Thursday 22 October 2015

MAGUFULI AMALIZA KAZI DAR


JIJI la Dar es Salaam jana lilizima baada ya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli kufanya mikutano mitano ya kampeni katika majimbo matano tofauti na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Dk. Magufuli, ambaye aliwasili Dar es Salaam, saa 3.30 asubuhi kwa ndege, akitokea Mwanza, alianza mkutano wake katika wa kwanza katika jimbo la Kigamboni na kufuatiwa na mikutano mingine iliyofanyika katika majimbo ya Mbagala, Temeke, Ubungo na Kinondoni. Pia alifanya mikutano midogo mitatu kutokana na kuzuiwa barabarani.

Katika mikutano hiyo, ambayo Dk. Magufuli alitumia zaidi ya saa tano kuwahutubia wananchi, alisema ameshaanza kusikia harufu ya urais kutokana na mikutano yake kufurika mamia ya wananchi na kuahidi kumpigia kura nyingi.

Aidha, Dk. Magufuli aliwataka wananchi wasiwachague viongozi wenye maamuzi magumu, badala yake wachague viongozi makini, katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, unaotarajiwa kufanyika Jumapili kote nchini.

Mgombea huyo pia aliwaeleza wananchi hao kuwa, Tanzania inahitaji kuwa na rais mkali ili mambo yaweze kwenda mbele, vinginevyo nchi itakwama.

Pia aliapa kumshughulikia kigogo mmoja wa serikali, aliyekwamisha kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji katika Jiji la Dar es Salaam, kutokana na kuifungulia kesi serikali mahakamani ya kupinga nyumba yake kubomolewa ili kupisha mradi huo.

Akihutubia mkutano wake wa kwanza uliofanyika Kigamboni, kuanzia saa 4.07 hadi saa 4.57, asubuhi, Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi kuwa, atakapokuwa rais, ataruhusu Daraja la Kigamboni kutumika bure kwa wanaotembea kwa miguu.

Hata hivyo, mgombea huyo alisema ruhusa hiyo haitawahusu wamiliki wa magari kwa vile watalazimika kulipia gharama za kuvuka kwenye daraja hilo kwa kutumia vyombo vyao vya usafiri.

Aidha, mgombea huyo aliahidi kuupa mji wa Kigamboni hadhi ya kuwa wilaya ili uweze kuwa na maendeleo makubwa zaidi kutokana na mipango inayofanywa na serikali ya kuufanya mji huo uwe mpya.

"Kigamboni inastahili kuwa wilaya, nitakapokuwa rais, nitalishughulikia suala hilo, sitawaangusha, nitawabeba,"alisema Dk. Magufuli huku akishangiliwa kwa mayowe mengi na wananchi.

Mgombea huyo alikanusha madai kuwa, wananchi wanaomiliki ardhi katika mji huo watanyang'anywa ili wapewe wawekezaji. Alisema jambo hilo si la kweli na kwamba wananchi wapo huru kuuza ardhi yao ama kuingia ubia na wawekezaji na kwamba wale, ambao maeneo yao yatachukuliwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu watalipwa kulingana na thamani ya maeneo yao.

Kutokana na mabadiliko yanayotaka kufanywa na serikali katika mji huo, Dk. Magufuli aliahidi kuwa serikali yake itajenga hospitali kubwa na yenye hadhi ya wilaya, ambayo itakuwa na huduma na vifaa vyote muhimu vya tiba.

Dk. Magufuli alisisitiza kuwa siku zote maamuzi yake ni makini kwa sababu lengo lake kubwa ni kuwaendeleza Watanzania, hasa waliomasikini ili waondokane na hali hiyo.

Akimtambulisha mgombea ubunge wa Kigamboni mwa wananchi, Dk. Faustine Ndugulile, alimwelezea kuwa ni muwazi, mchapakazi na anayependa watu, hivyo aliahidi kumbeba kwa nguvu zake zote.

