Thursday, 30 June 2016

MAGUFULI AFICHUA MTANDAO HATARI

RAIS Dk. John Magufuli amefichua mtandao hatari wa ufisadi, unaowahusisha baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Wakala wa Serikali wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), pamoja na mfanyabiashara mmoja, ambao ulikuwa ukijingiingizia sh. milioni nane kwa kila dakika moja.

Mtandao huo ulioisababishia serikali hasara ya mamilioni ya shilingi, umekuwa ukijihusisha kughushi risiti za Mashine za Kieletroniki (EFD) kwa kutoza asilimia tano badala ya 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Rais alisema, mfanyabiashara huyo alikuwa akiziuza risiti hizo kwa wafanyabiashara wengine kwa asilimia tano na wakishauza bidhaa zao wanakwenda TRA, kudai malipo ya asilimia 18.

Ufisadi huo ulifichuliwa jana, Ikulu, Dar es Salaam, wakati Dk. Magufuli, alipokuwa akizungumza na wakuu wa mikoa wapya watatu na wakuu wa wilaya wateule.

Alisema kutokana na wizi huo serikali imepoteza kiasi kikubwa cha fedha, lakini mfanyabiashara huyo yupo mikononi mwa serikali na serikali inafuatilia namna ya fedha hizo ziweze kurejeshwa.

“Ni matrilioni ya shilingi serikali imekuwa ikipoteza, lakini kuna mahusiano kati ya mfanyabiashara huyo, BRELA na TRA. Mapato tuliyokua tukiyapoteza ni mengi kuliko tulivyokua tukifikiria, alisisitiza Rais Dk. Magufuli

Hivyo rais, aliwataka wakuu hao kusimamia fedha za serikali ipasavyo, kwenye vituo vyao vya kazi.

Alisisitiza kuwa baadhi ya wakurugenzi wanafikiri fedha zinazopelekwa kwenye halmashauri ni za kwao, wakati ni za serikali hivyo ni muhimu kwa wakuu wa wilaya wakasimamia matumizi sahihi.

“Fedha hizo zitakazopelekwa kwenye halmashauri, mkahakikishe zinatumika kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi kama zinavyoelekeza,” aliongeza.

Pia, Rais Dk. Magufuli alibainisha kuwa katika uteuzi huo hakutaka mbunge kushikilia wadhifa wa mkuu wa wilaya, kwani kila kazi inapaswa kufanywa na mtu mmoja ili kuongeza ufanisi.

Alisema viongozi hao wanapaswa kushirikiana vya kutosha na vyombo vya ulinzi na usalama kwenye shughuli zao za kiutendaji kwa kuwa watapata taarifa za kutosha.

Aidha, alibainisha kuwa nafasi ya mkuu wa wilaya ni kubwa hivyo ana matumaini na wateule hao, hawataiangusha serikali na kusisitiza kuwa walioachwa hawakukidhi vigezo.

“Sitegemei wala kufikiri wakuu wa wilaya kuwa chanzo cha matatizo, hivyo mnapaswa kusimamia ukweli, kutokula rushwa, kuzingatia maadili pasipo ubaguzi kwa kusimamia ahadi zilizopo kwenye Ilani ya CCM,” alisema.

Rais Dk. Magufuli alisisitiza viongozi hao kuwahamasisha wananchi kufanya kazi ili katika kila wilaya kusijitokeze tatizo la njaa.

Alisema jukumu lingine waliokuwa nalo ni kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarika kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za maeneo yao.

Dk. Magufuli, aliwataka kusimamia maendeleo na kuchapakazi kwa maslahi ya wananchi bila kuogopa kejeli wala matusi kwa sababu serikali inawaunga mkono.


JAJI SALOME AWAFUNDA

KAMISHNA wa Tume ya Maadili ya Watumishi wa Umma, Jaji Salome Kaganda, amewataadharisha wakuu wa wilaya wateule kuzingatia maadili, ikiwemo kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi.

Aliwataka wafahamu uwepo wa sheria iliyotungwa kuhusu wanafunzi hivyo ni aibu endapo mkuu wa wilaya akipandishwa kizimbani kwa tuhuma hizo.

Jaji Salome aliyasema hayo jana, Ikulu, Dar es Salaam wakati akizungumza na wakuu wa mikoa na wilaya kabla ya kuwaapisha kiapo cha maadili kwa viongozi wa umma.

Alisema sheria hiyo pamoja na kutoa adhabu ya kifungo cha miaka 30, lakini kwa nafasi hizo za utumishi ni muhimu kutotumia madaraka vibaya.

“Mkuu wa mkoa au wilaya analazimisha kumchukua mwanafunzi na kumlazimu mkuu wa shule kukimbizana nao, nafahamu wengi mlioteuliwa ni vijana, lakini msitumie madaraka yenu vibaya,” Jaji Salome aliwatahadharisha.

Pia aliwataka kutoa taarifa kuhusu zawadi wanazozipokea ili kuzuia mgongano wa maslahi.
Alisema endapo viongozi hao wakipokea zawadi kuanzia sh. laki mbili, wanapaswa kutoa taarifa kwa ofisa masulufu ili azipangie matumizi.

“Inafamika kwamba, pindi kiongozi anapopokea zawadi, basi ni kwa ajili ya wananchi hivyo lazima wazitolee taarifa,” aliongeza.

Aliwakata baada ya kula kiapo hicho, hati za kiapo wanatakiwa kuziweka ukutani kwenye ofisi zao ili kila mwananchi au kiongozi aweze kuiona.

DC MPYA AONDOLEWA

Awali kabla ya tukio hilo, Jaji Salome alimtaka aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Emilly Mtakamulenga, kuondoka ukumbini hapo kutokana na jina lake kuwepo kwenye orodha ya wakuu wa wilaya kimakosa.

Alisema aliyeteuliwa kwenye nafasi hiyo ni Nurdin Hassan Babu, hivyo Mtakamulenga aliondoka ukumbini hapo kabla ya wenzake kuapa kiapo hicho cha maadili.

No comments:

Post a Comment