VIONGOZI na watendaji katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), wameanza kujifungia ili kujipanga upya juu ya namna watakavyotekeleza
majukumu yao na kuboresha utoaji huduma kwa wagonjwa.
Hatua hiyo imetajwa kuwa ni kuhakikisha viongozi na
wafanyakazi wanakwenda na kasi ya utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli na
utekelezaji wa falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa vitendo.
Hayo yamekuja ikiwa ni siku moja baada ya Dk. Magufuli
kufanya ziara ya kushtukiza Hospitali ya Muhimbili, kujionea hali halisi ya
utoaji huduma, ambapo alieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya mambo
aliyoyaona.
Katika ziara yake hiyo hospitalini hapo, Dk. Magufuli
alivunja Bodi ya Muhimbili, ambayo ilishamaliza muda wake na kumng’oa Dk. Hussein
Kidanto, aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa MNH.
Aidha, alimteua Profesa Lawrence Mseru, kaimu nafasi
hiyo kuanzia jana, hatua ambayo imewafurahisha Watanzania wengi, wakiwemo
wagonjwa ambao baadhi walinyanyuka vitandani kumshuhudia.
Jana, UHURU lilitembelea hospitalini hapo kujionea
mambo yanavyokwenda ambapo, ilielezwa kuwa viongozi wa kada mbalimbali walikuwa
wakiendelea na vikao kwa ajili ya kujipanga na kutekeleza maelekezo waliyopewa
na Dk. Magufuli.
Aidha, wakati vigogo hospitalini hapo wakiendelea na
vikao, wafanyakazi wa kada zingine walikuwa wakihaha huku na kule kutoa huduma
kwa wagonjwa huku kila mmoja akiongeza bidii katika kutekeleza majukumu yake.
Hali ya utoaji wa huduma hospitalini hapo ilionekana
kuwa tofauti na siku zingine zilizopita kabla ya Dk. Magufuli kufanya ziara
hospitalini hapo, huku madaktari wakinyooshewa kidole kufanya kazi kwa muda
mfupi na kukimbilia kwenye hospitali binafsi.
“Hapa kuna baadhi ya madaktari wanaondoka kabla ya
wakati na kwenda kutoa huduma katika hospitali binafsi na kuwaacha wagonjwa
wakiwa katika msururu mrefu wa kusubiri kuhudumiwa,” alidai mmoja wa wauguzi
hospitalini hapo.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa wakipatiwa matibabu
hospitalini hapo katika wodi za Mwaisela na Sewahaji, walisema ziara hiyo
itasaidia kuokoa maisha ya baadhi yao kwa kuwa watahudumiwa haraka na kwa
viwango vinavyostahili.
Walisema mgonjwa anaweza kulazwa kwa zaidi ya wiki
mbili bila ya kupatiwa matibabu, kutokana na kuharibika kwa baadhi ya vipimo na
kulazimika kwenda kupima katika hospitali binafsi kwa wenye uwezo.
Mgonjwa mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Chacha,
alisema alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo muda mrefu, lakini
alishindwa kutokana na kuharibika kwa kipimo cha CT-Scan.
Alisema baadhi ya wagonjwa wenye fedha wamekuwa
wakifanyiwa baada ya kwenda kupima kipimo hicho katika hospitali binafsi,
lakini alishindwa kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za vipimo.
Awatu Mbena, ambaye anamuuguza mtoto wake aliyelazwa
hospitalini hapo, alisema ziara ya rais imeudhihirishia umma kwamba kwa sasa
wananchi wote hata wa hali ya chini watahudumiwa vizuri.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa juzi jioni na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
ikimkariri Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ilisema rais
alisikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala
chini.
Pia, alikasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia
vifaa vya kufanyia kazi, ambapo alikuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa
kama vile MRI na CT-Scan zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa,
ilihali mashine kama hizo katika hospitali za binafsi zinafanya kazi na
wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko.
Balozi Sefue pia amesema, Rais Magufuli ametoa wiki
moja na kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili, kwa uongozi mpya wa Muhimbili
kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa, ambazo hazifanyi kazi
zinafanya kazi na kuhudumia wananchi ipasavyo.
Tayari Wizara ya Fedha imetoa sh. bilioni tatu kwa
ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa
magonjwa nchini.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuanzia sasa
hospitali zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe
na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote.
Balozi Sefue pia ametumia nafasi hiyo kuwaagiza
watendaji na viongozi wote katika sehemu za kazi, kuhakikisha wananchi
wanahudumiwa ipasavyo na kazi za umma zinatekelezwa ipasavyo.
No comments:
Post a Comment