Monday, 1 August 2016

PENGO AVITAKA VYOMBO VYA HABARI KUWA MAKINI



VYOMBO vya habari vimetakiwa kuwa kiunganishi cha familia badala ya kuzitenganisha kwa kuwa na vipindi vyenye maudhui yanayofaa kwa rika zote.

Hayo yalisemwa jana, Dar es Salaam na Muadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya Radio Maria.

Alisema vyombo vya habari duniani vimekuwa na maudhui yanayozigawa familia na kuipongeza Radio Maria kwa kuwa imekuwa ikizingatia hilo na kuwa kiungo cha familia zote.

Kardinali Pengo alisema Radio Maria imekuwa na vipindi vyenye maudhui, ambayo hukisikilizwa na watu wote, tofauti na vyombo vingine vya habari, ambavyo kwenye baadhi ya vipindi baba anapaswa kuondoka ili kumpisha mtoto aendelee kutazama au kusikiliza.

“Ninaposema vyombo vya habari vinaigawa familia, nina maana ya vipindi, ambavyo vimeviweka kwa siku nzima, ambavyo familia haiwezi kukusanyika pamoja na kuvitazama au kuvisikiliza bila mmoja wa wanafamilia kuondoka au kuzima TV au redio kutokana na ukiukaji wa maadili.

"Kwa mfano, familia inaangalia taarifa ya habari, ghafla ikatokea vikatuni vya picha za ajabu, baba hawezi kuendelea kutazama au hata mtoto mwenye maadili, japo anapenda katuni anaweza kuondoka au kuzima TV,"alisema.

Aidha, alitoa wito kwa Televisheni Maria, ambayo iko njiani kuanzishwa, itakapokuwa hewani kuendana na maudhui ya redio hiyo kwa lengo la kujenga kizazi kilichokuwa na hofu ya Mungu.

Kwa upande wake, Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, alisema ni fahari kuadhimisha miaka 20 ya Radio Maria kwa kuwa imekuwa na mafanikio katika kuuelimisha umma wa Watanzania.

Alisema jamii inatakiwa kuzingatia masuala yanayomhusu Mungu zaidi kuliko mambo ya dunia.

Pia, alisema maadhimisho hayo yamekuwa yakiunganisha wakristo duniani kote, hivyo aliwaomba kutumia fursa hiyo kujifunza zaidi.

No comments:

Post a Comment