Wednesday, 11 November 2015

BALOZI EU: USHINDI WA DK. MAGUFULI HAUNA MIZENGWE



NA SULEIMAN JONGO
JUMUIA ya Ulaya (EU), imepongeza uchaguzi mkuu wa Tanzania na ushindi wa Rais Dk. John Magufuli na kusema hauna mizengwe, ndio mana hakuna chama wala taasisi yoyote iliyochukua hatua za kisheria kuupinga.
Aidha, imetaka kuchukuliwa hatua sahihi na kwa wakati kuhakikisha uchaguzi wa Zanzibar unafanyiwa kazi ili kupatikana viongozi watakaounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na wamiliki, wahariri na wadau mbalimbali wa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam jana, Balozi wa EU anayemaliza muda wake hapa nchini, Filiberto Sebregondi, alisema ushindi wa CCM katika uchaguzi huo hususan Tanzania Bara, unaonekana kuridhiwa na wadau wote.
Balozi Sebregondi alisema kupitia uchaguzi huo mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, Tanzania imeonyesha mfano mzuri kwa ukomavu wa kidemokrasia.
Alisema ni vyema ukomavu huo ukaendelezwa kwa ajili ya kuwa taifa bora zaidi kulingana na mabadiliko yanayoendelea kuingia katika jamii.
Hata hivyo, Balozi Sebregondi alisema ni vyema mamlaka husika zikachukua hatua za haraka na stahili  kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, ambao matokeo yake yalifutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), baada ya kundua kuwepo kwa udanganyifu.
Alisema ili kuleta sura kamili ya ukomavu wa kidemokrasia hapa nchini, ni vyema mamlaka husika zikafanya kila liwezekanalo hadi pale Zanzibar itakapopata viongozi wake kidemokrasia.
“Suala la Zanzibar lipo mikononi mwa mamlaka zinazohusika. Tunaamini zinatambua umuhimu wa uchaguzi huo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo juhudi zitafanyika hadi pale visiwa hivyo vitakapopata viongozi wake,” alisema.
Kwa mujibu wa bolozi huyo aliyetumia hafla hiyo ya chakula cha mchana kuagana na wadau wa habari hapa nchini, alisema katika kipindi cha miaka minne aliyoiwakilisha EU hapa nchini, ameshuhudia mambo mbalimbali yenye kuridhisha.

UKUAJI WA DEMOKRASIA
Alisema kabla  ya kuja nchini, alikuwa akifahamu kuhusu uwepo wa demokrasia nchini Tanzania, lakini ikilinganishwa na miaka ya nyuma, eneo hilo limeendelea kuimarika na kutoa faraja kwa jumuia ya kimataifa.
Sebregondi alisema kutokana na ukomavu wa kidemokrasia , nchi itaendelea kuimarika na kwamba anaamini Tanzania itapiga hatua kubwa zaidi.

UGUNDUZI WA GESI
Akizungumzia ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi katika Pwani ya Kusini mwa Tanzania, hususan mkoani Mtwara, alisema EU inapongeza uvumilivu na ustahamilivu katika sekta ya gesi, hususan kutoka kwa wananchi walioko kwenye mikoa ilikovumbuliwa.
Balozi Sebregondi alisema licha ya uvumbuzi huo, taasisi mbalimbali zimeendelea kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha rasilimali hiyo inakuwa na manufaa kwa jamii.
Hata hivyo, aliiomba serikali kuchukua hatua zaidi kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu gesi ili kila mmoja kuwajibika ipasavyo, badala ya kujenga imani kwamba ugunduzi huo unaweza kumjaza fedha kila mwananchi.
“Tuliiomba na tunaendelea kuiomba serikali kuhakikisha inatoa elimu kwa wananchi kuhakikisha wanashiriki kwa namna tofauti kwenye ukuzaji uchumi na si kujenga imani kwa sekta ya gesi pekee,” alisema.

TANZANIA KUWA MFANO
Akizungumzia ushiriki wa Tanzania kwenye harakati mbalimbali za maendeleo katika eneo la Maziwa Makuu, Balozi Sebregondi alisema inapaswa kuhakikisha siasa za eneo hilo zinazingatia mahitaji ya kidemokrasia.
Alitoa mfano wa hali tete inayoendelea nchini Burundi, ambapo alisema ana imani juhudi zilizofanywa na serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, zitaendelezwa kwa ajili ya kujenga jumuia imara.
“Tunaiomba Tanzania iendelee kuwa mwalimu kwa nchi zingine katika kuhakikisha eneo la Afrika Mashariki na Maziwa Makuu linakuwa ni la kidemokrasia,” alisema.

UKUAJI WA UCHUMI
Kwa upande wa ukuaji wa uchumi, alisema kabla ya kuja nchini, alikuwa na taarifa za kukua na kuimarika kwa uchumi wa nchi.
Hata hivyo, alisema katika miaka yake minne aliyokaa hapa nchini, ameshuhudia kuimarika kwa kasi kwa uchumi na kufanikiwa kupunguza kiwango cha umasikini.
Alisema kutokana na ukuaji huo, amani na utulivu uliopo nchini umekuwa kivutio kikubwa kwa viongozi kutoka mataifa mbalimbali, yakiwemo makubwa, wanaokuja Tanzania kujifunza mambo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment