Friday, 4 December 2015

MAKONTENA TISA YAKAMATWA DAR


MAKONTENA tisa yaliyokamatwa jijini Dar es Salaam, juzi, yalibainika kubeba vyuma kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha nguo Bagamoyo.

Hata hivyo, imebainika kuwa makontena hayo yaliondolewa kwenye bandari kavu ya Kampuni ya PMM Estate (2001), saa 4:00 usiku.

Imeelezwa kuwa, makontena hayo yaliruhusiwa kutoka Septemba 17, mwaka huu, lakini yaliondolewa Novemba 30, mwaka huu na kupelekwa katika eneo tofauti na lililoelekezwa kwenye nyaraka za mzigo huo.

Aidha imedaiwa kuwa, baadhi ya wamiliki wa bandari kavu wanatumia mwanya wa kutofanyakazi saa 24 kwa maofi sa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwenye bandari kavu, kutorosha mizigo iliyopaswa kulipiwa ushuru.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema jana kuwa bado wanaendelea na upakuaji wa mizigo kwenye makontena hayo, ili kubaini uhalali wake na kama imelipiwa kodi stahiki.

Alisema, juzi usiku makontena hayo yalifunguliwa na kukutwa na machuma yanayotumika kutengenezea kiwanda na kwamba bado yana utata kutokana na namna yalivyotumika kusafi rishwa.

“Nyaraka zinaonyesha makontena hayo yalitakiwa kupelekwa bandari kavu ya EPZ iliyoko Ubungo, lakini kwanini yapelekwe Mbezi? Tena kwa kusafi rishwa usiku,” alihoji Kayombo.

Kutokana na utata huo, Uhuru,ilimtafuta, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Heritage Mpire, Beatus Kaboja, ambaye alisema waliiomba kampuni ya PMM kuyahifadhi makontena hayo kutokana na eneo la ujenzi wa kiwanda kutokamilika.

Alisema vifaa vilivyopo kwenye makontena hayo vitatumika kujenga kiwanda cha nguo, Bagamoyo, mkoani Pwani, lakini bado mkandarasi hajakamilisha eneo la ujenzi, hivyo wakaamua kutoyapeleka makontena hayo kwenye eneo hilo.

Kaboja alisema kampuni hiyo haikufahamu kama makontena hayo yamepelekwa katika eneo hilo hadi walipopigiwa simu na wakala.

Akizungumzia endapo sakata hilo limehusishwa na vitendo vya rushwa, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, (TAKUKURU), Edward Hosea, alisema suala hilo bado liko mikononi mwa polisi.

Alisema TAKUKURU wanasubiria taarifa kutoka kwa polisi ili waweze kuchukua hatua zaidi.

Makontena yaliyokamatwa yaliondolewa juzi kwenye bandari kavu ya PMM iliyoko Vingunguti , Dar es Salaam, ambako ilibainika kuwa yanamilikiwa na kampuni ya Heritage Mpire, yenye namba za usajili 116536501, huku wakala wake akiwa ni Kampuni ya NIPOC Afrika Limited, yenye namba ya mlipakodi 105595367.

Polisi wanawashikilia madereva pamoja na malori matatu yaliyohusika kuyasafi risha.

Kufuatia kuibuliwa kwa wizi huo, wananchi wa kanda ya Ziwa, wameiomba Serikali kufanya ukaguzi kwenye vituo vya forodha, hususan vya Sirari, Lusumo , Mtukula , Holoholo ,Uriri, Namanga   na Tunduma kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukwepaji kodi.

Inadaiwa, baadhi ya maofi sa wa forodha wanaoshirikiana na wafanyabiashara kuwagongea mihuri bila ya kuona magari wala bidhaa zinazosafi rishwa kwenda nje ya nchi.

Wakizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina yao, walisema kuna mtandao mkubwa wa wafanyabiashara wakishirikiana na baadhi ya watumishi kusafi risha makontena yenye bidhaa zinazotoka Bandarini ya Dar es Salaam kinyume na sheria.

Bidhaa hizo ni mafuta ya petroli, vipuri vya magari, nguo, vipuri vya pikipiki pamoja na vifaa vya ofi si.

No comments:

Post a Comment