza na kusimamia mradi wa maji kutoka katika ziwa Victoria unaoendelea kutekelezwa mjini Sengerema, uende haraka na kuondoa kabisa kero ya upungufu wa maji unaoukabili mji huo mdogo.

Akiwa katika ziara ya wilaya hizo, Dk Magufuli alizuiwa na wananchi wa vijiji vya Kasamwa, Busolwa, Ngoma, Nyanchenche, Tunyeye, Balatogwa na Mtaa wa Ntatukara, Nyapande, Busisi, Kigongo (wilayani Misungwi) na kulazimika kuwasalimia kabla ya kupokewa tena kwa shangwe na mamia ya wananchi wa jiji la Mwanza.

No comments:

Post a Comment