Msafara wa mgombea huyo ulipokewa kwa furaha kubwa na umati wa wananchi waliolipuka mayowe ya kumshangilia na kuimba 'rais, rais, rais.'

Kutokana na kufurahishwa na mapokezi hayo, Dk. Magufuli alisema anataka kushinda uchaguzi wa mwaka huu wa kishindo kwa kupata asilimia 99 na asilimia moja iliyobaki wagawane wapinzani.

Aidha, alisema mapokezi hayo yamemfanya aanze kusikia harufu ya urais, lakini aliwataka wananchi wasianze kushangilia, badala yake wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi kwenda kupiga kura.

Akihutubia mkutano uliofanyika Zakhem, Mbagala, kuanzia saa 5.32 hadi saa 6.21, mchana, mgombea huyo alisema jimbo hilo litaongezewa barabara za lami kutokana na fedha za mfuko wa barabara kuongezeka.

Aidha, alisema serikali haina mpango wa kulivunja soko la Mbagala, badala yake italipanua ili kulifanya la kisasa zaidi na kutoa huduma kwa watu wengi.

Aliwaambia wakazi wa jimbo hilo, mabadiliko ya kweli yanapatikana kwa kufanyakazi na kuwaletea maendeleo wananchi kwa kuwapelekea huduma za maji, umeme na afya ili kuboresha maisha yao.

Aliwatahadharisha wananchi hao waepuke kuwachagua viongozi wenye maamuzi magumu kwa sababu yanaweza kusababisha madhara mbalimbali kwa jamii. Badala yake aliwataka kuchagua viongozi wenye maamuzi makini.

Katika mkutano huo, Dk. Magufuli aliwatambulisha kwa wananchi, mgombea ubunge wa CCM, Murtaza Mangungu na mgombea wa udiwani wa kata ya Kigamboni, Yussuf Manji.

Wakati msafara wake ukiondoka Mbegala kwenda Temeke, baadhi ya wananchi waliusindikiza kwa maandamano huku wakiimba 'rais, rais, rais'.

Akihutubia mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, mgombea huyo alisema Tanzania inahitaji kuwa na rais mkali ili mambo yaende mbele.

Alisema iwapo rais atakuwa mpole na kuwaacha watendaji kufanya wanavyotaka, itakuwa ndoto kwa nchi kupata maendeleo.

Katika mkutano huo, Dk. Magufuli alimtambulisha kwa wananchi mgombea ubunge wa Temeke, Abbasi Mtemvu.

Kivutio kikubwa kwa mgombea huyo kilikuwa wakati aliposimamisha msafara wake eneo la mataa ubungo, na kuwasalimia wafuasi wa CHADEMA na CCM, waliokuwa wamejipanga barabarani.

Wakati akizungumza na wananchi hao, baadhi ya wafuasi wa CHADEMA walikuwa wakitamka maneno 'peoples power', lakini walizidiwa nguvu na wenzao wa CCM waliokuwa wakiimba 'rais, rais, rais.'Wafuasi hao waliusindikiza msafara wa Dk. Magufuli hadi eneo la darajani.

Msafara wa Dk. Magufuli pia ulisimama katika maeneo ya Shekilanga na Sinza Kijiweni, ambako mamia ya wananchi walijipanga barabarani, wakiwa na kiu ya kumuona na kumsikiliza. Muda wote alipokuwa akiwahutubia, wananchi hao walikuwa wakiimba 'rais, rais, rais.'

Fungakazi ilikuwa pale mgombea huyo alipowasili kwenye uwanja wa TP, Sinza, Dar es Salaam, ambako alipokelewa kwa shamrashamra nyingi na kuwahutubia wananchi wa jimbo la Ubungo.

Katika mkutano huo ulioanza saa 8.24 mchana, Magafuli aliwaeleza wananchi kuwa amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata, ikiwa ni pamoja na kuwapongeza viongozi wa CHADEMA na CUF kwa kuupamba mji kwa bendera za vyama vyao, ikiwa ni ishara ya kumpokea na kumkubali.

