Friday 1 July 2016

SERIKALI YAPINGA ADHABU ALIYOPEWA ALIYEMTUSI JPM

SERIKALI imewasiliana na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), kuhusu adhabu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha dhidi ya mshitakiwa Isaac Emilly, ambayo ni nyepesi ikilinganishwa na uzito wa shauri lenyewe.

Pia, imewakumbusha waendesha mashitaka nchini wawe macho na waweke mbele weledi na maslahi mapana ya taifa na kamwe wasiyumbishwe na mihemko ya kisiasa katika jamii.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema hayo bungeni, jana, wakati akijibu muongozo ulioombwa na Juma Nkamia (Nchemba-CCM) na kurejewa tena na Livingstone Lusinde (Mtera-CCM), kuhusu amri iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuhusu mshitakiwa huyo.

Alisema mshitakiwa analifanyia siasa suala hilo na hivyo kuligeuza adhabu rafiki aliyopewa kuwa burudani ya kisiasa kwenye mitandao ya kijamii.

“Nimejiridhisha na kilichotokea. Madhara ya mwelekeo huu mpya katika haki jinai, ni kuchochea vitendo zaidi vya ukaidi kwa mamlaka za nchi na hivyo kujenga msingi wa vurugu. Hili halikubaliki katika utawala wa sheria. Mdharau mwiba mguu huota tende,”alisema.

Alisema Juni 8, mwaka huu, kesi hiyo ilianza kusikilizwa ambapo  mshitakiwa alikubali moja kwa moja ushahidi wote uliokusanywa dhidi yake na kukiri kosa hilo, ambapo mahakama ilimtia hatiani na kumpa adhabu.

Dk. Mwakyembe alisema kama ilivyo ada, mahakama ilitaka kujua kama mshitakiwa huyo ni mshitakiwa mzoefu, ndipo wakili wa serikali aliitaarifu mahakama kwamba, hakuwa na rekodi ya kuhukumiwa huko nyuma.

Waziri huyo alisema wakili wa mshitakiwa huyo alijenga hoja kwa kuomba kwamba, mteja wake ni shitaka lake la kwanza, alikiri kosa na kuonyesha ushirikiano mkubwa kwa mamlaka na ana familia inayomtegemea.

Pia, wakili huyo aliomba mambo mawili kwamba, kwa kuwa sheria inaruhusu adhabu ya kulipa faini au kwenda jela, mteja wake apewe adhabu ya kulipa faini badala ya kwenda jela na mshitakiwa alipe faini kwa awamu ndani ya miezi sita.

Hata hivyo, wakili wa serikali hakupiga ombi hilo na kuiachia mahakama ndipo iliamuru mshitakiwa alipe faini ya sh. milioni saba kwa awamu mbili, yaani Julai 8, mwaka huu na Agosti 8, mwaka huu.

Waziri huyo alisema mfumo wa kikatiba unaheshimu mgawanyo wa madaraka kati ya mhimili wa utendaji wa utoaji haki na mhimili wa kutunga sheria.

“Hivyo, maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha hayawezi kurekebishwa au kusahihishwa ila ni kwa kukata rufani au kwa njia ya masahihisho ya mahakama ya juu zaidi,"alisema.

Dk. Mwakyembe alisema masharti ya adhabu yanaonekana mapesi mno ikilinganishwa na uzito wa shauri lenyewe na ni utekelezaji wa hukumu iliyotolewa, usioendana na dhana na dhamira ya adhabu.

Waziri huyo alisema kwa kuwa awamu ya kwanza ya malipo ya faini inaishia Julai 8, mwaka huu na awamu ya pili, amewasiliana na DPP kuhusu suala hilo kwa hatua zaidi ili kulinda dhana na dhamira ya adhabu katika mfumo wa haki jinai.

Dk. Mwakyembe alisema kwa kuwa awamu ya kwanza ya malipo ya faini inaishia Julai 8, mwaka huu na awamu ya pili, amewasiliana na DPP kuhusu suala hilo kwa hatua zaidi ili kulinda dhana na dhamira ya adhabu katika mfumo wa haki jinai.

Alisema  kutokana na hilo, mshitakiwa atajutia kosa lake na wengine wajifunze kutoka kwake, kwani hayawezi kufikiwa kwa mwenendo huo wa kuingiza siasa katika utekelezaji wa hukumu.

Waziri huyo alisema kosa kama hilo lilitokea nchini Kenya, mwaka jana, ambapo mwanafunzi wa Chuo Kikuu nchini humo, Alan Okengo (25), alihukumiwa kifungo cha mwaka moja na kulipa faini ya dola za Marekani 2,000, kwa kumtukana Rais wa Kenya kwenye mitandao ya kijamii.

Dk. Mwakyembe alisema pamoja na umri wake kuwa mdogo, alikuwa hana rekodi ya nyuma na alikuwa mwanafunzi, ambaye hana kipato kuweza kulipa faini kubwa.

“Dhana na dhamira ya adhabu ilibaki palepale, mkosaji ajutie kosa lake asije akarudia tena, jamii ijisikie salama zaidi kutokana na funzo alilopata na wengine wasidiriki kujaribu kutenda kosa kama hilo,”alisema.

Emilly (40), ambaye ni mkazi wa Orasiti mkoani Arusha, Machi 7, mwaka huu, alituma ujumbe wa maneno katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Facebook, akisema ‘Hizi ni siasa za maigizo, alafu mnamlinganisha huyu bwege na Nyerere wapi buana’.

Mshitakiwa huyo kutokana na ujumbe huo, alifikishwa katika mahakama hiyo akikabiliwa na shitaka la kumkashifu Rais Dk. John Magufuli kwa njia ya mtandao.

No comments:

Post a Comment