Friday 1 July 2016

AMSON GROUP KUJENGA MAJENGO MATATU YA HOSPITALI DAR


KAMPUNI  ya Amsom Group  imejitolea kujenga majengo matatu katika Hospitali za Amana, Temeke na Mwananyamala,  jijini Dar es Salaam, yatakayotumika kwa ajili ya kinamama wanaojifungua.

Ujenzi wa majengo hayo, kila moja likiwa na ghorofa mbili, utakaogharimu zaidi ya sh. bilioni 3.6, unatarajiwa kuanza Agosti, mwaka huu na kukamilika mapema mwakani.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukakibidhiwa ramani ya  majengo hayo, iliyofanyika katika Hospitali ya Amana, jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema serikali mkoani humo inakusudia kumaliza kabisa tatizo la mazingira duni kwa kinamama wanaojifungua.

Alisema ujenzi  wa majengo hayo, yatakayokuwa na wodi za kisasa, utaondoa kabisa tatizo la kinamama  kulala zaidi ya mmoja katika kitanda kimoja.

“Moja ya changamoto kubwa, ambazo mkoa wangu unakumbana nazo ni  idadi ya kinamama wengi kulala chini na hata tunapotafuta magodoro, hatuna mahala pa kuyaweka,”alisema Makonda.

Aliongeza kuwa kufuatia bajeti ndogo ya serikali kuu, serikali ya mkoa iliamua kutafuta njia mbadala ili kukabiliana na changamoto hiyo, ambapo kampuni ya Amsom Group ilijitokeza kusaidia ujenzi huo.

“Lengo letu ni mama mmoja kitanda kimoja. Tunakwenda kuondoa tatizo la kinamama kulala chini, na si tu kulala chini, bali hata kulala kinamama zaidi ya mmoja katika kitanda au godoro moja,”alisema  mkuu huyo wa mkoa.

Meneja Ukuzaji wa Biashara wa Amsom Group, Suleiman  Amour,  alisema kila jengo moja litakuwa na uwezo wa kuchukua wagonjwa  150 kwa wakati mmoja.

Alisema tayari maandalizi yameshafanyanyika, ikiwa ni pamoja na ramani ya  majengo.

“Lengo kuu ni kuisaidia jamii ili nayo iweze kunufaika na biashara tunayoifanya kwa kuwarudhishia kile ambacho  tunakipata. Nia yetu ni  kuisaidia jamii ili nayo ijisikie ni watu wenye kuthaminiwa na kuishi maisha ya kusaidiana,” alisema Amour.

Wakati huo huo, Makonda jana alikabidhi magodoro 100, katika Hospitali ya Amana,  yaliyotolewa na Kampuni ya GSM Foundation kwa ajili ya wagonjwa.

Akikabidhi  magodoro hayo, Meneja  Mkuu wa GSM Foundation, Shanon Kiwamba, alisema lengo ni kuondoa changamoto za mahali pa kulala kwa wagonjwa.

Alisema wamepanga kusambaza magodoro hayo katika hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke.

No comments:

Post a Comment