Alisema mapambo hayo yamedhihirisha wazi kuwa vyama hivyo viwili, ambavyo ni miongoni mwa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), vinamkubali na kutambua kuwa ndiye rais ajaye wa awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika mkutano huo, Dk. Magufuli alimnadi mgombea ubunge wa CCM katika jimbo la Ubungo, Didas Masaburi na kumuombea kura ili aweze kushirikiana naye kuwaletea wananchi maendeleo.

Dk. Magufuli alihitimisha mikutano yake siku ya jana, kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara kwenye viwanja vya Biafra, Jimbo la Kinondoni, wilaya ya Kinondoni, ambao ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi, waliokuwa wamevaa sare za njano na Kinondoni.

Akihutubia mkutano huo, Dk. Magufuli alisema anakerwa na kitendo cha kigogo mmoja wa serikali, kufungua kesi mahakamani kupinga amri ya kuibomoa nyumba yake ili kuwezesha mradi mkubwa wa maji katika Jiji la Dar es Salaam.

Alisema kitendo cha kigogo huyo kufungua kesi mahakamani na mahakama kuchelewa kutoa uamuzi, kimesababisha wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wakose huduma ya maji safi na salama, huku wengine wakifa kutokana na ugonjwa wa kipindupindu.

"Yupo tajiri mmoja amejenga nyumba yake juu ya mabomba, alipoambiwa aibomoe, aliipeleka serikali mahakamani, kesi hadi leo inaendelea, haijulikani lini itatolewa uamuzi na wananchi wanaendelea kupata shida.

"Watu wanakufa kwa kipindupindu, wanakosa maji safi, wao wanakunywa maji safi. Hivi watu hawa watakwenda kusema nini kwa Mungu.

"Ningekuwa mimi waziri wa maji, ningeibomoa ile nyumba kisha niende kufungwa kwa ajili ya kuwatetea wananchi wangu. Hata hivyo, zimebaki siku tano kabla sijawa raisi. Watu wanasema mimi mkorofi, lakini mimi si mkorofi, wakorofi ni waliofungua kesi na wanaochelewa kutoa uamuzi,"alisema.

Alisema iwapo mradi huo ungekuwa umeshaanza, Jiji la Dar es Salaam, lingekuwa linapata lita milioni 700 za maji kwa siku, ambazo zingeweza kuwahudumia wakazi wote wa Jiji na kumaliza kabisa tatizo la maji.

Dk. Magufuli alisema atakapokuwa rais, hataruhusu mambo kama hayo na kwamba, akiwa waziri wa ujenzi, amewahi kuwatimua wakandarasi 3,230 na wafanyakazi 400 wa mizani kwa makosa ya kupokea rushwa.

"Ndio maana nasema nipeni urais. Mniamini, nikafanyekazi, msiseme nimeshapata urais, nendeni mkanipigie kura,"alisema Dk. Magufuli.

Mgombea huyo pia alizungumzia tatizo la kukatika mara kwa mara nchini, ambalo alieleza wazi kuwa linatokana na hujuma za wazi zinazofanywa na vigogo wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa kufungulia maji kwenye mabwawa ya umeme ili wapate tenda ya kununua mafuta.

"Nikiwa rais, umeme utapatikana kwa uhakika, najua hii ni hujuma ya ajabu, watu wanafungulia maji makusudi. Najua vitu vingi sana katika nchi hii, ndio maana nataka mnipe urais ili niwashughulikie watu hawa,"alisema huku akionekana dhahiri kukerwa na vitendo hivyo.

Katika mkutano huo, Dk. Magufuli alimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Kinondoni, Iddi Azzan pamoja na wagombea wa udiwani.

Wakati huo huo, Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, amefichua mbinu zinazotaka kufanywa na UKAWA, kumteka nyara mgombea urais wa umoja huo, Edward Lowassa, ili aonekane amepotea katika mazingira ya kutatanisha.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika jana kwenye viwanja vya Biafra, Kinondoni, Shaka alisema CHADEMA pia imepanga kuwavalisha nguo za CCM vijana wake ili wakafanye vurugu mitaani siku ya kupiga kura.

