Sunday 27 March 2016

DK. MWAKYEMBE ASITISHA USAJILI WA WADHAMINI




WAZIRI wa Katiba na Sheria Dk. Harrison Mwakyembe, ameuagiza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kusitisha mara moja usajili mpya wa wadhamini wa asasi, vyama, misikiti na vikundi mbalimbali vya kijamii.
Amesema amefikia uamuzi huo kwa lengo la kufanya uhakiki wa uhalali wa kuwepo kwa taasisi hizo kisheria.
Pia, ameagiza kuwa uhakiki huo ukamilike ndani ya miezi mitatu (siku 90), kuanzia sasa na orodha kamili ya wadhamini ikiwa ni pamoja na picha zao, anuani za posta na makazi na taarifa nyingine muhimu za utambuzi wa taasisi hizo mahali zilipo.
Alisema taarifa hizo ziwasilishwe RITA na nakala zipelekwe wizarani kwa uhakiki na kumbukumbu.
Waziri Mwakyembe alitoa agizo hilo jana, alipokutana na watendaji na uongozi wa Bodi ya RITA, kwa lengo la kuboresha utendaji wa wakala, lengo likiwa kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano.
RITA ina zaidi ya wadhamini 5,000, walio kwenye vitabu vyao vya usajili.
Wakati huo huo, Waziri Dk. Mwakyembe ameitisha kikao wiki ijayo cha mamlaka zote zinazohusika na usajili wa vikundi vya kijamii, mashirika, kampuni na asasi mbalimbali.
Alisema lengo la kikao hicho ni kuimarisha taratibu za usajili na uendeshaji na kuboresha mawasiliano baina ya vyombo vya usajili vya dola ili kulinda maslahi mapana ya taifa.

No comments:

Post a Comment