Saturday 30 January 2016

MAHAKAMA YAMWACHIA HURU BOSI WA RITA



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemwachia huru aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufi lisi na Udhamini (RITA), Philip Saliboko, baada ya kumuona hana hatia katika tuhuma za kupokea sh.milioni 40.4 kutoka kwa Mkurugenzi wa zamani wa IPTL, James Rugemalira.

Imesema kwa mujibu wa Sheria za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mtoa rushwa na mpokea rushwa wote ni wakosaji, hivyo kwa maoni ya mahakama hiyo kama kweli fedha hiyo ilikuwa rushwa kwa nini Rugemalira hakuletwa mahakamani kushitakiwa maana ni mtoaji.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alisema kwa maoni ya mahakama kesi hiyo ilipelekwa kabla haijaiva katika upelelezi wake. Mahakama inaona upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi bila ya shaka. Mshitakiwa (Saliboko) hana hatia, anaachiliwa huru na mna haki ya kukata rufani kwa upande ambao haujaridhika,î alisema Hakimu Simba alipokuwa akisoma hukumu hiyo.

Alisema mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka kwa mara ya kwanza alikana na kwamba wakati wa usikilizwaji upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Dennis Lekayo, ulipeleka mashahidi watatu ambao ni mpelelezi mkuu na maofi sa wawili wa Benki ya Mkombozi iliyoko Ilala, Dar es Salaam.

Pia, alisema mshitakiwa ambaye anatetewa na Wakili Jamhuri Johnson, alijitetea mwenyewe baada ya mahakama kumuona ana kesi ya kujibu. Hakimu Simba alisema shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri alikuwa Mpelelezi Mkuu Emmanuel Korosso, ambaye alieleza kwamba alikabidhiwa jalada afanye upelelezi juu ya tuhuma za Saliboko Oktoba 9, mwaka 2014 na Mkurugenzi wa TAKUKURU.

Akichambua ushahidi wake, Hakimu Simba alisema shahidi huyo alieleza alikusanya hati mbalimbali na kuhoji watu na alijitosheleza fedha hizo ziliingizwa katika akaunti ya Saliboko na kwamba mshitakiwa huyo hakuwa na maelezo mazuri kuonyesha namna gani alipokea fedha hizo.

Hakimu huyo alisema mashahidi wawili kutoka Benki ya Mkombozi, walithibitisha Saliboko alienda kufungua akaunti kama mteja wao na fedha hizo ziliingizwa katika akaunti ya mshitakiwa huyo na alizitoa mara tatu.

Kwa upande wa utetezi wa mshitakiwa Saliboko, alikubali kufungua akaunti katika Benki ya Mkombozi na kuingiziwa fedha hizo na Rugemalira ambaye alikuwa na makubaliano naye ya kumtafutia shamba katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam ili aendeleze biashara zake.

Baada ya kuchambua ushahidi huo, Hakimu Simba alisema utaratibu wa sheria ni kwamba upande wa Jamhuri ndio wenye wajibu wa kuthibitisha mashitaka pasi kuacha shaka yoyote na si jukumu la mshitakiwa kuthibitisha kwamba hajafanya kosa.

ìKatika kesi hii, hakuna ubishi kwa upande wa Jamhuri na ule wa utetezi kwamba fedha ziliingizwa katika akaunti ya Saliboko, hivyo hakukuwa na ulazima wa kuwaleta wale mashahidi wawili kutoka Benki ya Mkombozi.

ìShahidi muhimu aliyebaki ni mpelelezi mkuu ambaye alipohojiwa na wakili wa utetezi, alidai hakuna siku hata moja alienda kumuuliza Rugemalira fedha ziliingia katika akaunti ya Saliboko kwa kazi gani.

Kwa mujibu wa sheria za TAKUKURU, mtoa rushwa na mpokea rushwa wote ni wakosaji, kama kweli ilikuwa rushwa kwa nini Rugemarila hakuletwa mahakamani kushitakiwa maana ni mtoaji,î alisema hakimu huyo.

Baada ya hakimu kutamka kusoma hukumu hiyo, Saliboko aliweka mikono mdomoni na baada ya kutoka nje alimkumbatia wakili wake kwa furaha. Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Saliboko anadaiwa kuwa Februari 5, mwaka 2014 katika Benki ya Mkombozi, iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam, akiwa Mkuu wa RITA, alipokea sh. milioni 40.4 kupitia akaunti ya VIP Engineering ya Rugemalira ambaye alikuwa Mkurugenzi wa IPTL.

Ilidaiwa alipokea fedha hizo kutokana na kazi yake kama bosi wa RITA wakati IPTL ilikuwa mufi lisi na yeye alishughulikia hilo.

No comments:

Post a Comment