Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi, Tarime
MKUU wa Jeshi la Polisi
nchini, Ernest Mangu, amewataka viongozi wa vyama vya siasa katika Wilaya za
Tarime na Rorya, kufanya kampeni za kistaarabu ili kufanikisha uchaguzi mkuu na
kuimarisha amani na usalama wilayani humo.
IGP Mangu aliyasema hayo wakati alipozungumza na wadau
wa polisi, wakiwemo viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na wagombea ubunge
na udiwani.
Aliyasema hayo alipokuwa katika ziara ya kikazi katika
Kanda Maalumu ya Polisi Tarime na Rorya.
“Ili uchaguzi wa mwaka huu uweze kufanyika kwa amani,
viongozi wa vyama vya siasa na wagombea hawana budi kuwashawishi wafuasi wao
kufuata maadili ya uchaguzi, ikiwemo kutotoleana lugha
za matusi.
“Baada ya uchaguzi maisha yataendelea kama kawaida,
hivyo ni jukumu la wananchi wote wa Tarime kuondoa uhasama katika mambo ya
siasa kwa kuwa siasa sio uhasama,” alisema.
Aidha, aliwashauri wagombea ubunge na udiwani katika
majimbo ya Tarime Mjini, Vijijini na Rorya, kukutana mara kwa mara ili kujenga
kuaminiana na kutatua changamoto zinazojitokeza katika kipindi hiki cha kampeni
na hatimaye siku ya uchaguzi mkuu.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi wa
Polisi (ACP), Lazaro Mambosasa, aliwahakikishia wadau wote kuwa Jeshi la Polisi
limejipanga vema kukabiliana na vitendo vyote vya vurugu vitakavyojitokeza.
Mambosasa alisema watahakikisha kwamba kila mwananchi
aliyejiandikisha anapata fursa ya kupigakura bila vitisho vya aina yoyote.
Naye mgombea ubunge katika Jimbo la Rorya kwa tiketi ya
CCM, Lameck Airo, alisema katika jimbo analogombea, hakuna vurugu kwa kuwa
wamekuwa wakiheshimiana katika kampeni ili kuepusha vurugu kwa wagombea na
wafuasi wao.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali
wakiwemo wa dini, vyamavya siasa, wafanyabiashara, asasi zisizo za kiserikali,
wazee wa kimila na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Tarime.
No comments:
Post a Comment