Sunday 27 March 2016

RITA KABATI, OLIVER WAUKWAA UBUNGE WA VITI MAALUMU CCM



CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeongeza idadi ya wabunge wake wa viti maalumu kutoka 64 hadi 66.

Idadi hiyo imeongezeka baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuwateua Ritha Kabati na Oliver Semuguruka kuwa wabunge wa viti maalumu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema tume yake imeteua wabunge wa viti maalumu watatu, wakiwemo wawili wa CCM na mmoja wa CHADEMA na kukamilisha uteuzi wake.

Jaji Lubuva alisema Novemba 11, mwaka huu, baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, tume ilipaswa kutangaza uteuzi wa wabunge wa viti maalumu 113, lakini ilishindwa kukamilisha idadi hiyo, kutokana na baadhi ya majimbo kushindwa kufanya uchaguzi.

Alisema baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa majimbo manane, vyama vya CCM, CHADEMA na CUF vilipata asilimia tano ya kura zote halali za ubunge, hivyo kupata uhalali wa kuendelea kufanyiwa mchakato wa viti vitatu vilivyobaki.

Mwenyekiti huyo wa NEC alisema, jumla ya kura zote halali za ubunge ilizopata CCM ni 8,495,488, CHADEMA ilipata kura 4,720,881 na CUF ilipata kura 1,274,911.

Lubuva alisema kwa idadi hiyo ya kura, CUF itaendelea kubakiwa na viti maalum 10, wakati CHADEMA imeongeza mbunge mmoja wa viti maalumu na hivyo  kutoka wabunge36 wa awali na kuwa 37.

Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, NEC imefanya uteuzi kwa kufuata mtiririko wa orodha iliyowasilishwa na makatibu wa vyama  husika vya siasa vilivyoshiriki kwenye uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa sheria za NEC, chama chenye asilimia tano ya wabunge wa kuchaguliwa, ndicho kinachopata sifa ya kuwa na wabunge wa viti maalumu.

No comments:

Post a Comment