Thursday, 1 October 2015

UCHAGUZI UTAFANIKIWA MISINGI IKISIMAMIWA-EU




NA WILLIAM SHECHAMBO

UCHAGUZI Mkuu wa Oktoba 25, utafanikiwa kwa kiasi kikubwa endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyama vya siasa vitasimamia misingi
waliyoianisha kwenye vikao maalumu kati yao na waangalizi wa kimataifa
wa uchaguzi siku chache zilizopita.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Mkuu wa jopo la Waangalizi
wa Uchaguzi Mkuu kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Judith Sargentini,
alipozungumza na waandishi wa habari kwenye uzinduzi wa uangalizi wao
hapa nchini.

Alisema tangu kuwasili kwake nchini mwanzoni mwa wiki hii, amefanya
vikao na viongozi wa kiserikali, wawakilishi wa baadhi ya vyama vya
siasa vinavyoshiriki uchaguzi wa mwaka huu na viongozi wa NEC, akiwemo
Mwenyekiti Jaji Damian Lubuva na kwamba maandalizi ni mazuri.

“Nimekutana na NEC, vyama vya siasa hapa Dar es Salaam na Zanzibar na
bado ninaendelea kufanya hivyo, ambapo baadaye leo (jana) nitakutana na
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, lakini kiujumla uchaguzi
unaonekana utakuwa mzuri,” alisema Judith.

Mkuu huyo wa ujumbe wa waangalizi hapa nchini kwa mwaka huu, ambaye pia ni Mbunge wa Bunge la Ulaya, alisema ni heshima kwake
kufuatilia mwenendo wa uchaguzi mkuu nchini ambao unaonyesha hatua kubwa ya nchi kwenye ukuaji wa demokrasia.

Alisema imani yao kama waangalizi maalumu ni kuwa na mchango mkubwa
katika  kuwachagua viongozi wa serikali ya awamu ya tano ya
Tanzania, ambao utakuwa shirikishi na  wa wazi na amani kwa manufaa ya
Watanzania.

Pia alisema waangalizi waliwasili kwa makundi nchini kuanzia Septemba
11 mwaka huu, kufuatia mialiko kutoka serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na NEC, ambao kwa ujumla wao wameshatawanywa kwenye mikoa mbalimbali kuangalia mwenendo wa maandalizi ya uchaguzi.

“Tulianza kufika tangu Septemba 11, mwaka huu, na tayari waangalizi takriban 34 wametawanyika mikoa mbalimbali kuanza majukumu yao husika. Wanakutana na maofisa wa uchaguzi, wagombea majimboni na wawakilishi wa asasi za kiraia, ili kuhakikisha kazi inakwenda vizuri,” alisema.

Pamoja na hayo alisema jopo hilo ambalo limegawanyika kwenye makundi
mawili ya wale wa muda mrefu na wa muda mfupi, litaendelea na
uangalizi wao kabla ya uchaguzi kama wanavyoendelea kufanya sasa,
wakati wa upigaji kura na baada ya matokeo watakuwepo nchini kwa wiki
sita tangu kutangazwa kwa matokeo husika.

Alisema miezi miwili baada ya uchaguzi wataandaa taarifa maalumu ya uangalizi walioufanya tangu kuwasili hapa nchini.

No comments:

Post a Comment