Thursday 7 January 2016

HOSPITALI BINAFSI KUTOPATA GAWIO LA NHIF KWA VIPIMO




SERIKALI imepiga marufuku hospitali binafsi zinazotoa huduma za vipimo, kupata gawio la malipo kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwa wagonjwa wanaoagizwa na hospitali za serikali kwenda kupima katika hospitali hizo.
Aidha, imeiagiza ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutoa orodha ya dawa zote za asili, ambazo zimethibitishwa katika ofisi hiyo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla, alitoa agizo hilo juzi, wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Taasisi ya  Kansa ya Ocean Road  na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Akiwa katika Hospitali ya Ocean Road, Dk. Kigwangalla alibaini kuwepo kwa ulaghai wanaofanyiwa wagonjwa wanapotumwa kutoka hospitali za serikali kwenda kupima katika hospitali za watu binafasi, ambapo zimekuwa zikiwaongezea idadi kubwa ya vipimo ili kunufaika na makato ya NHIF.
Dk. Kigwangalla alisema hospitali za watu binafsi zinapopokea wagonjwa walioagizwa na  hospitali  za serikali kupata vipimo, ni lazima zitekeleze maagizo yaliyotolewa na daktari na  sio kwenda kinyume.
Katika hatua nyingine, Dk. Kigwangalla aliuagiza uongozi wa taasisi hiyo kumuorodheshea changamoto zote muhimu ili kuzitafutia ufumbuzi.
Miongoni mwa changamoto hizo ni ununuzi wa mashine za vipimo na tiba za kansa, ikiwemo PECT, yenye uwezo  wa kuzalisha kemikali za kutibu maradhi ya kansa, ambapo hivi sasa taasisi hiyo inaagiza kemikali hizo  kutoka Afrika Kusini.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Julius Mwaiselange, alisema taasisi ina uwezo wa kutibu wagonjwa 180 hadi 200, kwa siku na kwamba hivi sasa wanatibu wagonjwa180 kutokana na ukosefu, uchakavu na kuharibika mara kwa mara kwa mashine za tiba na vipimo.
Akiwa katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Kigwangalla, alimuagiza Mkemia Mkuu, Profesa Samwel Manyelle, kuwasilisha orodha ya dawa zote za tiba mbadala zilizothibitishwa ili kuwabana na kuwachukulia hatua watengenezaji holela wa dawa hizo.
Hata hivyo, aliitaka ofisi hiyo kuwa na hifadhi ya kutosha ya kumbukumbu kwa njia ya teknolojia ili kurahisisha  utendaji wake.
Kwa upande wake, Profesa Manyelle alimueleza Dk. Kigwangalla kuwa, ofisi hiyo iko katika hatua ya kuboresha huduma zake ili ziweze kukidhi mahitaji ya wananchi.

No comments:

Post a Comment