Friday, 27 November 2015

HALI SASA SHWARI Z'BAR, VYAMA VYA SIASA VYAKUBALI UCHAGUZI URUDIWE



HATIMAYE viongozi wa serikali na wa vyama vya siasa Zanzibar, wamefikia makubaliano ya kurudiwa kwa uchaguzi mkuu wa Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao matokeo yake yalifutwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Muafaka huo unakuja wakati kukiwa na mlolongo wa vikao vya maridhiano vyenye nia ya kupatikana suluhu ya mvutano wa kisiasa uliokuwepo visiwani humo, baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Akizungumza jana na kituo kimoja cha redio cha kimataifa mjini Unguja, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema viongozi wa kisiasa kutoka serikalini na upinzani wamekubaliana uchaguzi mkuu kurudiwa baada ya kuwepo mvutano wa wiki kadhaa sasa.

Alisema kwa pamoja wamefikia makubaliano hayo ambayo awali yalikuwa yakipingwa na baadhi ya vyama vya upinzani hasa chama cha CUF, lakini mpaka sasa uamuzi wa tume ipi itumike kusimamia uchaguzi huo bado haujaafikiwa na viongozi hao.

“Tuko kwenye mazungumzo, imeshakubaliwa uchaguzi urudiwe sasa tunazungumza tume ipi isimamie uchaguzi huo. Haya yote yatazungumzwa baadaye kwa hiyo sina hakika kwamba ni tume ipi itatumika kusimamia uchaguzi huo,” alisema.

Balozi Iddi alisema wengi hawaafiki kuhusu kutumika tena kwa tume ya sasa ya uchaguzi inayoongozwa na Jecha ambaye alifuta matokeo ya awali ya uchaguzi uliopita baada ya kujiridhisha kuwa haukuwa wa haki hasa kwa upande wa Pemba.

“Wengi wanasema tume hii haifai, hivyo tupate tume mpya haya yote tutayazungumza kwa kuwa tuko pande mbili lazima tukubaliane na kwa mazungumza haya muafaka utapatikana,” alisema.

Alisema uchaguzi utafanyika Tarehe itakayokubaliwa kwenye vikao vya mazungumzo vinavyoendelea na kwamba maofisa wa ZEC, waliochangia kuvuruga uhalali wa uchaguzi uliopita watawajibishwa kisheria.

“Wale maofisa wote wa tume waliovuruga uchaguzi kwa sababu zao binafsi watashughulikiwa kisheria, nadhani

polisi wameshaanza kazi yao kwa sababu wamesababisha hasara kubwa kwa serikali,” alisema.

Alisema Wazanzibari ni waelewa waliweza kupuuza propaganda za baadhi ya wanasiasa kuwa Rais Ali Mohammed Shein, alitakiwa kuachia madaraka Novemba 2 mwaka huu, madai ambayo hayana ukweli.

Balozi Iddi alisema Rais Shein anaendelea kuongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar kifungu cha 28 (1), kinachobainisha kuwa Rais aliyeko madarakani atafikia ukomo wake wa uongozi pale ambapo Rais mwingine atachaguliwa na kuapishwa.

“Rais Shein yuko madarakani kikatiba, Wazanzibari wameendelea kuwa watulivu kwa kuwapuuza waliokuwa wakijaribu kuwapotosha kwa kuwa wana akili na serikali ilikuwa makini kuwaambia kila kitu kwa usahihi, haikukurupuka,” alisema.

AZIONYA JUMUIA ZA KIMATAIFA

Balozi Iddi alisema baadhi ya jumuia za kimataifa zinapenda kuona nchi zinazoendelea zinakosa amani, lakini nia hiyo imeshindikana kwa Zanzibar kutokana na mshikamano uliojengwa visiwani humo kwa muda mrefu.

Alisema jumuia hizo hazipaswi kuingilia suala la Zanzibar kwa kuwa ni nchi yenye uwezo wa kujisimamia mambo yake ambapo kwa kuwahakikishia waliweza kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa bila uwepo wa waangalizi wa kimataifa.

“Serikali ya umoja wa kitaifa imekuja tulikaa tukaona tu kuwa ipo haja wa kuwepo kwa serikali ya aina hii tukafanya na hakukuwa na taifa lolote la nje lililokuja kutusaidia,” alisema.

Aliongeza hata kwenye uchaguzi uliopita SMZ iliweza kutumia fedha zake za ndani kufanya uchaguzi huo kiasi ambacho hakikuwa na chembe ya fedha za wafadhili.



“Tunajisifu kuna mambo tunaweza kujisimamia uchaguzi uliopita tumetumia fedha zetu na huu ujao tutaweza kwa kuwa Waswahili wanasema ng’ombe hashindwi na nundu yake na demokrasia haina gharama.

Tutatumia gharama zozote zile kuendeleza demokrasia, hivyo tunaviomba vyombo vya kimataifa na jumuia zake zisilete chokochoko, wasituonee kwa kuwa wanatuona sisi masikini,” alisema Balozi Iddi.

Alisema kwenye uchaguzi uliopita ambao waaangalizi wa kimataifa walisema ulikuwa wa huru na haki, walisema uongo kwa kuwa hakuna mwanagalizi aliyefika Pemba bali waliandika ripoti ya uongo kwa kuwa hakukuwa na vurugu wala machafuko.

“Hapa walikuja waangalizi wakasema uchaguzi ulikuwa huru na haki, lakini hawakufika Pemba, kwanini. Na kule ndiko uchaguzi ulivurugika na kuharibikazaidi kutokana na udanganyifu mkubwa, wangeweza vipi kuona yaliyoendelea wakati hawakuwepo. Waliandika ripoti ya uongo,” alisema.

Aliwataka Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu wakisubiri vikao vya makubaliano vikamilike kwa kuwa hali ya Zanzibar ni shwari kutokana na nia ya SMZ ya kulitatua suala hilo kwa amani na utulivu.

Oktoba 28, mwaka huu, ZEC ilitangaza kufuta matokeo na uchaguzi mkuu wa Zanzibar kutokana na matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi huo.

Jecha alitoa tangazo hilo kwa njia ya televisheni ambapo alisema sababu kuu ni matatizo ndani ya tume yenyewe na pia katika vituo vya kupigia kura hasa kisiwani Pemba.

Hata hivyo, tangazo la kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi ya Zanzibar limechapishwa kwenye gazeti la Serikali ya Mapinzuzi ya Zanzibar na kulifanya tangazo hilo kuwa sheria.

No comments:

Post a Comment