Friday, 4 December 2015

ATAKAYEIHUJUMU CCM KUKIONA CHA MOTO



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakitamwonea haya yeyote atakayethibitika kukihujumu kwa namna moja ama nyingine.

Hayo yalisemwa jana na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula alipokuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wanachama wa wilaya ya Tanga.

Wanachama hao walisafiri kutoka wilayani Tanga kwa lengo la kuwaomba viongozi wawachukulie hatua wote waliosababisha jimbo la Tanga Mjini kuchukuliwa na upinzani.

Mangula aliwapongeza na kuwashukuru wanachama hao kwa moyo na upendo kwa chama, hivyo atatuma kamati yake ya wataalamu kwenda kufanya uchunguzi na atakayethibitika, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Alisema ataungana na wanachama hao katika kuhakikisha hatua zinachukuliwa kwa watakaothibitika kukihujumu chama.

“Kiongozi atakayethibitika kuwa ni msaliti atashughulikiwa kwa mujibu wa kanuni za chama, kwani hakuna anayeogopwa na hatuwezi kucheka na mtu wa namna hiyo,” alisema.

Mangula alisema fedha zinawapa shida sana kwa sababu kuna baadhi ya watu walijirahisisha kwa kujifanya bidhaa na kukubali kudhalilika.

Awali kiongozi wa wanachama hao, Frank Mhando alisema viongozi wa chama wa wilaya, wakiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Kassim Kisauji hawawataki kwa kuwa walikihujumu chama.

Alisema Kisauji kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Wilaya, Kassim Mbuguni na Katibu Lucia Mwilu, walikihujumu chama kwa kusaidiana na watumishi wa serikali na ofi si ya mkurugenzi wa halmashauri.

Mhando alisema wana ushahidi wa Kisauji kushiriki katika vikao vya wapinzani na kwamba alikuwa akitumika katika kugawa fedha ili chama kianguke.

Alisema licha ya kutoa taarifa kwa viongozi mbalimbali, hakuna hatua zilizochukuliwa, hivyo walimwomba Mangula ahakikishe kundi hilo linaondolewa, ili wabaki watu safi na wenye nia ya dhati ya kukitumikia chama.

No comments:

Post a Comment