Thursday 30 June 2016

CHADEMA WAPOTEZA MBUNGE

MBUNGE Onesmo Nangole (Longido - CHADEMA) amekuwa wa kwanza katika Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupoteza nafasi ya ubunge baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kutengua ubunge wake.

Hukumu hiyo ambayo ilisomwa kwa saa tatu kuanzia saa 3 ;23 asubuhi (jana)  mpaka saa 6 : 20 mchana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Sivangilwa Mwangesi,  alisema mahakama imetengua ubunge huo kutokana na mapungufu mbalimbali siku ya uchaguzi Oktoba 25, mwaka huu.

Aidha alisema baada ya kupitia hoja za pande zote za mleta maombi na mjibu maombi alibaini kwamba kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika chumba cha majumuisho ya kura ambapo mgombea huyo wa CHADEMA alisimama kutoka sehemu aliyokua amekaa na kwenda kwenye meza ya wataalamu wa kompyuta waliokuwa wakijumlisha matokeo.

Alisema alipofika hapo alianza kufanya fujo na kumwaga maji aliyokuwa nayo kwenye chupa yake na kumwagikia katika karatasi za kura na baadhi ya vifaa vya kompyuta ya kujumlisha matokeo.

Jaji Mwangesi alisema baada ya vurugu hiyo, Msimamizi wa Uchaguzi, Filex Kimaro, aliamuru wagombea wote kutoka nje, lakini dakika chache baadaye Nangole aliingia katika chumba hicho na matokeo kutangazwa bila mgombea wa CCM, Steven Kiluswa,  kuwepo.

Pia alisema mahakama ilibaini kuwa fomu namba 21 (C) zilizokuwa zinatumika kujaza kura za madiwani zilioneka kukatwa kwa kalamu na kuandikwa 24 (B) ambazo ni fomu zilizokuwa zinatumika kujaza matokeo ya wabunge ,

Alisema matokeo hayo yaliyokuwa katika fomu namba 21 (C) yalitumika katika mfumo wa kompyuta uliokua unatumika kujaza matokeo ya wabunge ili yaweze kutangazwa kwa wananchi.

“Mahakama imebaini kuwa fomu zenye matokeo ya udiwani 21 (C) zilikatwa kwa kalamu na kuandikwa 24 (C) ambazo ni fomu za ubunge hapa kulikuwa na lengo la kudanganya na kupotosha ukweli juu ya matokeo ya ubunge,” alisema Jaji Mwangesi.

Alisema kufuatia hoja hizo na vurugu zilizofanywa na mgombea wa CHADEMA, mahakama imebaini hakukua na mazigira rafiki katika chumba hicho ya kuweza kuhesabu kura kikamilifu.

Jaji huyo alisema hata msimamizi mkuu wa uchaguzi katika wilaya hiyo,  Kimaro, alikiri kutenda makosa hayo na kusema yalikuwa ni makosa madogo ya kibinadamu kwani alikua amechoka, lakini jaji alisema hayo si makosa  ya kibinadamu.

 Mgombea wa CCM, Kiluswa, aliwasilisha malalamiko tisa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kupitia wanasheria wake, David Haraka, Masumbuko Lamwai, Edmoond Ngemela, ambapo hoja sita zimetupwa na hoja nne zimewapa ushindi.

NJE YA MAHAKAMA

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kaji kubatilisha ubunge huo, Kiluswa alisema anaishukuru mahakama kwa kutenda haki na kwamba ushindi uliopatikana jana si wa kwake ni wananchi wa Longido waliomchagua.

Aidha, alisema anasubiri mchakato ufanyike ndani ya chama na endapo watampa nafasi ya kugombea basi atakua tayari kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wa Longido.

NANGOLE

Kwa upande wa Nangole alionekana kutoamini kilichotokea mahakamani na  kusema mahakama haijamtendea haki na kwamba atakutana na mwanasheria wake, Method Kimomogoro ili wanaone ni jinsi gani ya kukata rufani kwani anaamini alishinda kihalali.

Aidha, kesi hiyo ilivuta hamasa kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Longido ambapo mapema asubuhi magari aina ya noah ambayo hufanya safari zake kati ya Arusha - Namanga yalionekana katika mahakama hiyo yakuwashusha wananchi walifurika katika viwanja vya mahakama hiyo.

Pia, Nangole alifika katika mahakama hiyo na Kiluswa kila mmoja akiwa na wafuasi wake ambapo wana CCM wengi waliwenda wakiwa wamevaa sare za Chama.

Wengine waliohudhuri katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Laizer, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaban Mdoe, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Lengai Ole Sabaya.

WAZIMIA KWA FURAHA

Shahidi wa pili kwa upande wa mleta maombi Isango Kalakala ambaye alitoa ushahidi wa picha na video aliyoipiga kwa simu yake wakati vurugu zinatokea katika chumba cha kura alipandisha mori wa kimasai na kuzimia mahakamini hapo baada ya ubunge wa Nangole kutenguliwa.

Baada ya kuzimia, alibebwa na vijana (morani) wenzake na kupelekwa nje ambapo baada ya saa kadhaa alizinduka na kusema mahakama imetenda haki ba kuwa hicho ndicho kulichomfanya akazimia na kwamba hana tatizo lolote la kiafya,

Licha ya morani huyo, wengine ambao walikuwa wafuasi wa Kiluswa walizimia mahakamani hapo kwa furaha na kupewa huduma ya kwanza na baadaye kuzinduka na kuendelea na shamrashamra za kusherekea ushindi.

Pia kulikuwa na wanawake wengi wa kimasai kutoka wilaya hiyo ambao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumpongeza Kiluswa mara baada ya kutoka mahakamani,

Kesi hiyo imechukua miezi minne ambapo ilianza kutajwa kwa mara ya kwanza katika mahama hiyo, Februari 29, mwaka huu.

Nagole alishawahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha kwa miaka minane  tangu mwaka 2007 mpaka 2015 alipokimbia CCM.

No comments:

Post a Comment