Friday, 27 November 2015

TRAFFIKI 157 DAR WAHAMISHWA KAZI


POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam, imewabadilisha kazi wakaguzi saba na askari wa vyeo mbalimbali 157 wa Kikosi cha Usalama Barabarani kutokana na utendaji wao kukosa tija.

Aidha, imesema hatua hiyo ni ya kwanza na kwamba hatua ya pili inakuja wakati wowote baada ya uchunguzi wa kuwabaini askari wanaofanyakazi chini ya kiwango, utakapokamilika.

Kamisha wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleimani Kova alisema hayo jana Dar es Salaam kuwa askari hao wamepangiwa kazi nyingine za kipolisi na kwamba walitilia shaka tabia na mwenendo wao wa utendaji ambao ulionekana si wa kuridhisha.

Pangua pangua hiyo imefanyika ikiwa ni siku chache baada ya gazeti hili kufichua vitendo vya rushwa vinavyofanywa na askari wa usalama barabarani Mkoa wa Pwani, kuegeuza mradi wa kujiingizia kipato badala ya kusimamia majukumu yao ya kiusalama, ambapo tayari polisi wa mkoa huo imewapangua askari hao.

Askari 80 wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Pwani waliondolewa na kupangiwa kazi nyingine za kipolisi, kutokana na kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi.

Pangua pangua kama hiyo ilifanyika Mkoa wa Mbeya ambapo askari kadhaa wa kikosi cha
usalama barabarani walipangiwa kazi zingine, baada ya utendaji wao kutiliwa shaka.

Hata hivyo, Kova alisema utendaji wa askari hao umeonekana si wa kuridhisha na kwamba wanalalamikiwa mara kwa mara na wananchi.

Alisema malalamiko hayo yanatokana na askari hao kuwajibu wananchi lugha chafu na kutengeneza mazingira ya kuombwa na kupokea rushwa. Kova aliwaagiza makamanda wa mikoa yote ya kipolisi ya Dar es Salaam,kufuatilia kwa umakini tabia na mienendo ya askari walio chini yao ili kuhakikisha kero hizo hazijitokezi tena.

Aliwataka polisi kuwapatia wananchi huduma nzuri zitakazolifanya jeshi kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia weledi wa hali ya juu.

“Kuwabadilisha askari hao ni hatua ya kwanza kwani bado uchunguzi unafanyika kwa wale ambao wataendelea kufanyakazi chini ya kiwango,’’ alisema.

Aliwataka watendaji wa Jeshi la Polisi, kufanyakazi kwa bidii ili kuhakikisha wananchi wananufaika na utendaji wa jeshi hilo na kuufanya Mkoa wa Dar es Salaam kuwa salama.

No comments:

Post a Comment