Monday 30 May 2016

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MIFUKO YA PLASTIKI KUANZIA MWAKANI


SERIKALI imesema kuanzia mwakani ni marufuku utengenezaji, usambazaji, uingizaji na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini, kwa kuwa husababisha mafuriko na athari zingine kubwa za mazingira.

Pia, imesema inakamilisha majadiliano ndani ya serikali na baadaye kuwahusisha wadau kuhusu dhamira ya kupiga marufuku moja kwa moja matumizi ya mifuko hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais(Mazingira na Muungano), January Makamba, alisema mifuko ya plastiki imekuwa changamoto kubwa ya mazingira.

Alisema kwa sehemu kubwa, mifuko hiyo imekuwa ikitolewa bure na kusambaa, kuchafua mandhari na kuziba mifereji, hivyo kusababisha mafuriko na athari nyingine kubwa kwa mazingira.

"Serikali itatoa muda kwa walioajiriwa, kujiajiri na kuwekeza kwenye biashara ya mifuko ya plastiki, kujiandaa kuacha shughuli hizo na itawezesha mazingira ya utengenezaji na upatikanaji wa vifungio mbadala,''alisema.

Kwa mujibu wa January, wametuma wataalamu wa serikali katika nchi zilizofanikiwa kwenye jambo hilo kujifunza namna bora ya kulitekeleza.

Alisema nia ya serikali ni kuweka zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki ndani ya sheria, ambayo inahusu matumizi ya mifuko ya plastiki kufungashia pombe, maarufu kwa jina la viroba.

"Natoa wito kwa watengenezaji, wasambazaji na waagizaji wa mifuko ya plastiki, waanze kujiandaa sasa kwa zuio hili. Katika wiki zijazo, serikali itatoa utaratibu na maelekezo ya tarehe ya kuanza zuio hilo na taratibu nyingine mahususi,''alisema.

Hata hivyo, alisema zuio hilo halitowahusu watengenezaji wa mifuko ya plastiki wanaoiuza nje ya Tanzania, ambao wataendelea kuitengeneza kwa ajili ya soko la nje. 

Akizungumzia kilele cha siku ya mazingira Juni 5, mwaka huu, Waziri January alisema kwa mwaka huu, hakutakuwepo na sherehe za maadhimisho hayo, badala yake wamewaelekeza wakuu wa mikoa, kila mkoa wafanye maadhimisho hayo kwenye maeneo yao.

Alisema serikali imetoa mwongozo kwa mikoa kuhusu utekelezaji wa shughuli zinazolenga kutoa hamasa ya hifadhi ya mazingira, hususan vyanzo vya maji, ambavyo ni muhimu na ni uhai wa kila kiumbe.

"Shughuli za maadhimisho ya siku ya mazingira, ambayo yana kauli mbiu ya tuhifadhi vyanzo vya maji kwa uhai wa taifa letu,   zitaanza Juni mosi na kumalizika siku ya kilele  Juni 5, 2016,''alisema.

Aliwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kuadhimisha siku hiyo kwa kupanda miti kwenye vyanzo vya maji na kuacha kuchoma moto misitu.

No comments:

Post a Comment