Na Mwamvua Mwinyi, Vigwaza
MGOMBEA ubunge wa CCM katika jimbo la Chalinze,
Ridhiwani Kikwete, amesema iwapo atachaguliwa kuwa mbunge, atahakikisha
anasimamia vyema mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Amesema lengo la uamuzi wake huo ni kuondoa kero ya
migogoro baina ya wakulima na wafugaji katika
kata za Vigwaza na Pera, jimboni humo.
Ridhiwani alisema atahakikisha anashirikiana na viongozi
mbalimbali kusimamia matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya wakulima na
wafugaji ili kila mmoja aweze kunufaika kulingana na shughuli yake.
Alisema hayo juzi katika mkutano wa kampeni uliofanyika
Kata ya Vigwaza jimboni humo na kuongeza kuwa, migogoro ya ardhi jimboni humo
itapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Alisema inasikitisha kuona wakulima hawanufaiki kutokana
na mifugo kula mazao yao, ama wafugaji kukosa haki zao, hivyo atahakikisha
anasimamia kumaliza tatizo hilo.
Hata hivyo, alisema alishafanikiwa kupunguza tatizo hilo,
hivyo lengo lake ni kulimaliza kabisa.
Katibu CCM wilaya ya Bagamoyo, Kombo Kamote, alisema
kiongozi mwenye uwezo wa kushughulikia matatizo ya wananchi wa Chalinze ni
Ridhiwani, hivyo aliwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono ili aweze
kuliongoza jimbo hilo.
Alisema Ridhiwani amefanya mambo makubwa katika jimbo
hilo kwa kipindi kifupi, hivyo anaamini katika kipindi cha miaka mitano ijayo
atafanya mambo mengi zaidi.
Mgombea wa udiwani wa Kata ya Vigwaza, Muhsin Baruani,
alisema iwapo atachaguliwa, atasimamia sheria na kudhibiti migogoro ya ardhi
ambayo, kwa Vigwaza ni tatizo kubwa.
No comments:
Post a Comment