Friday 1 July 2016

LUKUVI: HATI ZA KIMILA ZIKUBALIKE UTOAJI MIKOPO

SERIKALI imezitaka benki nchini hususani za biashara, kukubali hati za kimila kama dhamana ya mikopo kwa wananchi kwa kuwa ni halali.

Aidha, imeziomba benki hizo kuziamini hati za kimila bila wasiwasi wowote kwa kuwa hazina tofauti yoyote na hati zinazotolewa na serikali.

Serikali pia imeziagiza benki hizo kuongezeka kasi ya utoaji wa hati za umiliki wa sehemu ya jengo (Unit Titles), ikiwemo kuondoa urasimu iwapo upo, kama inavyolalamikiwa na wadau mbalimbali.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alitoa magizo hayo jana, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua warsha ya wadau mbalimbali ya kujadili sheria ya hati ya umiliki wa ardhi.

“Benki zitambue kuwa thamani ya ardhi ni ile ile, iwe hati ya kimila ama ya serikali, na zote ni halali, wasihofu juu ya kurudishiwa fedha watakazowakopesha wananchi, watarudishiwa tu,” alisema.

Waziri Lukuvi aliagiza maofisa wa wizara hiyo wanaohusika na utoaji wa hati za umiliki wa sehemu ya jengo, kuhakikisha iwapo kuna urasimu wa aina yoyote kama inavyolalamikiwa, ili ukome na kutoa haki stahiki.

Alisema tangu kutungwa kwa sheria namba 16 ya mwaka 2008, ni hati 950 pekee ndizo zimetolewa, tena ni kwa mikoa mitatu tu nchini, ambayo ni Dar es Salaam hati (657), Morogoro (45) na Arusha (248).

“Nilipoingia katika wizara hii, nilichunguza ni nini tatizo na kubaini yapo malalamiko mbalimbali kuwa, upo urasimu wizarani juu ya utoaji wa hati hizo. Iwapo ni kweli, naomba suala hilo likome mara moja,” aliagiza Lukuvi.

Aliwataka wadau wa warsha hiyo, kuisuta wizara iwapo wanao ushahidi juu ya urasimu huo, ambapo aliwataka maofisa wa wizara kuondoa vikwazo vilivyopo.

Hata hivyo, alisema vikwazo anavyoviona yeye ni kwa mujibu wa sheria. Aliwataka wadau hao kufuata utaratibu na sheria na si vinginevyo hata kama hawapendi.

Alisisitiza kuwa matarajio ya serikali ya kuanzisha sheria hiyo ni kuwarahisishia wananchi ujenzi kwa kupatiwa mikopo, badala ya kutoa fedha zao mfukoni.

Alisema tatizo alilobaini ni wahusika kusajili majengo badala ya michoro kama sheria inavyoainisha, hivyo aliwataka kuhakikisha wanasajili michoro yenye mpango mzuri wa uendeshaji, ikiwemo miundombinu, maji, ulinzi na maegesho na si kusajili majengo.

No comments:

Post a Comment