Alisema njama hizo zinazofanywa na chama hicho, ni uthibitisho wa wazi wa kushindwa kwao mapema katika uchaguzi huo na kuwataka wananchi mara baada ya kumaliza kupiga kura, warejee nyumbani kwao.

Alisema ushindi kwa CCM katika uchaguzi huo ni wa dhahiri na itashinda kwa amani, haki, usawa na demokrasia kutokana na kukubalika kwa mgombea wake, Dk. John Magufuli.

Shaka alisema katika kipindi chote cha kampeni, Dk. Magufuli ameonyesha uwezo mkubwa wa kuinadi vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM na hicho ndicho Chama Cha Mapinduzi, kilichoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Rais wa zamani wa Zanzibar, Hayati Abeid Amaan Karume.

"Waende ardhini na mbinguni, CCM itashinda kwa kishindo Oktoba 25, mwaka huu,"alisema kiongozi huyo wa UVCCM.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema mgombea anayekubalika na kusema ukweli, ndiye anayepaswa kuchaguliwa na wananchi katika uchaguzi mkuu wa Jumapili.

Asha-Rose alisema siku zote za kampeni, Dk. Magufuli amekuwa akisema ukweli na kwa kutumia takwimu, hivyo ndiye mgombea mwenye sifa ya kuchaguliwa kuwa rais wa nchi.

Aidha, aliwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuichagua CCM, kutokana na Chama kutoa fursa kwa mwanamama, Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea mwenza wa urais.

"CCM ilitoa fursa kwa wanawake wawili kuingia hatua ya tatu bora na Dk. Magufuli amemteua Samia kuwa mgombea mwenza wake,sasa kwa nini tusijitokeze kwenda kupiga kura?" Alihoji.

Aliwataka wananchi wasiwapigie kura viongozi wababaishaji, wanaoendeleza udini, ukabila na kula rushwa kwa vile hawana uwezo wa kuwaletea wananchi maendeleo.

Naye Waziri Mkuu mstaafu, jaji Joseph Warioba, alisema Chama hakikufanya makosa au kukiuka katiba katika kufanya uteuzi wa mgombea urais wa CCM.

Alisema taratibu zilizotumika mwaka huu, ndizo zilizotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, ambapo naye alikuwa miongoni mwa waliojitokeza kuwania urais, lakini alitolewa hatua za awali.

Aidha, alisema kwa vile mgombea urais wa UKAWA, ametoka CCM na anapigiwa debe na waliotoka CCM, hawezi kuwa na lolote jipya, hivyo ni vyema wananchi wamchague mgombea aliyesimamishwa na Chama.

Alizielezea kauli za Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kwamba CCM imeishiwa pumzi kwamba hazina ukweli wowote kwa sababu, mgombea wa Chama, Dk. John Magufuli, hajaishiwa pumzi na ametembea umbali mrefu kwa ajili ya kuomba kura.

"Magufuli ana pumzi, ametembea miezi miwili kwa barabara kwa ajili ya kuomba kura
na kuhutubia mikutano yake kwa kutumia zaidi ya saa moja, je huyo hana pumzi? Na sijui kama alikuwa anapata muda wa kupumzika,"alisema.

Alisema Dk. Magufuli anaielewa vyema Tanzania kutokana na uzoefu wake wa kuwa waziri na mbunge kwa miaka 20, hivyo ndiye anayefaa zaidi kuwa rais wa nchi kuliko wagombea wengine wa upinzani.

Dk. Magufuli, ambaye ameshatembelea mikoa yote 31 ya Tanzania, na umbali wa kilometa zaidi ya 42,000, anatarajiwa kuendelea na mikutano yake ya kampeni leo katika jimbo moja la Dar es Salaam na mengine mawili yaliyoko mkoa wa Pwani.

No comments:

Post a Comment