Sunday 27 March 2016

TUMBUA MAJIPU YABISHA TENA HODI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, MKURUGENZI MKUU MISITU, WAKUU WA KANDA WASIMAMISHWA




RUNGU la tumbua tumbua majipu la serikali ya awamu ya tano limehamia Wizara ya Maliasili na Utalii, ambako watendaji wakuu, wakiwemo wakurugenzi wa Idara ya misitu na wanyamapori wameangukiwa na rungu hilo.   
Hatua hiyo imekuja baada ya rungu hilo kutembea kwenye wizara na idara kadhaa, tangu serikali ilipoanza kazi rasmi, Novemba 5, mwaka jana na kusababisha utendaji wenye kuzingatia weledi na maadili ya utumishi wa umma.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe,  jana alitangaza kuwasimamisha kazi  Mtendaji  Mkuu  wa Wakala wa Huduma za Misitu Nchini (TFS), Juma Mgoo na wakurugenzi wawili  wa wakala  huo.
Wakurugenzi hao ni Zawadi Mbwambo, ambaye alikuwa Mkurugenzi Rasilimali Misitu na Kaimu Mkurugenzi  wa Mipango, Matumizi na Uendelezaji wa Misitu, Nurdin Chamuya, ambao wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi kutokana na  ukusanyaji usioridhisha wa mapato yatokanayo na mazao ya misitu.
Aidha, rungu hilo limewaangukia wakuu wa kanda za wakala wa huduma za misitu  nchi nzima,  ambao ni Hubert Haule wa Kanda ya Kusini na  Bakari Rashidi wa Kanda ya Mashariki.
Wengine ni Shabani Mwinyi Juma wa Kanda ya Kati, Emmanuel Minja wa Kanda ya Magharibi na Bruno Mallya  wa Nyanda za Juu Kusini, ambao wamesimamishwa kutokana na kuwepo wa mapato yasiyoridhisha katika idara hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa Matumizi Endelevu, Dk. Charles Mulokozi, pia amesimamishwa kazi kwa kosa la kukaidi agizo la kutosaini vibali vya kusafirisha wanyamapori nje ya nchi.
Alisema amechukua hatua hiyo baada ya juzi, nyani 61, kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kubainika kuwa, Idara ya Wanyamapori ilitoa kibali cha kusafirisha nyani hao, kikiwa kimetiwa saini na mkurugenzi huyo.
Waziri Maghembe alisema ndege kutoka Ulaya iliyotakiwa kusafirisha nyani hao, imeshikiliwa pamoja na rubani wake kwa ajili ya kuhojiwa.
Taarifa zaidi zilizopatikana zimeeleza kuwa nyani 450, ndio waliokuwa wanawindwa kwa ajili ya kusafirishwa.
Katika kikao chake na waaandishi wa habari, Profesa Maghembe alifafanua zaidi kuwa kwa upande wa Idara ya Misitu, alibaini fedha zitokanazo na makusanyo ya mazao ya misitu zimekuwa hazipelekwi benki kwa wakati na hata zikipelekwa, huwa pungufu na kile kilichokusanywa.
Alisema siku chache zilizopita alipata taarifa zilizobainisha kuwa, shehena kubwa ya magogo ya miti aina ya mninga mkoani Rukwa, yalikatwa na kuwekwa ndani ya makontena msituni.
Alisema magogo hayo pia yalikuwa yametengenezewa nyaraka bandia zinazodaiwa kutoka Zambia, ambazo zilifanya maandalizi ya kusafirishwa kupelekwa China kukamilika.
Waziri Maghembe alisema licha ya magogo hayo kubainika, Wakala wa Misitu haukuchukua hatua yoyote kwa watuhumiwa ili kuonyesha kujali rasilimali za taifa.
Alisema baada ya kubaini hivyo, kulifanyika hila ambapo usiku wa jana, alipata taarifa kuwa  shehena ya magogo hayo yenye thamani  ya sh. milioni 500,  badala ya kupelekwa makao makuu ya wilaya ya Kalambo, yalimwagiwa petroli  na kuchomwa moto.

No comments:

Post a Comment