Sunday 29 May 2016

WAAJIRIWA SERIKALINI WALIOFOJI VYETI KUKIONA CHA MOTO



Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi Prof.Joyce Ndalichako akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati wa majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Na.Aron Msigwa – DODOMA.

Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa kampeni ya
kuwashughulikia na kuwaondoa katika utumishi wa umma watumishi wotewalioajiriwa katika  sekta hiyo  wakitumia vyeti bandia.


Aidha, imewataka watumishi hao waanze kujitathmini na kuanza kujiondoa wenyewe kabla ya kufikiwa na  mabadiliko makubwa ya kusafisha sekta ya elimu na utumishi wa umma yanayokuja nchini. 
 

Kauli hiyo imetolewa Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi Prof.Joyce Ndalichako wakati wa majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
 

Amesema Serikali ya awamu ya tano imejipanga kufanya mabadiliko makubwa katika Sekta ya Elimu nchini ili kuhakikisha kuwa Elimu inayotolewa katika shule, vyuo na taasisi mbalimbali inazalisha wahitimu wenye sifa na ubora kwa maslahi ya Taifa .
 

Amesema katika kulitimiza hilo Serikali itawachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria watendaji wote walioshiriki na wale wanaoendelea kushiriki kwa namna moja au nyingine kukwamisha maendeleo ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na wale waliohusika katika udahili wa wanafunzi wasio na sifa katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Songea.

“Serikali ya awamu ya tano imedhamilia kwa dhati
kabisa kuboresha kiwango cha elimu yetu kwa kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu, naomba niwahakikishie kwamba pale panapohitajika kufanyika mabadiliko tutayafanya bila woga,”amesisitiza.


Amesema katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za elimu hapa nchini, serikali imejipanga kubadilisha mfumo wa elimu ambao umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu na kwamba mabadiliko hayo yatafanyika kwa kuwashirikisha wadau wote wa sekta hiyo.
 

” Tunapotaka kufanya mabadiliko kwenye mfumo wetu wa elimu tumekubali tumekubali kwamba tuna changamoto,  katika changamoto hizi lazima tuwe na mahali pakuanzia hivyo tunapochukua hatua tunaomba Watanzania mtuunge mkono,”
amesisitiza Prof.Ndalichako.


Prof.Ndalichako Amesema lengo la Serikali kupitia Wizara yake ni kuhakikisha sekta ya elimu inaboreshwa hapa nchini kwa kuendelea kutoa wahitimu bora wanaokidhi vigezo na viwango katika soko la ajira.


Amesisitiza kuwa mkakati wa Serikali ni kuanza kuwafuatilia wahitimu wote wasio na viwango ambao wako katika maeneo mbalimbali ya ajira huku akisisitiza kwamba elimu ya Tanzania ni sawa na kiwanda kinahitaji malighafi nzuri ili kitoe bidhaa bora.


Ameeleza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuvikagua vyuo vyote vinavyotoa elimu ya juu kuona kama vinakidhi sifa na vigezo vya kiutendaji ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wale wote wanaowadanganya wananchi  na kuwapotezea muda vijana wanaowadahili bila kuzingatia sifa.


“Wizara yangu tunaendelea kufanya mawasiliano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tuchukue hatua kwa wote walioichezea sekta hii muhimu, tulichofanya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph kinaendelea kwa vyuo vingine.”
 

Akizungumzia suala la Ada elekezi amefafanua kuwa suala hilo linaendelea kutazamwa kwa umakini mkubwa kwa kuwashirikisha wadau husika wa sekta hiyo kwa kulifanyia utafiti kwa kuzingatia changamoto zinazojitokeza.
 

Ili kukidhi matarajio ya wananchi kuhusu suala la ada
elekezi amesema serikali inaendelea kuchukua hatua kwa kulifanyia utafiti kuliangalia na madaraja ya shule binafsi na kuongeza kuwa serikali itaendelea kutumia taratibu zilizowekwa na Ofisi ya Kamishna wa Elimu nchini.


Amesema Serikali kupitia Ofisi ya Kamishna wa Elimu
inaendelea kulifuatilia kwa karibu suala la ada na michango mingine kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuona kama michango na ada zinazotozwa zinazingatia maslahi ya Taifa.
 

Prof. Ndalichako amebainisha kuwa ukaguzi utakaofanywa katika shule hizo utajielekeza katika kuangalia uhalali wa michango inayotozwa kwa wanafunzi ikiwemo michango ya kila muhula ya majengo, ulinzi na mingineyo ambayo imekuwa kero kwa wananchi.
 

” Kama Serikali hatuwezi kukubali wananchi kuendelea
kutozwa michango ya majengo wakati kigezo kimojawapo cha mtu kuruhusiwa kutoa
elimu ni kuwa na majengo, hili halikubaliki na hatutalifumbia macho,”  amesisitiza Prof.Ndalichako.


Amewataka wananchi kuelewa kwamba serikali kutotoa ada elekezi haina maana kwamba imejitoa kabisa katika kufuatilia masuala ya elimu hapa nchini bali itaendelea kujenga mazingira mazuri ya kuwawezesha watanzania kupata elimu bora kwa gharama nafuu.
 

Kuhusu ujenzi wa maabara amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 12 kwa ajili ya kununulia vifaa vya maabara kwa shule zote 1536 ambazo zimekamilisha ujenzi wa majengo ya maabara kote nchini.
 

Katika hatua nyingine amesema kuwa Serikali katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 itafanya ukaguzi wa vyuo vyote vya Maendeleo ya Jamii kote nchini ili majengo ya vyuo hivyo yaweze kutumika kuanzishia vyuo vya Ufundi Stadi VETA katika wilaya na mikoa ili kuwapatia stadi za kazi vijana waweze kujitegemea kwa kujiajiri wenyewe.
 

Kwa upande wao baadhi ya Wabunge waliopata nafasi ya kuchangia wakati wa Kupitisha Bajeti ya wizara hiyo wameiomba Serikali kuweka mkazo katika usimamizi wa Sekta ya Elimu nchini ili shule, Taasisi na vyuo vya Tanzania vitoe wahitimu wenye ubora kwa maslahi ya Taifa.

Aidha, wameiomba Serikali kupitia Bajeti hiyo itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ukaguzi wa shule, kuboresha maslahi na kulipa madai ya walimu pamoja na kuziimarisha Mamlaka za Udhibiti wa Elimu ili ziweze kutimiza majukumu yao ipasavyo

No comments:

Post a Comment